LOWASSA ALETA KILIO 'UDOM' BAADA YA WANAFUNZI WAKE 'FEKI' SASA AGEUKIWA PROFESA SOMA HAPA KUJUA
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Peter Kopoka amebanwa
na uongozi wa chuo hicho kutokana na kushiriki maandamano ya kwenda nyumbani
kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kumshawishi achukue fomu ya kugombea
urais.
Profesa huyo akiwa
na wahadhiri pamoja na watu wengine walioelezwa kuwa ni wanafunzi wa vyuo vikuu
mkoani Dodoma walifanya maandamano hayo Machi 22, mwaka huu.
Kutokana na
tukio hilo, uongozi wa Udom umemtaka ajieleze kwa nini ameshiriki harakati hizo
za kisiasa huku akijua kuwa ni mtumishi wa umma anayepaswa kuwahudumia watu
wenye itikadi tofauti.
Makamu Mkuu wa
Chuo hicho, Profesa Idris Kikula alisema kwa kuwa jambo hilo lilionekana
kukiwakilisha chuo katika masuala ya siasa, uongozi ulilazimika kumhoji mhadhiri
huyo.
“Ametuandikia
barua ya kujieleza na kubainisha kuwa alikwenda yeye binafsi na siyo kama
mwakilishi wa chuo. Lakini mambo haya ni magumu sana kutofautisha. Mimi kwa
mfano, siwezi kwenda sehemu halafu nikasema sikwenda kama mkuu wa chuo kwa sababu
siwezi kutofautisha hilo. Lakini tumechukua maelezo yake na tumeyahifadhi,”
alisema Profesa Kikula.
Kuhusu wanafunzi
wanaodaiwa kushiriki harakati hizo kutoka chuoni hapo, alisema hakuna
wanachoweza kufanya kwa sababu mbili kubwa. Kwanza, ni vigumu kuwatambua
waliofanya hivyo na pili walifanya hivyo nje ya chuo, jambo linalowezekana.
“Maandamano hayo
yalifanyika mtaani. Huko walikuwa wanavunja sheria za nchi, kama hayakufuata
sheria, Jeshi la Polisi ndilo lenye mamlaka ya kudhibiti au kuruhusu jambo kama
hilo kufanyika,” alisema. Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Profesa Kopoka alikiri kuandika barua
hiyo na kueleza kuwa alichokifanya ni kutekeleza haki yake ya uraia ya ushiriki
katika utawala wa haki na demokrasia nchini.
“Nimefanya hivyo.
Nilikwenda kutokana na imani yangu kutokana na vile ninavyomfahamu Lowassa.
Sikuwa peke yangu. Ni kama ilivyoripotiwa, walikuwapo pia wahadhiri kutoka vyuo
vikuu vya Mtakatifu Yohana (St. John) na Mipango,” alisema Profesa Kopoka.
Alisema pamoja
na kufanya hivyo, suala hilo halijaathiri utendaji wake wala mkataba wake wa
ajira.
Mfululizo
wa kukanusha
Siku nne baada ya
maandamano hayo, viongozi wa Serikali za wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali
walijitokeza na kukanusha habari hiyo kwa maelezo kuwa waliofanya hivyo hawakuwa
wanafunzi na wala suala hilo halikupata baraka kutoka vyuoni.
Katika taarifa ya
pamoja ya marais wa serikali za vyuo vikuu hivyo vilivyomo mkoani humo
iliyosomwa na Rais wa St. John, Daniel Daniel imepinga kushiriki kwao na
kubainisha kuwa waliofanya hivyo ni watu wa mtaani.
“Tunapenda
kukanusha kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma kwa ujumla wetu hatukuhusika
na jambo lile na kama viongozi wa serikali za wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya
mkoa huu wa Dodoma, tunapinga na kulaani kitendo cha watu wachache kwenda
kutuingiza sisi wanafunzi wa vyuo vikuu katika jambo ambalo halituhusu na wala
siyo lililotuleta hapa Dodoma,” alisema Daniel.
Walisema watu
waliokusanyika nyumbani kwa Lowassa walijumuisha wamachinga, wenyeviti wa
jumuiya za wazazi pamoja na wanafunzi wachache kutoka vyuoni ambao walifanya
hivyo kutoka mtaani yalikoanzia maandamano hayo.
Walieleza kuwa:
“Idadi ya watu waliojikusanya nyumbani kwa Lowassa haizidi 230. Idadi ya
wanafunzi waliokuwapo kwenye tukio lile hawazidi 150. Idadi hii ni sawa na
asilimia 0.4 ya wanafunzi wote wanaosoma vyuo vikuu vya Dodoma.”
Wanafunzi hao ni
kundi la pili kupinga ushiriki wake katika maandamano yaliyoripotiwa kufanya
hivyo baada ya Sheikh wa Wilaya ya Bagamoyo, Abdulkadir Mohammed Ramiya
kukanusha taarifa ya masheikh 50 kutoka wilayani mwake kwenda kwa Lowassa
kumuomba kuchukua fomu ya urais pia. Mapema wiki hii, iliripotiwa kuwa
masheikh 50 kutoka Bagamoyo walifunga safari mpaka Area D, Dodoma yalipo makazi
ya Lowassa na kumtaka agombee urais na kisha kumkabidhi kiasi cha Sh700,000 za
kuchukulia fomu husika.
Siku chache
baadaye, Sheikh Ramiya alikanusha taarifa hizo na kueleza kuwa kati ya masheikh
50 waliokwenda huko hapakuwa na hata mmoja kutoka wilayani mwake.
Makundi
ya kushawishi
Katika siku za hivi
karibuni kumekuwa na makundi mbalimbali yanayoripotiwa kwenda Dodoma na
kumshawishi Lowassa kugombea nafasi hiyo ikiwa ni kutekeleza kauli aliyowahi
kuitoa Rais Jakaya Kikwete katika kilele cha sherehe za kuanzishwa kwa CCM
mwaka huu kuwa wanaostahili kugombea wapo kimya na wanahitaji kuambiwa wafanye
hivyo.
Baadhi ya makundi
yaliyofanya ushawishi huo mpaka sasa, ukiacha jumuiya ya masheikh kutoka
Bagamoyo na wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Dodoma, ni pamoja na Jumuiya ya
Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste na umoja wa madereva bodaboda kutoka
Mbarali mkoani Mbeya.
Alipoulizwa kuhusu
suala hilo, Kamanda wa Polisi Dodoma, David Misime alisema “Sijaelewa unauliza
nini,” kisha kutaka simu.
Chanzo ni
gazeti la mwananchi
No comments
Post a Comment