Zinazobamba

LOWASSA NA WASAKA URAIS WENZAKE,KUPIGWA MSASA ITV,NI MPANGO WA KITILA MKUMBO-SOMA HAPA KUJUA


Pichani ni Profesa Kitila Mkumbo picha na Maktaba
Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa) kwa kushirikiana na kituo cha kurusha matangazo ya runinga na redio cha ITV/Radio One, wametangaza kuandaa midahalo itakayotoa fursa kwa wagombea urais wa vyama vyote vya siasa kuelekea katika uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika nchini kote mwaka huu.

       Hatua hiyo imefikiwa baada ya Udasa na ITV/Radio One kufikia makubaliano kuandaa midahalo hiyo, ikiwa ni sehemu ya mchango wao muhimu wa kijamii katika kufanikisha uchaguzi huo.

       Mwenyekiti wa Udasa, Prof. Kitila Mkumbo na Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na Radio One, Joyce Mhavile, walisema kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam kuwa vyama vyote vitakavyoshiriki katika uchaguzi huo na ambavyo vitasimamisha wagombea wa urais, vitaalikwa kushiriki katika midahalo hiyo.

      Taarifa hiyo ilieleza pia kuwa wagombea wote watakaojitokeza kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi huo, wataalikwa kushiriki midahalo hiyo.

       Ilieleza kuwa midahalo hiyo itaanza kwa kushirikisha wagombea ndani ya vyama vyao pale chama kitapokuwa na wagombea zaidi ya mmoja na baadaye kati ya wagombea watakaokuwa wameteuliwa na vyama vyao.

      “Utaratibu kamili wa midahalo hii utatolewa baadaye,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

       Iliviomba vyama vya siasa na wagombea wote watakaojitokeza kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi huo kushiriki katika midahalo hiyo ili kuwapa wananchi fursa ya kuwajua na wao kuwaeleza falsafa, sera na mikakati yao na ya vyama vyao katika kukabiliana na matatizo yanayoikabili nchi sasa na baadaye.

       Taarifa hiyo ilifafanua kuwa katika nchi za kidemokrasia, midahalo ya wagombea imekuwa ni sehemu muhimu katika kufanikisha uchaguzi ulio huru, haki, wazi na amani.

“Midahalo hutoa fursa muhimu kwa wagombea kueleza falsafa, sera na mikakati yao ya kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi na nchi zao,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

       Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa midahalo huwapa fursa ya kipekee wapigakura na wananchi kwa jumla katika kuwajua na kupima umahiri na weledi wagombea na vyama vyao.

           Kwa sababu hiyo, taarifa hiyo ilieleza kuwa midahalo imekuwa ni sehemu muhimu ya uchaguzi katika nchi zinazoamini na kuzingatia misingi ya demokrasia.

“Tafiti zinaonyesha kuwa midahalo ya wagombea urais ina nafasi ya kipekee katika kuwawezesha wapigakura kuamua mgombea gani wamchague na kwamba midahalo imekuwa ni chombo muhimu katika kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura kwa wingi,” ilieleza.

Hadi sasa ni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambako baadhi ya makada wake wametangaza nia ya kugombea huku wengine wakitajwa kuwa wana nia hiyo.

Waliotangaza nia ni pamoja na Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, January Makamba; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba; Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla; Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.

Wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na mawaziri  wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Wanatajwa pia Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Prof. Mark Mwandosya na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira.

VIONGOZI WA DINI
Wakati Udasa na ITV/Radio One wakitangaza hilo, Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Dar es Salaam imetangaza azma yake ya kukutana na wagombea watakaoteuliwa na vyama vyao na kupitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuwania urais katika uchaguzi huo, ili kuzungumza nao kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki na amani.

Pia imetangaza azma ya kutoa semina kwa wagombea wa nafasi hiyo, ili kuwaandaa kisaikolojia kukubaliana na matokeo yatakayotangazwa na Nec wanakuwa waadilifu na kuweka utaratibu mzuri kipindi cha uchaguzi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Sheikh Alhaad Musa Salum, alisema hayo alipozungumza katika mkutano wa kuratibu mipango ya mwaka 2015 katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu pamoja na upigaji wa kura wa ama kuikubali au kuikataa katiba iliyopendekezwa.

Alisema azma ya kutaka kukutana na wagombea hao kabla ya uchaguzi na kuwapa semina hiyo, inatokana na mitiririko wa matukio ya mara kwa mara ya upingaji wa matokeo, ambao umekuwa ukisababisha uvunjifu wa amani.

Aliwataka viongozi wa dini nchini kuepuka kujidhalilisha kwa kutumiwa na wanasiasa, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi huo, kwani ni hatari kwa nchi.

Alisema viongozi wa dini wanapaswa kuwa makini na kuacha kuonyesha uelekeo  na masuala ya itikadi, kwani jambo hilo linaweza kuleta mkanganyiko na kuwagawa Watanzania kutokana na imani zao.

Hata hivyo, kamati hiyo pia imepanga kukutana na wahariri wa vyombo vya habari kote nchini ili kuhakikisha wanaripoti habari za uchaguzi pasipo kuelemea upande mmoja ili kuepusha kuigawa nchi.

“Kamati yetu imejipanga vizuri kuhakikisha nchi inakuwa na amani, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na upigaji kura wa kuichagua katiba iliyopendekezwa kwa kuwahubiria wagombea wa nafasi ya urais juu ya amani, kwani wao ndiyo chanzo cha machafuko ya nchi,” alisema Alhaad ambaye ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema wakati wa uchaguzi, hasa kwa wagombea wa nafasi za urais, huwa chanzo cha kutokea vurugu pale matokeo yanapotangazwa kwa aliyeshindwa kutokukubaliana nayo.

Sheikh Alhaad alisema katika kuhakikisha nchi inakuwa salama na amani, kamati itawafuata wabunge bungeni na kuwapa semina ili wafahamu dhamana ya nchi ipo mikononi mwao, kwani wamekuwa wakiwagawa wananchi kutokana na vurugu wanazozizua bungeni.

Imam wa Msikiti wa Kigogo, Sheikh Jalala Mwakindenge, alisema jambo la uongozi wa dini ni kubwa sana, kwani wanashinda na waumini wao kwenye nyumba za ibada.

Kwa maana hiyo, alisema Taifa linahitaji sana viongozi wa dini kuliko wanasiasa, kwani ndiyo wahubiri wakuu wa amani kwa muda mrefu wakiwa makanisani.

“Kitendo cha kulingania amani ni kitendo cha ujasiri sana, kwa maana hiyo nawaomba mapadri, masheikh na maaskofu tuwe na msimamo mmoja wa kutetea nchi yetu isipoteze amani iliyopo,” alisema Mwakindenge.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa Dar es Salaam, Mchungaji Aman Lyimo, alisisitiza kuwa viongozi wa dini kuwa na kauli moja, hasa kipindi hiki, kwani kuna baadhi ya viongozi wameanza kujigawa kutokana na itikadi za vyama kitu ambacho ni chukizo mbele za Mungu.

Hatua ya kamati hiyo imekuja baada ya kuwapo kwa historia ya  vurugu na uvunjifu wa amani nchini, hasa kipindi cha uchaguzi mkuu kuibuka hisia za udini

Hakuna maoni