LOWASSA AMESHINDIKANA,WABUNGE WA CCM WANAWA MIKONO,SOMA HAPA KUJUA
pichani ni Lowassa |
Mbio za kuusaka urais
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimezidi kupamba moto baada ya kundi la
wabunge wapatao 150 kujitokeza hadharani na kueleza kumuunga mkono mmoja wa
wanaotajwa kuwa wagombea, Edward Lowassa, wakimtaka kujitosa kwenye
kinyang’anyiro hicho.
Hali hiyo
inajitokeza wakati wa Mkutano wa Bunge wa 18 ukihitimishwa mwishoni mwa wiki na
kubakia miwili tu Bunge la 10 kufikia tamati, hivyo kwa kila hali uchaguzi mkuu
kuzidi kunukia kazi kubwa ikiwa ni kupatikana kwa rais wa tano wa Tanzania.
Kwa kitambo sasa
kumekuwa na makundi yanayosigana kila moja likiwa na mgombea wake, hata hivyo
mpambano mkubwa wa kumpata mgombea unaonekana kuwa zaidi ndani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kurithi mikoba ya Rais Jakaya Kikwete, anayehitimisha uongozi
wake wa utawala Oktoba mwaka huu kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Katika mbio hizo,
sasa ni rasmi kwamba kundi la wabunge wanaodaiwa kufikia 150 walikutana katika
chakula cha jioni mjini Dodoma eneo la Kilimani mwishoni wiki iliyopita wote
waliopata fursa ya kuzungumza katika hafla hiyo, walisema wazi kuwa wanamuunga
mkono Lowassa katika mbio za urais.
Lowassa ambaye
pia ni mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, anadaiwa kutakiwa na wabunge
hao kuwa muda ukifika achukue fomu za kuwania urais kwa tiketi ya CCM katika
uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Ingawa kumekuwa
na tetesi na minong’ono ya Lowassa kuungwa mkono ndani ya CCM kuwania nafasi
hiyo ya juu kabisa ambayo pia itampa fursa ya kuwa Mwenyekiti wa chama hicho,
uamuzi wa wiki iliyopita wa wabunge hao kusimama hadharani unaibua moto mkubwa
wa kinyang’anyoro cha urais huku jina la Lowassa likizidi kutajwa kama chaguo
la wengi.
Habari ambazo
chanzo changu imezipata zinasema kuwa wengi wa wabunge waliozungumza walitaja sifa
za kuwania urais, wakisisitiza kuwa Lowassa anazo na kwamba ni mtu pekee kwa
sasa wanaoona kuwa CCM inaweza kuingia kwenye uchaguzi ikiwa na uhakika wa
ushindi kama ataipeperusha bendera ya chama hicho.
Katika hafla
hiyo ambayo pia Lowassa anadaiwa kuhudhuria, mbunge mmoja mkongwe mkoani Kagera
(CCM), anadaiwa kusema kuwa wabunge marafiki wa Lowassa wanamuomba agombee
kutokana na kuwa na sifa zote za uongozi hasa katika zama za sasa ambazo taifa
linahitaji mtu wa kulikwamua.
"Mimi as a
senior citizen (kama raia mkongwe), huu ni mwaka muhimu, Oktoba tutakuwa na
uchaguzi mkuu wa kumchagua kiongozi atakayeisukuma mbele nchi yetu… sote
tunafahamu chama chetu bado hakijatangaza taratibu, lakini sisi wabunge
marafiki zako tunakuomba, muda ukifika chukua fomu kwa sababu unatosha,"
vyanzo vyetu vilimnuku mbunge huyo akimshawishi Lowassa katika hafla hiyo.
Mbunge huyo
anadaiwa kuainisha sifa muhimu za kiongozi kuwa ni mwenye elimu madhubuti,
uwezo wa kuona mbali (vision), muwajibikaji na mchapakazi, uwezo wa kutenda na
tabia nzuri, vitu ambavyo alisema kuwa Lowassa anavyo hasa akirejea rekodi yake
ya uwaziri mkuu kati ya 2005 hadi Februari 2008.
"Kule
kwangu wananiuliza yule waziri mkuu aliyeleta hizi shule za kata yuko wapi?
Mimi nawajibu atarudi tu. Na kila mtu mitaani anataja jina lako kwa hiyo sauti
ya watu (wengi) ni sauti ya Mungu," alisema mbunge huyo.
Wabunge wengine
ambao walipata fursa ya kuzungumza ni pamoja na Viti Maalum (Singida), Diana
Chilolo, mbunge shabiki wa klabu ya Simba atokaye mkoa wa Tanga(CCM), Mary
Chatanda wa Viti Maalum (CCM) na mbunge kutoka Ruvuma ambaye ni kada muhimu wa
kuipigia debe CCM katika kila kipindi cha uchaguzi.
Chilolo
anadaiwa kuungana na mbunge mkongwe kutoka Kagera, akisema kuwa Lowassa ni
chaguo la wengi, huku mbunge kutoka Tanga akinukuliwa akisema kuwa Lowassa ni
binadamu mwenye imani na upendo wa hali ya juu.
"Huyu mzee
mbali ya uwezo mkubwa wa kufanya kazi, lakini ana huruma... mimi niko tayari
kufukuzwa CCM kwa kumuunga mkono Lowassa,” alisema mbunge kutoka Tanga.
Pia mbunge huyo
(kutoka Tanga), anadaiwa kuahidi kuwa atatumia nafasi yake kuhakikisha kwamba
watu wote wanamuunga mkono Lowassa.
Mbunge huyo wa
Tanga anadaiwa kusema kuwa kwa kumuona Chatanda katika hafla hiyo,
kunadhihirisha kukubalika kwa Lowassa.
Chatanda ambaye
pia ni Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, inaaminika kuwa alikuwa hasimu mkubwa wa
Lowassa wakati akiwa katibu wa chama tawala mkoa wa Arusha.
Habari
zinasema kuwa Chatanda na Lowassa walikuwa na uhasama mkubwa na wote waliokuwa
wanamuunga mkono Lowassa mkoani Arusha walionja makali ya Chatanda.
Vyanzo vya habari
vilivyojipenyeza kwenye hafla hiyo iliyofanyika baada ya iliyokuwa imeandaliwa
na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, vinasema kuwa Chatanda mwenyewe aliposimama
kuzungumza alikiri kuwa alikuwa hamuungi mkono Lowassa pamoja na kwamba
wanafahamiana kwa muda mrefu, lakini sasa anaungana na wale wanaomuomba
agombee.
"Mimi na
Edward hatuna ugomvi, wapambe wake ndiyo walikuwa wanatuchonganisha, na kwa
kweli sikuwa kabisa namuunga mkono, lakini wagombanao ndiyo wapatanao…mimi sasa
hivi nimeingia mwili mzima kumuunga mkono Edward na hakuna wa kunitoa,"
chanzo chetu kinamnukuu Chatanda, akitangaza msimamo mpya wa kisiasa katika
makundi ya kusaka urais kupitia CCM.
Kutokana na msimamo huo mpya, habari zinasema kuwa Chatanda
alipigiwa makofi na wabunge wenzake.
Hata hivyo,
alipotafutwa na Chanzo changu kwa njia ya simu jana kuelezea tukio hilo,
Chatanda alikanusha vikali, akieleza kuwa hakuwapo kwenye chakula hicho na wala
hafahamu chochote kuhusiana na hafla hiyo.
"Mimi sikuwapo, na wala sijui kama hicho kitu kilikuwepo,
sijui chochote na wewe ndiyo kwanza unaniambia," alisema.
Naye Chilolo alipotafutwa, alikanusha kushiriki hafla hiyo,
akisema kwamba hata Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliandaa chakula cha jioni
siku hiyo lakini hakuweza kuhudhuria kwa sababu hakuwa anajisikia vizuri.
"Spika aliandaa chakula cha jioni, nasikia watu walikula,
walikunywa na kuserebuka... sasa ningewezaje kuacha kwenda kwa Spika niende kwa
Lowassa?" alisema Chilolo.
Naye mbunge kutoka Ruvuma ambaye alishatangaza siku nyingi kuwa
anamuunga mkono Lowassa katika safari yake kuelekea Ikulu, anadaiwa kusema kuwa
ushahidi wa kukubalika kwa Lowassa ulidhihirika wakati wa kilele cha sherehe za
miaka 38 ya CCM mjini Songea Februari Mosi mwaka huu, kutokana na kushangiliwa
na uwanja mzima mara alipowasili.
"Sikilizeni niwaambie... miye nilikuwapo uwanjani, wale
wengine wote hawakushangiliwa pamoja na kutembea mbali na jukwaa ili watu
wawaone. Lakini huyu Lowassa alivyoteremka mbele tu ya jukwaa kuu, uwanja mzima
ulilipuka," vyanzo vyetu vilimnukuu mbunge huyo akisema kwenye hafla hiyo.
Naye mbunge wa jimbo mojawapo linaloaminika kuwa ni ngome ya CCM
jijini Dar es Salaam ananukuliwa akimuelezea Lowassa kama kiongozi shupavu na
makini.
"Uwezo wake naujua... kwa kweli tunajifundisha mengi kutoka
kwake," alisema mbunge huyo.
Mbunge huyo kutoka Dar es Salaam alipotafutwa kwa njia ya simu
jana, alisema yuko msibani Kipunguni A kulikotokea maafa ya moto na kuteketeza
ndugu sita wa familia moja, hivyo asingeweza kueleza chochote.
Naye mbunge kutoka Zanzibar (CCM), anayesifika kwa kuwa mkali
kila mara linapofikia suala la kutetea maslahi ya visiwa hivyo, ananukuliwa
akimuomba Lowassa kukubali ombi lao kwani anatosha kwenye kiti cha urais.
Habari za ndani zinasema kuwa Lowassa ambaye hata hivyo
hajatangaza rasmi nia ya kuwania urais, aliposimama kujibu kauli za wabunge
hao, anadaiwa kusema suala la urais ni jambo zito hivyo kwa sasa anamwachia
kwanza Mungu.
"Ndugu zangu nafarijika sana kwa kauli zenu, lakini hili
suala la urais ni kubwa, tumuachie huyu aliye juu (Mungu), yeye akiamua liwe
linakuwa," vyanzo vyetu vilimnukuu Lowassa akisema wakati wa hafla hiyo.
Ombi la wabunge hao limekuja miezi michache baada ya matokeo ya
utafiti wa Taasisi ya Twaweza, kuonyesha kuwa Lowassa anaongoza kwa kukubalika
miongoni mwa watu wanaotajwa kuwania nafasi hiyo.
Matokeo ya utafiti huo ambayo yalitolewa mwishoni mwa mwaka jana
yalionyesha kuwa iwapo uchaguzi mkuu ungefanyika wakati huo, Lowassa angeibuka
mshindi kwa asilimia 13, wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, angefuatia kwa
karibu akiwa na asilimia 12 huku Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa
akiwa wa tatu kwa asilimia 11.
Hata hivyo, asilimia 33 ya wananchi waliohojiwa walisema
bado hawajaamua wampigie kura mgombea gani.
Utafiti huo wa Twaweza ulifanywa Septemba 2014 kwa kuwahoji
wananchi 1,445 kutoka Tanzania Bara.
CHANZO: NIPASHE
Hakuna maoni
Chapisha Maoni