SERIKALI YAWACHARUKIA VIONGOZI WA DINI,SASA YATUMIA UBABE WAKE,SOMA HAPA KUJUA
SERIKALI sasa imefungua makucha yake kwa
viongozi wa dini. Hatua hii inatokana na matamko ya viongozi hao ya kuipinga
Katiba inayopendekezwa pamoja na kuchangishana fedha za kumshaiwishi Waziri
Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa agombee urais. Anaandika
Sarafina Lidwino … (endelea).
Kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mathias Chikawe, serikali “imewafunga midomo” viongozi wa dini. Imesema
wamekuwa wakitoa matamko yanayoashiria kungilia masuala ya kisiasa kinyume na
sheria ya vyama, sura 337 na kanuni zake, pamoja na katiba zinazosimamia
uendeshaji wa taasisi hizo.
Amri ya serikali
inakuja wakati ambapo shinikizo la viongozi wa dini limeshika kasi hadi
kuilazimisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuahirisha kura ya maoni iliyokuwa
ifanyike 30 Aprili mwaka huu.
Viongozi wa dini na makundi mengine ya kijamii, wanasema
kulazimisha kura hiyo kungechochea machafuko kwani uandikishaji wa wapigakura
kwa mfumo wa BVR unaoendeshwa na NEC haujakamilika katika mkoa hata mmoja.
Mbali na hilo,
maaskofu wanaounda Jukwaa la Kikristo, walikwenda mbali zaidi katika matamko
yao wakiwataka waumini wao kuipigia kura ya hapana katiba inayopendekezwa kwa
kile walichodai kuwa mchakato wake ulikuwa haramu.
Bila shaka
matamko hayo ndiyo yameikwaza serikali, ingawa haikuwaja moja kwa moja
maaskofu. Lakini waziri Chikawe amesema “Kwa mfano viongozi wa taasisi za dini
wanapokutana na kutoa matamko yanayolenga kuwashawishi waumini wao wafuate
maelekezo yao hususani masuala ya katiba inayopendekezwa au uchaguzi mkuu ujao,
matamshi kama hayo yanakiuka sheria za usajili wa taasisi hizo”.
Amefafanua kuwa
viongozi wa taasisi za dini wana haki ya kushiriki katika masuala ya kisiasa
kama watu binafsi ila ni kinyume cha sheria kutumia uongozi wao kushawishi
waumini wao watekeleze matakwa yao ya kisiasa.
“Aidha, waumini
wa dini mbalimbali wana haki ya kuamini mafundisho ya dini zao lakini wanapaswa
kutekeleza masuala yao ya kisiasa na kijamii kwa utashi wao wenyewe bila ya
kushawishiwa na mtu yeyote, kama sheria za nchi zinavyotaka,” anasema.
Chikawe
ametaja mfano mwingine akisema ni pale kiongozi au viongozi wa dini
wanapochangisha fedha na kuandamana au kukutana na wanasiasa kwa kile
kinachoelezewa kuwa ni kuwashawishi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Pamoja na
kutowataja viongozi husika, bila shaka Chikawe aliwalenga baadhi ya wachungaji
na masheikh kutoka mikoa mbalimbali ambao hivi karibuni walikusanyika kwa
Lowassa na kumchangia fedha wakimwomba agombe urais.
“Serikali inapenda
kuwataka wananchi mmojammoja au vikundi, zikiwemo taasisi za dini kuepuka
kushiriki katika vitendo ambavyo vinaashiria kuvuruga amani na utulivu nchini.
Serikali itachukua hatua za kisheria kudhibiti hali hiyo,” amesema Chikawe.
Ameongeza kuwa
kuanzia wiki ijayo 20 Aprili mwaka huu, wizara yake itaanza kuvifuta vyama
vyote vilivyosajiliwa chini ya sheria ya vyama, sura 337, ambavyo havifuati
matakwa ya kisheria ya kuwasilisha taarifa zao za mwaka za ukaguzi wa hesabu na
kulipa ada za kisheria.
Chanzo ni
Mwanahalisi.oline
No comments
Post a Comment