WALIOTOA KINDUGU AJIRA ZA UHAMIAJI WALINDWA,NI WALIOWAPA WATOTO WAO,SOMA HAPA KUJUA
PICHANI NI VIJANA WASOMI MBALIMBALI WALIOJITOKEZA KWENYE USAHILI WA AJIRA ZA UHAMIAJI MWAKA JANA ZILIZOFANYIKA KWENYE UWANJA WA TAIFA AMBAPOA AJIRA HIZO ZILIZUA UTATA PICHA NA MAKTABA |
Serikali imeshindwa
kuwachukulia hatua watumishi wa Idara ya Uhamiaji nchini waliohusika na ajira
200 za upendeleo kwa nafasi ya Konstebo na Koplo, licha ya kamati ya uchunguzi
iliyoundwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, kubaini kashfa hiyo.
Katika uchunguzi
wake, kamati hiyo ilibaini kuwa walioitwa katika ajira hizo walikuwa ni ndugu
na jamaa za maafisa wa idara hiyo.
Hata hivyo,
akizungumza na Chanzo chetu jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa wizara hiyo,
Isaac Nantanga, alisema kuwa watumishi hao wameshindwa kuchukuliwa hatua kwa
kuwa hakuna ushahidi wa wazi uliopatikana kuthibitisha tuhuma za upendeleo
zilizoelekezwa kwao.
Alisema ndugu na
jamaa za maafisa hao walikuwa na sifa za kuajiriwa ndani ya idara hiyo na
hivyo, kukosekana kigezo cha kuwachukulia hatua.
Hata hivyo, alisema
Wizara ilitoa onyo dhidi ya waliohusika na mchakato huo kutokana na kutoa
mwanya wa kuzuka malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusiana na ajira hizo.
“Waliitwa kazini,
walistahili kuajiriwa, kwani walikuwa na sifa. Pia walistahili kuomba mara ya
pili, maombi hayakubagua, bali zilizingatiwa sifa tu,” alisema Nantanga.
Hata hivyo,
alisisitiza kuwa malalamiko ya kuajiriwa ndugu na jamaa za maafisa hao hayakuwa
na msingi wowote na kwamba, onyo la wizara limelenga kuwatahadharisha
waliohusika na mchakato huo ili tukio kama hilo lisijirudie tena ndani ya idara
hiyo.
Alisema watumishi
wa umma nao pia wanalindwa na sheria ya ajira, hivyo, hawawezi kufukuzwa kazi
kwa kutuhumiwa tu, lazima uthibisho uwasilishwe na mamlaka husika zijiridhishe.
Agosti 22, mwaka
jana, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil, alizungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam na kusema baada ya waombaji wa nafasi hizo
kufanyiwa usaili na kuitwa kazini, ziliibuka tuhuma mbalimbali zilizotolewa na
baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Tuhuma hizo zilihusu upendeleo wa ajira kwa ndugu na jamaa za
watumishi wa idara hiyo, hivyo wizara ililazimika kuzisitisha na kuunda kamati
ndogo ya watu watano ili kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai hayo.
Kamati hiyo ilipewa siku 10, kuanzia Agosti mosi, mwaka jana
kukamilisha kazi hiyo, ambayo waliifanya kwa muda waliopewa na kutoa matokeo.
“Katika uchunguzi wao, kamati imebaini kuwa baadhi ya wasailiwa
waliolalamikiwa wamethibitika kuwa ni watoto wa ndugu au jamaa wa watumishi wa
idara hii.
“Baadhi ya waombaji wa nafasi hizi, walikuwa na umri mkubwa
zaidi ya ule uliotajwa kwenye matangazo ya kazi (Konstebo miaka 25 na Koplo
miaka 30), lakini walisailiwa na kuitwa kazini,” alisema Abdulwakil.
Alisema baadhi ya wasailiwa waliopata alama za juu katika ufaulu
hawakuitwa kazini na hakuna sababu maalumu, ambazo zimetolewa, matangazo ya
kazi yaliyotolewa kwenye vyombo vya habari, yalikuwa ya jumla na hayakuainisha
viwango na madaraja ya ufaulu kwa waliomaliza kidato cha nne na sita.
Abdulwakil alisema kutokana na matokeo ya uchunguzi huo, ajira
hizo zimefutwa na zitatangazwa upya.
Awali, ajira hizo zilitangazwa na Kamishna wa Uhamiaji katika
Gazeti la Serikali, Februari 17, mwaka jana na kutoa tangazo hilo kwenye tovuti
ya wizara na idara ya Uhamiaji.
Baada ya kutangazwa ajira hizo, maombi 15,707 yalipokelewa na
waombaji 1,005 waliitwa katika usaili. Kati yao, 200 walishinda na kuitwa
kazini, lakini baada ya kutoa tangazo la kuitwa kazini, malalamiko yalitolewa
kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuwa walioitwa katika ajira hizi
ni watoto wa jamaa na ndugu
CHANZO GAZETI LA NIPASHE
Hakuna maoni
Chapisha Maoni