Zinazobamba

TANESCO YAENDELEA KUTOA ELIMU YA TEKNOLOJIA MPYA YA KUFUATILIA MATUMIZI YA UMEME MAJUMBANI KWA KUTUMIA SIMU YA MKONONI

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la shirika hilo lililopo katika maonesho ya sabasaba.

Na Mussa Augustine 

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limekuja na mfumo mpya wa teknolojia ya nyumba Janja(Smart House)utakaowapa wateja uwezo wa kufuatilia matumizi ya umeme majumbani kwa kutumia simu za mkononi, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema mfumo huo utamwezesha mteja kuona kifaa kinachotumia umeme mwingi zaidi ndani ya nyumba na kukizima akiwa popote duniani kupitia simu yake.

Akizungumza leo Julai 13,2026 and katika Banda la TANESCO kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Twange alisema amemweleza Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kuhusu ubunifu huo wakati alipotembelea banda la shirika hilo.

Alisema mfumo huo umebuniwa kufuatia malalamiko ya baadhi ya wateja waliokuwa wakieleza kuwa umeme unaisha haraka licha ya matumizi yao kuwa madogo, pamoja na changamoto zinazohusiana na usomaji wa mita na ukaguzi wa matumizi.

"Teknolojia hii itamwezesha mteja kufahamu kifaa kinachotumia umeme mwingi na kukidhibiti kwa njia ya simu hata kama yuko mbali na nyumbani," alisema Twange.

Aliongeza kuwa TANESCO ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuuzindua mfumo huo kabla ya kuanza kuusambaza kwa wateja nchini, akibainisha kuwa ni sehemu ya jitihada za wahandisi wa shirika hilo kutafuta suluhisho la changamoto zinazowasilishwa na wananchi.

Katika hatua nyingine, Twange alisema alimpa Rais Mwinyi taarifa kuhusu utekelezaji wa mkakati wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia mpango wa Bill Financing, unaowawezesha wateja kukopeshwa majiko ya umeme na kulipa gharama zake taratibu kupitia ununuzi wa umeme.Amesema mpango huo umepata mafanikio makubwa kwa kuwa zaidi ya asilimia 90 ya walionufaika wameuitikia vizuri, hali iliyowezesha TANESCO kushirikiana na sekta binafsi kuongeza upatikanaji wa majiko hayo.

Amewahimiza wananchi kuendelea kutumia umeme kwa shughuli za kupikia akieleza kuwa ni nishati yenye gharama nafuu na salama zaidi ikilinganishwa na nishati nyingine, huku akibainisha kuwa majiko ya kisasa yanayotumia umeme yameboreshwa ili kutumia umeme kwa ufanisi.

Twange pia amesema alimwelezea Rais Mwinyi maendeleo ya mradi wa kujenga njia mpya za kusafirisha umeme kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar kupitia nyaya zitakazopita chini ya bahari.

Amefafanua kuwa mradi huo utahusisha njia kutoka Dar es Salaam kwenda Unguja, Tanga kwenda Pemba na nyingine kuelekea Mafia,ambapo mhandisi mshauri anatarajiwa kupatikana mwezi Agosti na mkandarasi Januari,huku utekelezaji wake ukitarajiwa kukamilika ndani ya miezi 20 hadi 22.

Hata hivyo amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uwezo wa kusafirisha umeme kwenda Zanzibar na kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na kasi ya maendeleo ya kiuchumi na miundombinu visiwani humo.

No comments