MBUNGE MNYIKA ALIA NA KIKWETE,SOMA HAPA KUJUA
MBUNGE wa Ubongo, John Mnyika, amemtaka Rais Jakaya Kikwete,
kulieleza taifa kwa nini ameshidwa kutekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati
akizundua Bunge la Jamhuri, Novemba 2005.Anaandika Pendo Omary ….
(endelea).
Kile ambacho Mnyika amekiita
kimeshindwa kutekelezwa na Rais Kikwete, ni ahadi kuwa anatambua “maji ni kero
nambari wani” na kwamba serikali yake itaandaa mpango kabambe wa kuhakikisha
“tatizo la maji linakuwa historia nchini.”
Mnyika alitoa kauli hiyo jijini
jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
“Rais
Kikwete ameonesha udhaifu mkubwa wa kutekeleza ahadi zake alizozitoa kwa
wananchi. Mwaka 2010 alilieleza Bunge kuwa serikali yake itamaliza matatizo ya
maji nchini, lakini mpaka sasa imeshindwa kutekeleza ahadi hiyo.”
Mnyika anatoa kauli hiyo, ikiwa ni
kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji kitaifa; huku ujumbe wa mwaka huu, ukiwa
“Maji kwa maendeleo endelevu.”
Maadhimisho ya mwaka huu
yanafanyika mjini Musoma, mkoani Mara ambapo Rais Kikwete amepangwa kuhutubia
taifa. Maadhimisho hayo ni ya mwisho kuhudhuriwa na Kikwete kama mkuu wa nchi.
Akiongea kwa uchungu, Mnyika amemtaka
Waziri Mkuu wa Jamhuri, Mizengo Pinda, kutekeleze ahadi iliyotolewa na
aliyekuwa waziri wa maji, Prof. Mark Mwandosya kwa niaba ya serikali kuwa
katika kila mkutano wa Bunge kutawasilishwa taarifa ya mpango wa dharura kuhusu
upatikanaji wa maji.
Mbali na ahadi ya rais, ilani
ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005, iliahidi ifikapo mwaka 2010 maji
yangepatikana mijini ikiwemo jiji la Dar es Salaam kwa asilimia 90 na vijijini
kwa asilimia 75. Amesema yote hayo yameshindwa kutekelezwa.
Wakati Rais Kikwete anaingia
madarakani, Desemba mwaka 2005, upatikanaji wa maji ulikuwa ni asilimia 65.
Lakini mwaka 2010 upatikanaji wa maji ulishuka hadi kufikia asilimia 55.
“Ili Rais asiendelee kuonekana
dhaifu zaidi, walau kupitia siku hii ya maji awaagize watendaji katika ofsi
yake watekeleze agizo alilowapa la kuitisha kikao cha kazi Ikulu kuhusu
matatizo ya maji katika jiji la Dar es Salaam kama alivyoahidi,” amesema
Mnyika.
Amesema zipo hatua zinazoweza
kuchukuliwa katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa iwapo watakutana na
kujadili udhaifu uliopo katika utekelezaji wa mpango maalum wa maji jijini Dar
es Saam.
“Kwa kuwa nimeshamkumbusha yeye
mwenyewe na wasaidizi wake mara kadhaa bila kikao hicho kuitishwa, ni wakati
sasa wa wananchi wa Dar es Salaam kushiriki kumkumbusha kwa njia mtakazoona
zinafaa,” ameeleza.
Chanzo ni
mwanahalisi.online
No comments
Post a Comment