UFISADI WA ESROW WAIANGAMIZA CCM,WAZEE WAIBUKA WAMLALUA KIKWETE SOMA HAPA KUJUA
SAKATA la ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi ndani ya Benki Kuu
(BoT), limeanza kukipasua Chama Cha Mapinduzi (CCM). Tayari wazee na viongozi
wa chama hicho kutoka mkoani Kagera, wametishia kuondoka chama hicho kwa madai
ya unyanyasaji dhidi ya wananchi wa mkoa wa Kagera.” Anaandika Saed
Kubenea…(endelea)
Hatua ya viongozi hao, inafuatia
kuwapo taarifa kuwa chama hicho, kimepanga kumfukuza katika Kamati Kuu (CC),
Prof. Anna Tibaijuka.
Tayari wazee na viongozi hao, wako
jijini Dar es Salaam kuonana na rais kupinga Prof. Tibaijuka “kufanywa mbuzi wa
kafara.”
Prof. Tibaijuka alifukuzwa kazi na
Rais Kikwete mwishoni mwa mwaka jana. Ametajwa kuwa miongoni mwa walionufaika
na mgawo wa Sh. 1.6 bilioni kutoka kwa James Rugemalira, mmoja wa waliokuwa
wamiliki wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited
(IPTL).
Rugemalira alikuwa akilimiki
asilimia 30 ya hisa katika IPTL, kupitia kampuni yake ya VIP Engineering and
Marketing Limited.
Mmoja wa viongozi katika ujumbe huo
amekiambia Chanzo changu kuwa kumfukuza Prof. Tibaijuka ni mkakati wa kuengua
viongozi kutoka mkoa wa Kagera; na kuonya kuwa Tibaijuka akifukuzwa CC, basi
chama hicho kisitegemee kupata “hata kiti kimoja cha ubunge” mkoani Kagera.
Prof. Tibaijuka ni mbunge wa
Muleba Kusini (CCM). Alikuwa waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Ni
mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa mkoani humo.
Taarifa zinasema, mkakati wa kumfukuza
kazi Prof. Tibaijuka, kuondolewa kwenye kamati kuu na baadaye kufikishwa
mahakamani, unasukwa kwa ustadi mkubwa na waziri mmoja mwandamizi katika
serikali ya Rais Kikwete.
Katika jitihada za kutaka kujiondoa
katika dimbwi la lawama, mtoa taarifa anasema, baadhi ya maafisa waandamizi wa
ikulu wamemshauri Rais Kikwete kumtosa Prof. Tibaijuka, ili kulainisha nchi
wahisani.
Mtoa taarifa anasema, mmoja wa
mawaziri katika serikali ya Rais Kikwete, aliwasilisha pendekezo kwa rais kuwa
Tibaijuka ana sifa kubwa ndani na nje ya nchi, hivyo akifukuzwa kazi dunia
nzima itaona kuwa “serikali iko makini.”
Amesema washauri walidai kuwa
kufukuzwa kazi kwa Prof. Tibaijuka kutazima sakata zima la Escrow; kwani
kusingekuwa tena na kelele za wahisani; na misaada yote ingerejea na hali kuwa
kama awali.
Viongozi wanaotajwa kutinga jijini,
wanaongozwa na Pius Ngeze, mwenyekiti mstaafu wa chama hicho mkoani Kagera;
Costancia Buhiye, ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho mkoani Kagera na Ally
Ameiry, katibu wa CCM mkoani.
Wengine walioko jijini kukabiliana
na wanaotaka kumuondoa Prof. Tibaijuka katika kamati kuu, ni Faustine Kamaleki,
Sebastian Rwitelana, ambaye ni diwani wa kata ya Nshamba na Zaidia Juma, katibu
wa tawi la Bujumbi.
Taarifa za awali zilisema
ujumbe huo umeshikilia kwamba, kwa kuwa rais alisema fedha za Escrow ni mali ya
mtu binafsi, hakukuwa na sababu ya kumgeuza Prof. Tibajuka kuwa “mbuzi wa
kafara.”
Wachambuzi wa mambo ya kisiasa
wanasema, hatua ya viongozi hao kujitosa kumtetea Prof. Tibaijuka, imekupasua
chama hicho. Hii inatokana na udhaifu wa Rais Kikwete katika kushughulikia
suala hilo.
“Wako wapi wezi wa Escrow katika
akaunti ya Stanbic? Hakuna anayejadili hilo. Badala yake, viongozi wa CCM
wanahaha kuhangaika na Tibaijuka, aliyepewa fedha na ndugu yake,” ameeleza
mmoja wa viongozi serikalini.
Chanzo ni Gazeti la mwanahalisi.online
Hakuna maoni
Chapisha Maoni