HIVI NI KWELI WANAFUNZI WA CHUO KIKUU WANAMTAKA LOWASSA?SOMA HAPA KUJUA
Na
Edson Kamukara
KUMBE watoto wa maskini wana fedha. Ni wale tuliozoea kuona wakishinda na kukesha barabarani, wakigoma na kushinikiza serikali iwapatie mikopo ya kugharamia elimu ya juu.
Kama wasingekuwa na fedha, wasingejitokeza na kujipanga kumpelekea fedha tajiri mmoja anayewania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Na kama hawana fedha, basi tuamini kwamba kilichotokea ni magumashi, danganya toto.
Haya ndiyo maajabu yanayoendelea nchini wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015. Makundi mbalimbali wakiwemo wanaojiita wanyonge “maskini” eti wamechangishana fedha na kusafiri hadi kwa Edward Lowassa, Mbunge wa Monduli aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa serikali ya ya nne, kumsihi agombee urais.
Miongoni mwao wamo “wanafunzi wa vyuo mbalimbali nchini.” Tumewaona kwenye vyombo mbalimbali vya habari. Eti wanataka Lowassa agombee urais kwa kuwa ni mwanasiasa jasiri.
Nimekuwa mmoja wa wanavyuo wachache kutoka familia maskini ambao tulikuwa wa kwanza kunufaika na mfumo wa mikopo ya vyuo vikuu, ulipoanzishwa rasmi mwaka 2004/2005 na serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa.
Wakati huo mikopo hiyo ikianza kutolewa Lowassa alikuwa waziri wa kawaida katika serikali ya Mkapa. Sikuwahi kusikia popote alipohusika kusaidia watoto wa maskini wapate mikopo bila matatizo.
Ninachokumbuka ni kwamba muda mfupi baada ya serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2005, Lowassa akiwa Waziri Mkuu, “kasheshe” ya mikopo ilianza vyuoni.
Katika mwaka wetu wa kwanza chuoni, serikali ya Mkapa ilitupatia mkopo kwa asilimia 100 lakini mwaka uliofuata, Lowassa akiwa waziri mkuu, serikali iligeuza utaratibu na kubuni kigezo walichokiita “means test” cha kutoa mikopo hiyo kwa matabaka.
Tabaka la kwanza lilinyimwa mkopo kabisa. Kigezo kilikuwa kwamba watoto hawa wanatoka kwenye familia zinazomudu kugharamia elimu hiyo. Watoto wengi wa maskini waliingizwa kwenye kundi hili, wakashindwa kupata elimu ya juu.
Makundi mengine yalipewa asilimia 20, 40, 60, 80 hadi 100 kulingana na wapangaji wa vigezo walivyomtathmini mwombaji. Hapa ndipo nawashangaa “wasomi” wanaomtaka Lowassa agombee urais.
Hawatuelezi jinsi Lowassa alivyosukuma serikali yake kumaliza mgogoro huo wa mikopo kwa watoto wa maskini. Hakuweza kuzuia vyuo yetu kugeuka sehemu ya migomo na maandamano ya kudai mikopo hadi leo.
Maana wanavyuo wengi walionufaika na mikopo hiyo kwa asilimia 60 hadi 100 walikuwa ni watoto wa matajiri wakiwemo pia watoto wa viongozi. Kwanini wanavyuo wanaompigia debe au kumpinga Lowassa hawatuelezi ujasiri au udhaifu wake katika mchango wa elimu ya juu?
Sasa inashangaza kuona wasomi wetu wa vyuo vikuu wamegeuka bendera na kufuata upepo. Badala ya kuhoji na kutafiti ili wajue zaidi na kuwasaidia wasiojua, wao wamebaki kukaririshwa mambo na wanasiasa kama kasuku.
Nimeandika makala haya nikiwa na mfano hai wa Februari 21, mwaka huu. Nikiwa mmoja wa wahariri katika gazeti la Tanzania Daima, walifika wasichana sita ofisini.
Walionekana kama hawajiamini kwa hoja iliyowaleta. Walijitambulisha kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu tofauti jijini Dar es Salaam wakiwa wanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Walipomaliza kujitambulisha, nikataka kufahamu sababu ya ziara yao. Wakasema wamekuja kutoa tamko lao kumwomba Edward Lowassa agombee urais mwaka huu.
Ujumbe wao ulinishtua kidogo kwa sababu ilikuwa imepita siku moja baada ya “wanaojiita” wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kuandikwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba wanamtaka Lowassa agombee, ingawa kesho yake uongozi wa chuo na serikali ya wanafunzi walidai watoa tamko walikuwa wamejituma.
Kwa kuwa harakati kama hizo za wanavyuo mbalimbali kumpigia debe Lowassa na wagombea wengine ndio kwanza zilikuwa zinaanza kushika kasi, niliwadadisi wale wageni wangu hao “wanavyuo” kuhusu mtazamo wao juu ya huyo wanayempigia chapuo.
Swali langu lilikuwa jepesi; ni kwanini awe Lowassa na si Stephen Wassira, Bernard Membe wala Mizengo Pinda? Nikaona wanatazamana na kutafuna kucha, kisha kiongozi wao akajibu kitoto kabisa akisema, “tunamtaka Lowassa kwa sababu kwa kipindi chote cha miaka 35 ya utumishi wake serikalini amefanya mengi na pia ni jasiri...atatupigania wanavyuo.”
Nilitarajia walau kusikia kati ya hayo mengi aliyoyafanya Lowassa machache yake ni yapi. Hawakusema…jibu lao likabakia lile lile la Lowassa ana maamuzi magumu na jasiri, atatusaidia.
Sikuona sababu ya kupoteza tena muda wangu kuwasikiliza wasomi wa chuo kikuu wasioweza kujenga hoja ya kutetea kile wanachokiamini. Badala yake nikawatafutia mwandishi awasikilize.
Wakiwa kando yangu wanazungumza hoja yao, mara kiongozi wao akapokea simu ambayo ilionesha kuwa na maelekezo ya nini wazungumze. Wakaulizwa wako wapi…wakajibu, kisha wakapewa maelekezo waende chombo gani wakishatoka Tanzania Daima.
Nimeandika haya kuonesha kwamba kwa kiasi fulani “wasomi” wetu wa vyuo vikuu wamepoteza hadhi na heshima ya vyuo kuwa mahala pa kuzalisha fikra na kuisaidia jamii kutambua kilicho bora na sahihi kwa mustakabali wa maisha yao.
Vyuoni ndipo kunapaswa kuwa kitovu cha kuzalisha fikra ya demokrasia pana yenye hoja za kushawishi, lakini badala yake siku hizi, wasomi wetu wengi wameelemewa na siasa za bendera fuata upepo.
Mwanasiasa mmoja akisimama jukwaani na kusema fulani ni fisadi au mtu safi basi kuanzia pale kila mtu anaimba fulani ni fisadi au ni mtu safi, japokuwa hajui ufisadi wa mtuhumiwa au usafi wa huyo anayesifiwa.
Mifano ni mingi. Mwaka 2008 baada ya Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu kwa kashfa ya Richmond, wasomi hawa wa vyuo vikuu ndio walimzomea na kuendesha midahalo wakimwita fisadi.
Viongozi wa dini nao walisikika kila kona wakikemea ufisadi kwa nguvu zote. Lowassa wa watu akanyooshewa vidole kila mahali hata ndani ya chama chake cha CCM akiambiwa ajivue gamba.
Ajabu sasa ni pale alipogeukia nyumba za Mungu na makundi ya kijamii akawaonesha noti kwenye harambee. Ufisadi wake ukaisha. Sasa hatukanwi tena. Sasa anaitwa kiongozi jasiri, mwenye uamuzi mgumu anayefaa kuwa rais wetu.
Hawa watu wako makini kweli? Si wako radhi kufanya lolote mbele ya fedha kama wanaweza kumshangilia “fisadi” wa miaka michache nyuma ili awe “mfalme” wa leo. Iko wapi elimu ya vyuo vyetu?
Ili kumpata rais bora na makini, tunapaswa kujiepusha na mihemko itokanayo na nguvu ya rushwa na ushabiki.
Badala yake mijadala yetu ijikite kwenye hoja makini za kuonesha ama uwezo na upungufu wa yule tunayemjadili badala ya kuchafuliana majina au kupeana sifa za kipuuzi. Tafakari!
SOURCE: GAZETI LA MAWIO

No comments
Post a Comment