WAZIRI TIBAIJUKA ATOA MASHITI,MAPOKEZI YAKE JIMBONI KWAKE YAWEKA HISTORIA SOMA HAPA KUJUA
pichani ni waziri Tibaijuka |
Siku nne baada ya Rais
Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, mwanasiasa huyo ametua jimboni kwake
na kupokelewa kwa mbwembwe na wananchi wa jimbo hilo huku akisema hajutii kung’olewa.
Jumatatu wiki hii, Rais Kikwete akihutubia Taifa kupitia mkutano
wa wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, alitangaza kumvua nafasi ya uwaziri
Prof. Tibaijuka kutokana na kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow ambayo yeye
(Tibaijuka) alipata mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni ya VIP Engineering and Marketing LTD, James Rugemalira.
Prof. Tibaijuka ambaye ni Mbunge wa Muleba Kusini kupitia Chama
Cha Mapinduzi (CCM), aliwasili jimboni mwake juzi ikiwa ni siku moja baada ya
kutimuliwa katika wadhifa wake na kupokelewa na wapigakura wake ambao
walimuahidi kumpa ushirikiano wakati akitekeleza majukumu yake jimboni akiwa
mbunge.
ALIVYOPOKEWA
Profesa Tibaijuka aliwasili mjini Bukoba kwa ndege na kupokelewa
na mamia ya wananchi na msafara wa mapokezi ulianza kuondoka katika uwanja huo
saa 7:00 mchana kuelekea kijijini kwake Kagabiro, wilayani Muleba.
Msafara huo ulikuwa na magari zaidi ya 35 na pikipiki 50
yaliyowabeba wapambe, wakereketwa na wanachama wa CCM.
Wakati wa msafara huo, wananchi hao walikuwa wakiimba nyimbo za
kumsifu Prof. Tibaijuka wakisema “ni jembe”.
Msafara uliwasili kijijini kwa Prof. Tibaijuka saa 10: 00 jioni
na wananchi waliohudhuria hafla ya kumpokea kutoa salamu wakimtakia afya njema
na kumuomba kuwa mvumilivu kwa yote yaliyojitokeza kutokana na kuvuliwa
uwaziri.
Wananchi hao walimweleza Prof.Tibaijuka kuwa licha ya Rais
Kikwete kumvua uwaziri, lakini wao wana imani naye katika kuwaletea
maendeleo jimboni humo.
“Mheshimiwa Mbunge, sisi wananchi wa jimbo lako bado tuna imani
nawe, tupo tayari kukupa ushirikiano kuhakikisha unatekeleza vyema yale yote
uliyoyapanga kuwaletea wanaMuleba,” alisema Josephat Rweyemamu wakati
akizungumza kwa niaba ya wananchi.
Rweyemamu alisema kuwa wananchi wa jimbo hilo walimchagua Prof.
Tibaijuka kuwa mbunge wao, hivyo kuvuliwa nafasi ya uwaziri haiwapi tabu kwani
hizo ni nafasi za ziada kwa kiongozi yeyote.
Naye Alhaji Shakiru Kyetema, alisema Prof. Tibaijuka hana sababu
ya kusikitika kutokana na kuvuliwa uwaziri kwani kuanzia sasa atapata muda
mzuri wa kuwatumikia wapiga kura wake tofauti na alipokuwa waziri.
Aidha, wananchi hao walimzawadia Prof.Tibaijuka zawadi
mbalimbali akiwamo ng’ombe dume aliyetolewa na Alhaji Shakiru kama ishara ya
kumpongeza kwa msimamo wake kama kiongozi mwanamke.
ATEMA CHECHE
Prof. Tibaijuka akizungumza na wananchi hao, aliwataka
wasisikitike kwa kuvuliwa kwake nafasi ya uwaziri kwani aliyetoa ndiye
aliyetwaa.
Alisema binafsi hajutii kuvuliwa cheo hicho kwani kama angekuwa
na tamaa ya cheo asingetoka Umoja wa Mataifa (UN) ambako alilazimika kuacha
cheo ili akawatumikie wananchi wa jimbo la Muleba.
“Najua wengi wenu mmeumizwa na masuala ya sakata la Escrow, niwaombe
yasiwaumize vichwa kwani Bwana alitoa na Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe,”
alisema Prof. Tibaijuka.
Prof. Tibaijuka alisema kimsingi, suala la yeye kupokea fedha
kutoka kwa James Rugemalira halina utata kwani fedha hizo zilitolewa kuwasaidia
kuwalipia karo baadhi ya wanafunzi wanasoma kwenye shule zake, hivyo hawezi
kuwa mbinafsi kama ilivyotafsiriwa na baadhi ya Watanzania.
“Watanzania tumejaa ubinafsi, kila mtu anafikiria kila anafanya
jambo anategemea kupata posho, na niwahakikishieni mimi sina uchu wa ubinafsi
wala tamaa za vyeo kwani kama ni cheo nilichoacha UN kilikuwa kikubwa zaidi,”
alisema akimaanisha ni cha ukamishna mkuu wa makazi.
Aliwahakikishia wananchi hao kuwa kwa sasa nguvu zake
anazirudisha jimboni na kila mwananchi atatambua kuwa yeye ni nani kwani
atahakikisha muda uliobaki jimbo lake linainuka kimaendeleo kuanzia kata kwa
kata hususani katika sekta ya elimu.
Aidha, aliwahadharisha watu wanaonyemelea jimbo lake kwa
kuwaambia wakae chonjo.
Kabla ya kuvuliwa uwaziri, Alhamis iliyopita Prof. Tibaijuka
aliitisha mkutano wa waandishi wa habari ghafla na kusema hawezi kujiuzulu.
Prof. Tibaijuka alisema kamwe hawezi kujiuzulu na pia anajivunia
na kuona fahari kupata fedha hizo. Kampuni hiyo ya Rugemalira ilikuwa mwana
hisa katika IPTL.
Alisema ni bora alivyopata fedha hizo na kuzipeleka katika shule
yake kwa ajili ya kusaidia shughuli za elimu kwa watoto wa kike wasio na uwezo.
Kutokana na hali hiyo, alisema anahitaji kusifiwa kwa ujasiri
wake wa kukiri kupokea fedha hizo na kuzitolea maelezo, ingawa alikosa nafasi
hiyo katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Alisema angejiuzulu iwapo ingethibitika fedha hizo za
Rugemalira, siyo halali.
Prof. Tibaijuka alisema fedha hizo hazijathibitishwa na serikali
kuwa siyo halali, kiasi cha yeye kutakiwa kujiuzulu nafasi yake serikalini.
Alisema fedha hizo hazina uhusiano kati yake na nafasi ya
uwaziri aliyonayo, kwani zilikwenda moja kwa moja kusaidia kulipa deni la Sh.
bilioni 2, ambazo moja ya shule zake ilikopa kutoka Benki M.
Prof. Tibaijuka alisema iwapo itabainika fedha hizo si halali
atakuwa tayari kuzirudisha.
“Iwapo fedha hizo zitathibitika siyo halali, Joha Trust
itazirudisha, kama taasisi inavyoitwa nia njema, sisi hatuhifadhi fedha zisizo
halali,” alisema Prof. Tibaijuka.
Alisema fedha hizo alizipokea Februari 12, mwaka huu, zilitokana
na maombi ya awali kutafuta michango kutoka kwa wafanyabiashara wa ndani na
wafadhili wa nje.
Alisema hoja kwamba, alipokea mchango mkubwa, haina uzito
kutokana aina ya mtu, ambaye alimpaa mchango huo na kusema ni mtu mwenye fedha
na pia ni mfanyabiashara.
“Labda mnafikiri unapoomba fedha kwa mtu kama Bill Gates
unategemea atakuchangia kama kiasi gani? Siyo senti.
Hata mimi nilipoambiwa na Rugemalira nikaangalie akaunti yangu
ina shilingi ngapi nakukuta fedha nyingi, nilijua leo nimeamkia mkono wa kulia.
Nilifurahi,” alisema Prof. Tibaijuka.
Alisema fedha hizo alichangiwa kwa ajili ya kulipa sehemu ya
deni la Sh. bilioni mbili anazodaiwa na Benki M baada ya kukopa kwa ajili ya
ujenzi wa bweni la shule lenye uwezo wa vitanda 163.
Alisema fedha hizo zimechangia maendeleo ya elimu kwa
kuwatengenezea wanafunzi mazingira bora.
“Hii kitu inabidi tuwe makini kama Taifa, kwani mimi nilikuwa
mtumishi Umoja wa Mataifa. Lakini sikuweza kubeba fedha. Na kuna mapesa kule.
Iwe katika nchi hii, ambayo nafahamu hata wapigakura wangu wa kule Muleba
Kusini na wakulima wanaishi maisha ya chini?” alihoji Prof. Tibaijuka.
Alisema uamuzi wa kuzitoa fedha hizo haraka katika Benki ya
Mkombozi, ulifikiwa na Bodi ya Wadhamini ya Joha Trust, ambayo ilitoa maamuzi
kwamba, zitumike kulipa deni la Benki M.
Hata hivyo, katika mkutano huo Prof. Tibaijuka
hakutoa nyaraka zozote zikiwamo risiti zinazoonyesha deni hilo lilivyolipwa
kupitia benki hiyo.
Prof. Tibaijuka alisema analazimika kutoa maelezo hayo katika
vyombo vya habari kutokana na kutopewa nafasi ya kufanya hivyo mbele ya PAC.
Alisema serikali bado haijathibitisha kuwa fedha za Rugemalira
ni haramu kiasi cha yeye kulaumiwa.
Kutokana na hali hiyo, alionya kuwa kujiuzulu kusiwe kama
mtindo, kwani fedha hizo hazikugusa utendaji kazi wake kama mtumishi wa
serikali.
Alisema mitandao inaendelea kuandika na asilimia kubwa
wakimtukana.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni