Zinazobamba

KAMANDA KOVA AUMBULIWA,NI PICHA YA PANYA ROAD,AMMBAKIA KESI MWOSHA MAGARI,SOMA HAPA KUJUA

Pichani Ni Kamanda Kova akionyesha picha ya Viongozi wa Panya Road a,bayo imezua kizaaza
Jeshi la polisi mkoani Dar es Salaam limezidi kuumbuka kutokana na tambo zake za kulishughulikia genge la kihalifu linaloundwa na watoto na vijana linalojiita ‘panya road’ kuonekana kuwa ni sinema baada ya baadhi ya wanaodaiwa kuwa ni watuhumiwa kuibuka hadharani na kulishangaa  jeshi hilo kuwachafua.

         Panya road ni vijana na watoto wenye umri kati ya miaka 15 na 30 wanaotumia silaha za jadi kupora sehemu mitaani na barabarani jijini ,ambapo wiki iliyopita walitikisa na kusababisha  biashara kufungwa na watu kikimbia ovyo mitaani.

        Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, amekaririwa mara kadhaa akitoa matamko kuhusu kundi hilo ambayo yapingana ama kupingwa, kuhusiana na ukweli wa kikundi hicho.

        Hivi karibuni aliibuka na orodha ya wahalifu akiwamo kijana Justine Mwacha (26) akidai kuwa ni miongoni mwa panya road hao, lakini kijana huyo amejitokeza na kushangaa kuwa jina na picha yake vilionyeshwa na Kova kuwa ni miongoni mwa washtakiwa 510 waliotiwa nguvuni na jeshi hilo.

     Mwacha alihojiwa jana na Chanzo change Jumamosi na kukanusha kukamatwa, huku akimtaka Kova kulifuta jina lake miongoni mwa yale aliyoyataja kuunda kikosi cha panya road.

       Katika hali ya kustaajabisha, kijana huyo anaelezea kushangazwa na tamko la Kova kumuingiza katika orodha hiyo huku akiwa huru na kujishughulisha na uoshaji wa magari pembeni mwa kituo cha polisi  cha Chang’ombe kilichopo Wilayani Temeke.

          Mwacha maarufu kama Dogo Lino anajishughulisha na uoshaji wa magari kwa zaidi ya miaka 10 katika kituo hicho.

        Alisema taarifa hizo zimemshtua na kumuweka katika hali mbaya, huku baadhi ya watu wakimkimbia na wengine kutokumpa kazi kutokana na jambo hilo. Mwacha alisema ili awe katika hali ya kiusalama, Jeshi la polisi linatakiwa kumsafisha kama ilivyotumika kumchafua.

       Akizungumzia jinsi polisi walivyofanikiwa kuipata picha yake, anaeleza kuwa mwaka jana  mwezi Marchi na April akiwa eneo la klabu ya Sugar ray iliyopo eneo la Sokota alikuwa anakunywa pombe.

        Anasema ilivyofika saa 7 usiku akiwa nje lilipita gari la polisi likiwa kwenye doria na kuwakamata baadhi ya vijana na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Chang’ombe.

       Anaeleza kuwa walilala kituoni hapo kwa siku moja na siku iliyofuatwa walipigwa picha na baada ya zoezi hilo kuisha walipewa adhabu ya kusafisha bustani pamoja na kufagia.

         Baada ya kukamilisha zoezi hilo ndipo waliruhusiwa kuondoka bila kufahamu kwanini wamepigwa picha.

“Hivi ndivyo polisi  walivyofanikiwa kuipata picha yangu na kuitumia katika tukio la panya road na kunidhalilisha kuwa wamenikamata wakati nipo mtaani naendelea na shughuli zangu za kuosha magari,” alisema.

        Alisema ameshangazwa na kauli ya Kova kudai kukesha saa 120 kuwasaka panya road huku akiwataja watu ambao hawahusiki na tukio hilo.

        Mwacha alisema siku ya tukio la panya road alikuwa kituoni hapo Chang’ombe na kwamba hapakuwepo na jambo hilo  mbali na kwamba kulikuwepo na habari za wahalifu hao kuleta taharuki jijini.

       “Nilikuwa hapa masikani na wenzangu  tukawa tunasikia watu wanasema panya road na wengine wanakimbia lakini sijawaona baadaye nashangaa kuona picha inaonyeshwa kwenye televisheni,” alishangaa Mwacha

         Aidha, alisema alipatwa na mshtuko kuona yupo kwenye vyombo vya habari wakati hajawahi kujihusisha na tukio la kihalifu.

        Alisema tukio hilo limemuathiri katika shughuli zake baadhi na watu kushindwa kumuamini tena na kwa upande wa ndugu wamevunja ukaribu naye kwa kuamini ni mhalifu.

“Baadhi ya watu ambao walikuwa wananipa kazi hawanipi  tena , ndugu zangu nao  wenyewe wamepunguza ukaribu nami  naanza kuogopa hata kupita mitaani,” alisema na kulilaumu jeshi kwa kuonea wanyonge.

Aliongezea kusema kuwa “Nashangazwa kuitwa panya road aliyekamatwa huku nikiwa naosha magari ya askari wa kituo cha Chang’ombe pamoja na ya wateja wengine.”

       Akizungumzia picha zilizoonyeshwa,  alieleza kuwa kuna wengine kama 10 wapo mitaani na wanaendelea na shughuli zao :“Ninamshangaa Kova kusema hajalala  saa 120 wakati wanaodaiwa kukamatwa wapo mtaani na hawajakamatwa kama anavyodai,” alisema

      Ndugu wa kijana huyo, Kaisi Shaban, alisema hajawahi kusikia Mwacha  akijihusisha na tukio la uhalifu mbali na kumuona akijituma kutafuta riziki Polisi Chang’ombe.

          Alisema siku ya tukio la panya road akiwa nyumbani Mbagala alipiga simu kwa marafiki wa ndugu yake kujua kama yupo salama ambapo aliwajulisha  kuwa hana tatizo.

          Mmoja wa madereva teksi , Mohamed Mawazo, alisema anamfahamu kijana huyo kwa zaidi ya miaka mitano na kwamba  wanamuachia magari yao.

        “Hata magari ya polisi kituoni hapo huwa anawaoshea kitendo cha kutangazwa ni miongoni mwa panya road ni kuhatarisha maisha yake kwani tangu nimjue sijawahi kumsikia na matukio ya kihalifu na wala hana ugomvi na mtu,” alisema Mawazo 

KOVA AJITETEA
Kwa upande wake Kamanda Kova, alisema hajatoa picha za kijana huyo katika vyombo vya habari.

Alijitetea kuwa  kijana huyo anatakiwa kulishtaki gazeti la Amani ambalo limetoa picha yake na si kuilalamikia polisi.

Kamanda Kova alisema anachokifahamu ni kwamba miaka ya nyuma kijana huyo alikamatwa na kupigwa picha na polisi lakini si kwa kuhusika na panya

Hakuna maoni