EXCLUSIVE-UFISADI WA BILIONI 230 ZA MABEHEWA MABOVU,MAPYA YAIBUKA SOMA HAPA KUJUA
| pichani ni Katibu mkuu Wizara ya Uchukuzi Shaaban Mwinjaka, akiyabokea miongoni mwa mabehewa 200 ambayo ni mabovu na Fullhabari.blogs ulishuhudia kipindi yanaingia nchini |
Sasa yagundulika aliyeleta mabehewa feki alikuwa na bei ya juu
kuliko wote, Aliruhusiwa na kufanyia marekebisho zabuni yake kinyemela
Madudu zaidi yameendelea kuibuka katika sakata
la mabehewa feki 274 yaliyonunuliwa na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), na sasa
imebainika kuwa kampuni iliyopewa zabuni ya kuleta mabehewa hayo ndiyo
iliyokuwa ya bei ya juu zaidi kuliko kampuni 10 zilizokuwa zimeomba na
haikuweka dhamana yoyote kama sheria ya manunuzi inavyotaka.
Aidha,
imebainika pia kuwa ya Hindustan Engineering Ltd ya India, ambayo ilishinda
zabuni hiyo, ilibadilishiwa vigezo (specification), vya aina ya mabehewa
kinyemela baada ya zabuni kutangazwa na wazabuni kuwasilisha maombi yao.
Kwa mujibu wa taarifa
za uhakika ambazo Chanzo changu imezipata, kampuni hiyo iliomba kuiuzia TRL
mabehewa 174 yenye ‘rubber’ badala ya ‘spring’ kwa dola za Marekani
18,209,317.50 (Sh. bilioni 32.8) wakati kampuni ya Baotou Beifang
Chuangye Co. Ltd ya China ilikuwa tayari kuleta idadi hiyo ya mabehewa
yenye viwango vinavyokubalika kwa dola za Marekani 13,907,907 (Sh. bilioni
25).
Kampuni hiyo
pia ilishinda zabuni hiyo ambayo ilihusisha kuleta mabehewa mengine 100 ya
mizigo ambayo ni ya muundo wa matangi (tank wagon) na yasiyofunikwa (flat
wagon) kwa dola za Marekani 10,278,182.50 (Sh. bilioni 18.5) wakati kampuni
ya Baotou Beifang Chuangye Co. Ltd ya China iliyokuwa ndiyo yenye bei
ndogo ilikuwa tayari kuleta idadi hiyo ya mabehewa kwa dola za Marekani
7,272,975 (Sh. bilioni 13.09).
Kampuni hiyo pia
ilishinda zabuni ya kuiuzia TRL vipuri kwa thamani ya dola za Marekani
2,561,187.50 (Sh. bilioni 4.4) baada ya kuirekebisha na taarifa ya zabuni
inaonyesha kuwa iliwasilisha zabuni iliyorekebishwa na ilikubaliwa.'
Kampuni ya
Baotou Beifang Chuangye Co. Ltd iliomba kuleta vipuri hivyo kwa dola za
Marekani 2,475,835 (Sh. bilioni 4.46) wakati kampuni nyingine kama
Transnet iliomba kwa dola za Marekani 3,108,687 (Sh. bilioni 5.6) wakati Modern
Industries iliyoshindwa kwa kutowasilisha dhamana iliomba kwa dola za
Marekani 3,344,925 (Sh. bilioni 6.02).
Kwa ujumla
taarifa zinaonyesha kuwa kampuni ya Hindustan Engineering ililipwa dola za
Marekani 31,048,688 (Sh. bilioni 55.9) wakati kampuni iliyokuwa ya bei
ndogo kuliko zote ingeweza kufanyakazi hiyo kwa dola za Marekani 24,368,757
(Sh. bilioni 43.86) hatua ambayo ingeokoa dola za Marekani 6,677,931 (Sh.
bilioni 12.02) na kutoitumbukiza nchi kwenye hasara hiyo ya mabehewa feki.
“Mabehewa
nyenye rubber hayawezi kabisa kwa namna yoyote ile kupita kwenye reli yetu.
Kilichotokea ni kwamba zabuni iliyotangazwa ilitaka wazabuni walete
mabehewa yenye spring ambayo ndiyo sahihi, lakini baadaye inaonekana
walibadilisha vigezo na kuielekeza kampuni waliyoipa zabuni vigezo vipya
ndiyo maana unaona mabehewa yaliyokuja hayafai,” alisema mmoja wa wataalam
wa reli ambaye hakutaka jina lake litajwe .
Taarifa zaidi
zinaeleza kuwa kampuni ya Hindustan Engineering Ltd haikuweka dhamana yoyote
jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma na ilitaka ilipwe
fedha yote kabla ya kuingiza mabehewa nchini jambo ambalo TRL ilitekeleza.
Wakati mzabuni
huyo akiweka masharti hayo, ka mpuni nyingine zilizoomba ikiwamo iliyokuwa ya bei
ndogo zaidi, iliweka dhamana na ilitaka ilipwe kwa awamu hadi
itakapokamilisha kazi husika.
Taarifa zaidi
zinaeleza kuwa pamoja na kwamba kampuni ya Hindustan Engineering Ltd ilikuwa ya
gharama kubwa iliomba kufanya kazi hiyo kwa miaka miwili, wakati kampuni
nyingine zilizoshindana kwenye zabuni zingeweza kufanya kazi hiyo
kwa miezi tisa hadi mwaka mmoja.
Kampuni ya Hindustan Engineering Ltd haikuweka gharama za
matengenezo wakati kampuni nyingine zote ziliweka.
Taarifa
zinaonyesha kuwa kampuni nyingine zilikosa sifa za kushinda zabuni kwa
kutowasilisha dhamana (bid security), ikiwamo ile ya Modern Industries,
DCD rolling stock ambayo pia iliwasilisha bei zilizokuwa na kasoro za
kiuandishi pamoja na Lucky Export.
Kampuni nyingine
zilizoomba zabuni hiyo ni Caeic Beigin Ltd, CNR Import and Export Corporation
Ltd, Hyunan Construction Engineering Ltd, Texmaco Rail and Engineering na
Transnet.
Taarifa hizo
zimeibuliwa siku sita tu baada ya Alhamisi iliyopita Waziri wa Uchukuzi, Samuel
Sitta, kuwasimamisha kazi vigogo watano wa TRL, akiwamo Mkurugenzi
Mtendaji wake, Kipallo Kisamfu, kutokana tuhuma za kuihujumu serikali katika
sakata la ununuzi wa mabehewa feki 274 ya mizigo na kuisababishia hasara
ya Sh. bilioni 230.
Wengine
waliosimamishwa ni Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile Ngosomiles; Mhasibu
Mkuu, Mbaraka Mchopa; Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiranga na Meneja
Mkuu wa Manunuzi, Ferdinand Soka.
Sitta alisema baada
ya kuwasimamisha vigogo hao, utafanyika uchunguzi dhidi yao kwa wiki tatu
kuanzia wiki iliyopita.
Kufuatia uamuzi
huo, Sitta alimteua aliyekuwa Mhandisi wa TRL, Elias Mshana, kuwa Kaimu
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, na kumwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya
Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka, kusimamia kuundwa kwa kamati ya uchunguzi huo.
Alisema kamati
hiyo itaongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
akishirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika Sekta ya Umma (PPRA) pamoja na Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Sitta
alichukua uamuzi huo baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi ya kamati iliyoundwa
na Waziri aliyemtangulia wizarani hapo, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye
alihamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambayo imegundua kuwako
kuna hujuma mbalimbali katika kuendesha TRL.
Kabla ya
kuchukua uamuzi wa jana, Waziri Sitta aliiagiza bodi ya Wakurugenzi ya Reli
kupitia taarifa hiyo na kutoa maelezo kwake juu ya suala ya ununuzi wa
mabehewa hayo.
Mabehewa hayo
yaliingizwa nchini kupitia kandarasi ya Kampuni ya M/S Hindustan Engineering
and Industrial Limited ya India ikishirikiana na kampuni moja nchini
inayomilikiwa na mfanyabiashara mmoja ambaye amekuwa akijihusisha na biashara
nyingi za kulaghai mashirika ya umma na kujipatia ukwasi wa kupindukia.
Mabehewa hayo
yaligundulika kuwa mabovu baada ya kufanyiwa majaribio na baadhi kuanguka kwa
kukosa ‘stability’ yakiwa relini na yaliyopokelewa na Dk. Mwakyembe Julai
24, mwaka jana, hayakupitiwa na jopo la mafundi wa TRL ili
kuthibitisha ubora wake.
Jana Chanzo Changu kilimtafuta
Waziri Sitta kuzungumzia taarifa hizo bila mafanikio kutokana na simu
zake za mkononi kushindwa kupatikana.
Hata hivyo mmoja wa
walinzi wake aliliambia Chanzo changu kuwa waziri huyo alikuwa kwenye kikao
ambacho hata hivyo hakueleza kilikuwa kinafanyikia wapi.
CHANZO: NIPASHE
No comments
Post a Comment