WEZI WA ESCROW WAZIDI KUJICHANGANYA MAADILI,BOSI TCAA AJIINGIZA MKENGE,SOMA HAPA KUJUA
MKURUGENZI wa Idara ya
Udhibiti masuala ya Kiuchumi wa Mamlaka ya Usafiri
wa Anga Tanzania(TCAA), Dk. James Diu, amekiri kupokea kiasi cha sh.
milioni 80.8 kutoka kwa James Rugemalira, lakini “akajikoroga” kuhusu matumizi
halisi ya fedha hizo. Anaandika Mwandishi wetu…(endelea).
Hatua hiyo ni baada ya Dk. Diu ambaye pia
aliwahi kuwa Meneja Udhibiti Uchumi katika Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na
Maji (EWURA), kudai kuwa alitumia fedha hizo kwa ajili ya matibabu ya mkewe
aliyefariki dunia Agosti mwaka jana, kwa ugonjwa wa saratani.
Maelezo yake yanatofautiana na yale
aliyoyatoa mbele ya Kamati ya Uchunguzi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi
wa Umma na tamko lake la mali na madeni la Desemba 30, mwaka jana,
linalobainisha kuwa alitumia fedha hizokulipia deni lake la nyumba alilokuwa
akidaiwa.
Kutokana na mkorogano
huo mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, Wakili wa Sekrtarieti hiyo,
Getrude Cyriacus,
akihitimisha hoja hiyo, aliomba Dk. Diu ajibu mashtaka na kutoa maelezo zaidi
kwa kuwa amejichanganya
kuhusu matumizi ya fedha hizo.
Awali, Wakili wa Sekretarieti hiyo,
Wemaeli Mtei, amedai kuwa Dk. Diu aliomba na kupokea sh. milioni 80.8 kutoka
kampuni ya VIP Engeneering and Marketing Limited kinyume cha Sheria ya Maadili
ya Viongozi wa Umma.
Amesema pamoja na fedha hizo, pia
Dk. Diu amejipatia maslahi ya kiuchumi kwa kupokea kiasi cha dola za Marekani
25,000 kutoka kampuni ya Mabibo Beers, Wine and Spirit mali ya Rugemalira,
kinyume cha Sheria hiyo ya maadili.
Katika hati hiyo ya mashtaka,
pia Dk. Diu anadaiwa kupokea dola za Marekani 10,100 kutoka Kampuni ya Prime
Fuel Tanzania limited ambazo zote hakuzitamka kama Sheria hiyo ya maadili
inavyotaka.
Kwamba, mlalamikiwa
ambaye amewahi kufanyakazi EWURA inayoshughulika na masuala ya nishati, alijipatia
kiasi hicho cha fedha kutoka kampuni ya VIP yenye hisa asilimia 30 katika
kampuni ya IPTL yenye mkataba wa umeme na Tanesco, jambo linalosababisha
mgongano wa kimaslahi.
Shahidi wa Sekteratieti hiyo, Zahara Guga,
amesema kitendo cha mlalakiwa kuwa na historia ya kufanya kazi EWURA na kupokea
fedha kutoka kampuni ya VIP ambayo inasimamiwa na mamlaka hiyo ni kinyume na
Sheria ya maadili na pia ni mgongano wa kimaslahi.
Ameongeza kuwa katika
uchunguzi walibaini kuwa Dk. Diu alifungua akaunti Februari 4, mwaka jana
katika Benki ya Mkombozi tawi la Kariakoo na kuingiziwa sh. milioni 80.8
Februari 5, mwaka huo na kampuni ya VIP.
Katika utetezi wake, Dk Diu,
alikanusha kuomba fedha hizo kwa Rugemalira na kukiri kuwa alipokea kiasi hicho
ambacho alipatiwa kama ahadi ya kumsaidia katika matibabu ya mkewe ikiwa ni
pamoja na kumsafirisha kwenda India kwa matibabu zaidi.
“Rugemalira ni
rafiki yangu wa karibu pamoja na familia yangu, lakini pia nimesoma naye
shahada yangu ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1982 hadi 1985,
alinipatia fedha hizo kama ahadi sijamuomba, kudai wala kupokea maslahi ya
kiuchumi kutoka kwake,” alijitetea.
Alisema kutokana na hali mbaya
aliyokuwa nayo mkewe, Rugemalira alikwenda kumjulia hali alipolazwa hospitali
ya TMJ na baadaye Sanitarius iliyopo Mikocheni, ndipo aliahidi kutoa fedha hiyo
kama mchango na msaada wa matibabu na baadaye mazishi baada ya mkewe kufariki.
Ameendelea kujitetea kuwa hata katika
fomu yake ya tamko la mali na madeni kwa sekretarieti hiyo, aliyoiwasilisha
Februari 30, mwaka jana, alizitamka fedha hizo kuwa amezipokea kutoka kwa
Rugemalira. “Awali sikuona umuhimu wa kuiwasilisha kwa ofisa masuhuli wangu kwa
sababu haikuwa zawadi na sikuona umuhimu wa kufanya hivyo,”alidai.
Aidha alisisitiza kuwa
kupokea kwake fedha hizo hakuna mgongano wowote wa kimaslahi kwa kuwa hana
uhusiano wowote wa kibiashara na Rugmalira na hata kazi yake katika mamlaka ya
TCAA haina uhusiano na kampuni za Rugemalira kibishara.
Utetezi wake, ulionekana
kulikanganya baraza hilo, ambapo wakili wa Sekrtarieti hiyo, Getrude Cyriacus,
alibainisha kuwa Dk. Diu alijitetea kuwa fedha hizo alizitumia kulipia deni la
nyumba alilokuwa akidaiwa.
“Hata katika tamko la
mali na madeni aliloliwasilisha mwaka 2012, aliandika maelezo kuwa anadaiwa sh.
milioni 80 za nyumba ambayo haijakamilika aliyonunua huko Mbezi kwa Godson
Shangwe, na tamko lake la mwaka jana alibainiha kuwa ametumia fedha hizo
alizopewa na Rugemalira kumalizia deni hilo,” alisema Cyriacus.
Dk. Diu alipobanwa,
alijitetea kuwa ni kweli alitumia sh. milioni 80.8 kulipia deni hilo la nyumba
kutoka kwa Rugemalira
lakini fedha hizo si hizo zinazodaiwa na Sekretarieti bali ni nyingine.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji Hamis
Msumi, amesema kuwa wamesikiliza shauri hilo na litatoa uamuzi wake na
mapendekezo kwa mamlaka husika.
Chanzo ni mwanahalisi.online
Hakuna maoni
Chapisha Maoni