ZITTO KABWE AJIFALIJI NA ACT YAKE,ASEMA MANENO HAYA,MSANII AFANDE SELE AMUFUATA SOMA HAPA KUJUA
Sasa ninapenda kuwataarifu, kama
ambavyo baadhi yenu tayari mnajua, kwamba jana siku ya Jumamosi tarehe 20 Machi
2015 nilijiunga rasmi na Chama cha ACT - Wazalendo na kukabidhiwa kadi na
Mwenyekti wa Tawi la Tegeta. Hii ilikuwa ni moja kati ya siku muhimu kabisa
katika maisha yangu ya kisiasa. Na kwa leo kwa kweli nisingependa nizungumzie
mgogoro uliokuwepo kati yangu na viongozi wangu wa chama cha zamani wala kile
kilichotokea Bungeni. Hayo yote mnayajua, yameandikwa sana na yameshapita. Sasa
ni wakati wa kusonga mbele. Rais Kwame Nkrumah alipata kusema "forward
ever, backward never". Na kama nilivyosema Bungeni, yaliyopita si ndwele,
tugange yajayo. Kwa hiyo leo nitazungumzia uanachama wangu katika chama changu
kipya cha ACT - Wazalendo.
Tuna vyama 22 kwa sasa. Na kwa kweli
wengi watakuwa wanajiuliza kwa nini nijiunge na chama kipya ambacho
kimeanzishwa juzi tu na ambacho pengine wanachama wake bado wanajaa katika
kiganja cha mkono?
Nimejiunga na ACT kwa sababu ninaona
kwamba huku ndiko kunakoendana na kile ambacho mimi nimekipigania kwa miaka
yote tangu nianze siasa, ambacho ni kuweka mbele maslahi ya Taifa dhidi ya kitu
kingine chochote. Kwa kifupi nimepigania uzalendo kwa nchi yangu na huu ndiyo
msingi mama wa Chama cha ACT - Wazalendo.
Kama mnavyojua mimi ni mjamaa na
ninaamini katika misingi ambayo Mwalimu Nyerere aliisimamia. ACT-Wazalendo ni
chama pekee nchini kinachokubaliana na Itikadi ya ujamaa na kinaamini katika
Falsafa ya Unyerere ikiwa na lengo la kuirudisha nchi katika misingi iliyoasisi
taifa. Ninajiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ni chama kinachoamini katika
msingi wa uadilifu na kimeweka miiko na maadili ya viongozi katika kuhakikisha
kwamba viongozi wote wa ACT-Wazalendo wanakubaliana nayo kwa kusaini. Naamini
kuwa na miiko na maadili kwa viongozi ni mwanzo wa kuhakikisha kwamba jamii
yetu inaishi katika uadilifu na kwamba viongozi wanakuwa mfano wa uadilifu
katika jamii. Uadilifu ni nguzo muhimu katika kujenga mfumo madhubuti wa
uwajibikaji nchini kwetu.
Mtakumbuka kwamba katika miaka yangu
yote ya ubunge nimepigania uwajibikaji na uwazi. Hii ni misingi ambayo ninaamini
kwamba ni moyo wa utumishi wa umma. Nimefurahi kwamba kati ya misingi kumi ya
ACT-Wazalendo, uwajibikaji na uwazi ni sehemu muhimu kabisa ya misingi hiyo.
Uwazi ni sehemu ya jina la chama hiki. Yote haya yamenifanya nione kwamba
sitojiona mgeni katika chama hiki. Huku ndiko nyumbani kwangu kisiasa na katika
utumishi wa umma.
Nimejiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu
ninakubaliana na imani yao kwamba Kujitegemea, bidii, umakini na weledi katika
kazi ndiyo msingi wa maendeleo. Hakuna namna nchi yetu na wananchi watapiga
hatua ya kimaendeleo bila sisi sote kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia
umakini na weledi. Ninakubaliana na ACT-Wazalendo kwamba raslimali za Taifa
lazima zitumike kuondosha umaskini wa watu wetu. Ninajiunga na ACT-Wazalendo
kwa sababu ninakubaliana na imani yao kwamba Umoja ni ngao muhimu katika ujenzi
wa taifa letu na Afrika kwa ujumla. Lazima tuirudishe nchi yetu katika misingi
iliyoasisi taifa hili. Lazima tuirudishe nchi yetu katika heshima na uongozi wa
bara hili la Afrika.
Ninaahidi kufanya kazi na vijana,
wanawake, wanaume na watu wote wanaoamini katika siasa safi na siasa za hoja.
Tunataka tufungue ukurasa mpya wa siasa hapa nchini. Siasa za masuala ya nchi
yetu. Siasa za masuala ya vijana, wanawake, wazee, wakulima, wafanyakazi,
wajasirialimali, wafanyabiashara na wote wanahangaika kuijenga nchi yetu na
katika kuondoa umaskini. Tunataka tuzungumze namna bora ya kuendesha elimu,
afya, hifadhi ya jamii, na ajira. Tunataka tujenga hoja mbadala kuhusu namna
endelevu ya kujenga uchumi shirikishi ambapo kila mwananchi anajisikia sehemu
yake.
Mwezi Oktoba mwaka 1966 Mwalimu Nyerere
alipokea maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Ikulu.
Maandamano yale yalichochewa na kasi kubwa ya rushwa na maisha ya kifahari ya
viongozi (wabenzi). Mwalimu alifoka kwa kuuliza “ Tunajenga nchi ya namna
gani”? Hatimaye Azimio la Arusha likatangazwa.
Chama hiki kipya kimeanzishwa katika
mazingira yale yale ya mwaka 1966. Ni wakati wa kujiuliza na kupata majawabu ya
aina ya nchi tunayojenga. Sisi ACT – Wazalendo tumeona jawabu ni kurudi kwenye
misingi. Waingereza wanasema ‘back to the future’ Let the new beginning begin.
Chama cha ACT-Tanzania leo kimemtangaza aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Zitto Kabwe kuwa mwanachama mpya wa chama hicho kuanzia.
Zitto amesema ameamua kujiunga na chama hicho kwa kuwa ni chama chenye misingi bora ya uongozi na hivyo yeye kama kiongozi ameamua kwenda huko kwani anaamini kuwa Chama hicho ndicho kitakacholeta mapinduzi ya kweli kwenye siasa.
Mbali na Mh. Zitto Kabwe,wengine waliojiunga na chama hivyo ni pamoja na hao waliopo kwenye orodha hiyo hapo chini.
Orodha ya waliojiunga na Chama cha ACT-Tanzania leo.
Aliekuwa Mbunge wa Jimbo Khamisma Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Zitto Kabwe akinzungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kutambulishwa kwake kujiunga na Chama cha ACT-Tanzania,katika mkutano uliofanyika mapema leo kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Serena,Jijini Dar es salaam.kushoto ni Mwenyekiti wa Tawi la Tegeta wa Chama cha ACT-Tanzania,Lugano Mwaikenda.Picha zote na Othman Michuzi.
Aliekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Zitto Kabwe akionyesha kadi ya Chama chake kipya yenye namba 007184 mbele ya waandishi wa habari waliofika kwenye mkutano wa Chama cha ACT-Tanzania,uliofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Serena,jijini Dar es salaam leo.kushoto ni Mwenyekiti wa Tawi la Tegeta wa Chama cha ACT-Tanzania,Lugano Mwaikenda.
Mwenyekiti wa Tawi la Tegeta wa Chama cha ACT-Tanzania,Lugano Mwaikenda akionyesha kipeperushi cha Chama chao mbele ya waandishi wa habari wakati wa kumtangaza mwanachama wao mpya ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Zitto Kabwe.
Msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya,Selemani Msindi "Afande Selle" akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza kuungana na Mh. Zitto Kabwe kujiunga na chama ACT-Tanzania kutokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).Kulia ni Katibu Mkuu wa Chama ACT-Tanzania,Samson Mwigamba na kushoto ni rafiki wa Afande Selle ambaye nae amejiunga na Chama hicho,Adam Shanzy.
Katibu Mkuu wa Chama ACT-Tanzania,Samson Mwigamba akimkabishi kadi ya uwanachama,Msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya,Selemani Msindi "Afande Selle" ambaye amejiunga na chama hicho akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Sehemu ya Wanachama wa Chama ACT-Tanzania wakionyesha mabango ya kumkaribisha Mwanachama mwenzao ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Zitto Kabwe.
Katibu Mkuu wa Chama ACT-Tanzania,Samson Mwigamba pamoja na Zitto Kabwe wakinukuu kwenye makaratasi maswali mbali mbali yaliyokuwa yakiulizwa na waandishi wa habari katika mkutano wao uliofanyika leo kwenye hoteli ya Serena,Jijini Dar es salaam.
Sehemu ya Wanahabari wakifatilia kwa makini hotuba ya Aliekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Zitto Kabwe,wakati akitangaza kujiunga na Chama cha ACT-Tanzania.
Katibu Mkuu wa Chama ACT-Tanzania,Samson Mwigamba akiteta jambo na Aliekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Zitto Kabwe,Zitto Kabwe
Sehemu ya Wanachama wa ACT-Tanzania pamoja na Waandishi wa habari wakiwa kwenye Mkutano huo leo.













1 comment
Duuh mungu yupo pamoja nawe, jitahidi kuchanga karata rafiki yangu nimezibitisha matamshi ya waziri mkuu mizengo pinda aliyesema kijana Zitto Kabwe uchaguzi ujao jifunge mkanda vizuri, kana kwamba alijua kinachoendela ndani ya chadema, hatujafuarahishwa na hiyo hali lakini hakuna namna kadhaa buti
Post a Comment