UFAFANUZI WA POLISI, KUTEKWA KWA MJESHI WA JKT,SOMA HAPA KUJUA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANI
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA
PRESS RELEASE
23/02/2015
MWENYEKITI WA UMOJA WA WAHITIMU WA JKT NA KATIBU
WAKE WASHIKILIWA NA POLISI KWA MAKOSA YA UCHOCHEZI NA MIKUSANYIKO ISIYO HALALI
JIJINI DAR ES SALAAM.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limewakamata vijana
wapatao watano wanaojiita viongozi wa “Umoja wa Kikundi cha wahitimu wa mafunzo
ya Jeshi la kujenga Taifa” kwa makosa ya uchochezi na mikusanyiko isiyo halali
jijini Dar Es Salaam. Watu hao wanatabia ya kujikusanya kwenye kundi la vijana
wasiopungua 300.
Lengo la mikusanyiko hiyo ni kutaka kuandamana kwenda Ikulu kumwona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ili awapatie majibu
ya tatizo la ajira ya kudumu ambali ndiyo madai yao.
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa umoja huo hauna usajili kisheria na
hakuna ahadi yeyote ambayo kikundi hicho kimepewa.
Wanaohojiwa mpaka sasa ni pamoja na Mwenyekiti wa kikundi hicho aitwaye
GEORGE S/O GALUS MGOBA, Miaka 28, Mkazi wa Mabibo Loyola.
Mwingine ni Katibu wa kikundi hicho aitwaye LINUS S/O EMMANUEL, Miaka 28,
Mkazi wa Tabata.
Aidha, GEORGE S/O GALUS hivi sasa
amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa madai kwamba alitekwa nyara
huko Mabibo Mwisho tarehe 16/02/2015 hadi alipopatikana tarehe 19/02/2015
majira ya saa nne usiku huko Tumbi Kibaha kando ya barabara. Mtuhumiwa huyo
yupo chini ya ulinzi wa Polisi kwa makosa yaliyotajwa hapo juu.
Mnamo tarehe 22/02/2015 majira ya saa 11:45 jioni mtuhumiwa GEORGE S/O
GALUS akiwa chini ya ulinzi alijaribu kutoroka kutoka wodini katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili alikolazwa lakini Polisi walimbaini na kumkamata kabla
hajatokomea. Jalada la utoro chini ya ulinzi halali limefunguliwa na uchunguzi linaendelea.
Aidha tukio la mtuhumiwa
GEORGE S/O GALUS kudai kutekwa kati ya tarehe 16/02/2015 hadi 19/02/2015
linaendelea kuchunguzwa kwa ushirikiano kati ya Mkoa wa Pwani na Polisi Kanda
Maalum ya Dar es salaam ili kubaini ukweli wa taarifa hiyo na kuwajua
wanaosemekana kumteka.
KUJISALIMISHA
Wakati huo huo Makamu Mwenyekiti
wa umoja wa vijana waliohitimu JKT anayejulikana kwa jina la PARALI S/O ARUWERA
KIWANGO, Miaka 25, Mkazi wa Temeke Mikoroshini, anatakiwa kujisalimisha haraka
katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Polisi Kanda Maalum Dar es salaam au kituo
chochote cha Polisi cha karibu na mahali aliko. Mtuhumiwa huyo alitoroka baada
ya kugundua katibu wake amekamatwa hivyo anatakiwa ajisalimishe kuhojiwa kwa
matukio hayo.
Katika suala hili la wahitimu wa JKT, kuanzia sasa Jeshi la Polisi
litachukua hatua kali kudhibiti mkusanyiko au mkutano wa aina yeyote kwani
haina uhalali wowote kisheria. Imegundulika kwamba mikusanyiko ya vijana hawa
ni uchochezi na siyo halali kisheria hivyo haikubaliki. Yeyote atakayejaribu
kushiriki katika mkusanyiko wa aina hiyo awe ni kiongozi au mjumbe atachukuliwa
hatua kali haraka sana.
Mpaka sasa baadhi ya wajumbe wafuatao wamekamatwa kwa makosa ya
mikusanyiko hiyo ambao ni;
1. EMMANUEL S/O RICHARD, Miaka 28, Mkazi wa Kawe
2. JACOB S/O JOSEPH, Mika 36, Mkazi wa Mabibo
3. RIZIONE S/O NGOWI, Miaka 27, Mkazi
wa Mtoni Mtongani
4. LINUS S/O EMMANUEL, Miaka 28, Mkazi wa Tabata Katibu Mkuu
Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa makundi yeyote ya aina hiyo
kuacha kujitokeza na kufanya mikusanyiko au mikutano kwani mikutano ya aina
hiyo itachukuliwa ni kunyume cha sheria na hatua zitachukuliwa bila ajizi.
Uchunguzi wa awali wa mashauri hayo utakapokamilika majalada yao
yatapelekwa kwa mwanasheria wa serikali kabla ya kufikishwa mahakamani ili
sheria ichukue mkondo wake.
S. H. KOVA,
KAMISHNA WA
POLISI KANDA MAALUM
DAR ES
SALAAM
Hakuna maoni
Chapisha Maoni