HABARI KUBWA- NIMROD MKONO ALIUA TAIFA,ALIMALIZA SHIRIKA LA TANESCO KAMA LA KWAKE,SOMA HAPA KUJUA
KAMPUNI ya mbunge wa Musoma Vijijini
(CCM), Nimrod Mkono (Pichani) inadaiwa kulipwa na TANESCO, takriban shilingi 18 bilioni
kwa huduma ya ushauri, chanzo Changu kimegundua.
Nyaraka ambazo Chanzo hicho kimeona
zinaonyesha kuwa tayari kampuni ya Mkono imetumia kiasi hicho kutoka shirika la
umeme linalolegalega kifedha.
Mkono na kampuni yake ya Mkono &
Co. Advocates ya jijini Dar es Salaam, amekuwa mshauri wa kisheria na wakili wa
TANESCO tangu Mei 1995.
Nyaraka zinaonyesha kuwa shilingi 18
bilioni zimelipwa kwa ushauri na utetezi ambao kampuni ya Mkono imefanya katika
minyukano ya kudaiana kati ya TANESCO na kampuni nyingine ya umeme, Independent
Power Tanzania Limited (IPTL).
Hivi sasa uhusiano wa TANESCO, kampuni
ya umeme ya serikali na kampuni ya Mkono, umekuwa wa kilio kama mawasiliano ya
ndani yanavyoonyesha.
Moja ya mawasiliano hayo ni barura ya Jenerali Robert Mboma,Aliyekuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi TANESCO,
ambayo inalalamikia matumizi ya mabilioni ya shilingi ya kampuni ya Mkono, tena
bila mafanikio.
Barua ya Mboma ya 10 Septemba 2013;
kwenda kwa Mkono, inalalamikia matumizi ya kiasi hicho cha fedha katika
mashauri ambayo yamechukua muda mrefu na bila kuleta tija.
Barua yenye Kumb. Na.
SEC.427/IPTL/9/2013; ambayo imebeba kichwa cha maneno kisemacho, “Ushauri ambao
kampuni yako imetoa kwa Tanzania Electric Supply Company Limited,” imenukuliwa
kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
“Kwa sasa, kulingana na kumbukumbu
tulizonazo, kampuni yako imekwishatumia takribani Sh. 18 bilioni kama gharama
za ushauri katika kusimamia suala hili kufikia Aprili 2013,” anaeleza Jenerali
Mboma.
Anasema, “Hiki ni kiasi kikubwa mno
cha fedha za walipa kodi ambazo zingeweza kuwekezwa kwenye miradi mingine ya
uzalishaji kwa manufaa ya Watanzania wote.”
Kana kwamba hiyo haitoshi, Mboma
anasema, “TANESCO inataka ieleweke kuwa inasikitishwa na namna kampuni yako
ilivyotoa ushauri wa kisheria kuhusiana na mivutano iliyohusu Mkataba wa mauziano (PPA) wa
tarehe 26 Mei 1995 kati yetu na IPTL, kwa vile ulivyotushauri na katika
kuisimamia kesi tangu ilipofunguliwa mwaka 1998.”
TANESCO sasa inatuhumu kampuni ya
mkono kutoishauri vizuri hadi kupoteza kesi yake dhidi ya IPTL. Kesi
ambayo TANESCO inasema imeipoteza kwa kutoshauriwa vizuri inahusu mkataba wa
kununua umeme – Power Purchase Agreement (PPA) wa 26 Mei 1995.
Kampuni ya IPTL ndiyo kampuni ya
kwanza ya nje kuingiza mitambo ya kuzalisha umeme wa dharula nchini. Mitambo
yake inatumia mafuta mazito (Industrial Diezel Oil – IDO); jambo ambalo
linasababisha umeme inaozalisha kuwa ghali kuliko ule wa kuzalisha kwa kutumia
gesi na, au maji.
Taarifa kutoka ndani ya TANESCO
zinasema, mbali na malipo kwa Mkono, kampuni ya IPTL hukomba kiasi cha Sh. 1.8
bilioni kila mwezi zikiwa malipo kwa gharama za kuweka mitambo yake nchini –Capacity
Charge.
Mtoa taarifa kutoka ndani ya serikali
anasema, kwa kuwa TANESCO inakabiliwa na ukata mkubwa wa fedha kutokana na
mikataba ya kinyonyaji ya umeme, serikali hutoa kila mwezi, kiasi cha Sh. 3.8
bilioni kuwezesha shirika hilo kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya dharula.
(Waziri, Katibu mkuu, Mboma, Mkono,
TANESCO na CEO wanasemaje?)
Kampuni ya Mkono imo katika umoja na
kampuni ya SNR Denton. Imeelezwa kuwa umoja huo wa kampuni unaundwa na zaidi ya
wanasheria 1,100 wa Uingereza, Marekani, Canada na Tanzania; na una makao makuu
jijini London, Uingereza.
TANESCO limeeleza kwamba
lilishauriwa na wanasheria wa Mkono & Co. Advocates kuwa lina hoja za
msingi kudai urekebishaji wa kiwango cha bei na kwamba “TANESCO watapaswa kudai
kiasi kitakachokuwa kimezidi kutokana na ankara za IPTL zilizotozwa baada ya
maamuzi.”
“…ulitushauri tutoe indhari ya
madai ya ankara za ziada kwa IPTL. Tukapinga ankara za malipo zilizohusu
gharama za kuweka mitambo – Capacity Charge. Yote haya yalifanywa kwa
kuzingatia ushauri wako,” imeeleza barua ya Mboma kwa Mkono na kwamba hatua hiyo
haikufanikiwa.
Katika barua , TANESCO inalalamikia
kampuni ya Mkono kwamba pamoja na kutoa ushauri 30 Juni 2004 kuwa shirika hilo
lina hoja za msingi na halali kuomba urekebishaji wa bei ya umeme na
kurudishiwa malipo ya ziada, lakini 4 Oktoba 2012, Mkono alikwenda na mtizamo
tofauti.
“Katika barua yako ya 4 Oktoba 2012,
umesema kuna uwezekano mdogo sana wa kushinda kesi hiyo kutokana na kugundulika
kwa baadhi ya nyaraka zilizodhoofisha utetezi uliotolewa mapema na shirika,”
barua ya Mboma inaeleza.
Inaongeza, “Ulitushauri kwa hoja
nzito kuwa tupiganie usuluhishi na Benki ya Hong Kong – SCB HK au kampuni
yako ielekezwe zaidi kuwasilisha ombi la kukataliwa kwa uamuzi unaoinufaisha
benki hiyo,” Mboma anaeleza Mkono kwa njia ya malalamiko.
Barua ya shirika hilo inajibu
maelezo ya Mkono ya kutaka malipo ya ziada ya fedha kwenye kesi hiyo wakati
TANESCO haioni manufaa ya malipo hayo.
Wakati wote wa mgogoro, fedha
zilizokuwa zinabishaniwa mahakamani, ziliingizwa kwenye akaunti maalum
iliyofunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kutokana na mfumo huo wa kubishania
ankara, IPTL ilifungua malalamiko mbele ya Taasisi ya Usuluhishi wa Migogoro ya
Uwekezaji (ICSID)
wakitaka kupatikana tafsiri halisi ya eneo hilo kulingana na mkataba wa
mauziano ya umeme.
Katika hatua hiyo, TANESCO
inalalamikia kampuni ya Mkono ambayo iliiwakilisha mpaka pale shauri hilo
lilipofutwa kwa manufaa ya IPTL kutokana na amri iliyotolewa 19 Agosti
2010.
Kwa barua ya kampuni ya Mkono ya
4 Oktoba 2010, TANESCO inajulishwa kuhusu nia ya benki ya Standard Chartered
Hong Kong (SCB HK) kufungua ombi la usuluhishi baada ya IPTL kuacha kuendelea
kwa shauri.
Matokeo yake, mbali ya kuihakikishia TANESCO
kuwa itashinda, ikashauri pia shirika lielekeze kampuni hiyo ya uwakili
kuendelea kutaka kusimamishwa kwa usajili wa malalamiko ya SCB HK mbele ya
ICSID kwa hoja kwamba SCB HK haina uhalali katika suala hilo. TANESCO walitoa
maelekezo hayo kwa mawakili wa Mkono.
Hata hivyo, TANESCO inalalamika kuwa
mawakili hao walishindwa kuzuia SCB HK kusajili malalamiko yake na hatimaye,
“Ombi (letu) kuhusu suala hilo lilitupwa.”
“Usajili wa SCB HK ulikubaliwa na
ICSID, na ukasikilizwa kama ulivyopangwa,” imesema TANESCO katika barua yake
kwa kampuni ya Mkono.
Mara tu usikilizaji wa usuluhishi
ulipofungwa Aprili 2013, TANESCO inasema kampuni ya uwakili ya Mkono ilishauri
shirika kufungua ombi la kucheleweshwa tamko la ICSID la kuipa SCB HK ushindi
mpaka kwanza kusubiri uamuzi wa ombi la SCB HK lililokuwa likiendelea
kusikilizwa kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania.
“TANESCO ilizuia, lakini pia
ilishindwa. ICSID ilisema kuwa itatoa tamko lake ndani ya miezi mitatu,” barua
ya Mbona inaeleza.
TANESCO, mbali na kulipa mabilioni
hayo ya shilingi kwa ushauri, imekuwa ikilipa fedha nyingi kwa makampuni
yanayodai kutoa huduma za kisheria, ikiwamo kesi kati ya shirika hilo na
makampuni ya Richmond Development Company (DRC), Dowans Holding na Dowans
Tanzania Limited.
Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja miaka
saba baada ya Mkono kutajwa na kiongozi mkuu wa upinzani nchini, Dk. Willibrod
Slaa kuwa ni miongoni mwa watuhumiwa 11 wa ufisadi nchini.
Mbele ya umati mkubwa, kwenye
mkutano wa hadhara katika viwanja vya Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam, Dk.
Slaa alisema Mkono, kupitia kampuni yake ya Mkono & Co. Advocates amekuwa
akilipwa malipo makubwa, hasa yale yanayohusu kesi ya Valambhia, ambamo BoT
inadaiwa jumla ya Sh. 60 bilioni.
Dk. Slaa alisema, kwa mujibu wa
Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), kampuni ya Mkono tayari
imelipwa zaidi ya Sh. 8.1 bilioni, fedha taslimu kwa kesi hiyo ambayo bado iko
mahakamani. Malipo hayo, wakati huo, yalikuwa sawa na asilimia 13.5 ya deni
lote inalodaiwa BoT.
Chini ya Kanuni za Malipo ya
Mawakili na Uamuzi wa Gharama za Kesi za mwaka 1991 (Tangazo la Serikali Na.
515 la 1995), kiwango cha malipo ya mawakili katika kesi ambazo fedha
inayodaiwa ni zaidi ya Sh. 10 milioni, kitakuwa asilimia tatu.
Kwa kufuata masharti ya sheria
hii, kampuni ya Mkono ilipaswa kulipwa Sh. 1.8 bilioni.
Aidha, kampuni ya Mkono inatajwa
katika taarifa ya uchunguzi kuhusu tuhuma dhidi ya makampuni ya Tanfarms Ltd.,
Makinyumbi Estates Ltd., Centrepoint Investments Ltd., na Arusha Farms Ltd.,
yanayomilikiwa na V. G. Chavda kuhusiana na matumizi mabaya ya fedha za Debt
Conversion Programme
Chanzo ni Gazeti la Mawio pamoja na Gazeti la Mtandaoni la Mwanahalisi.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni