Zinazobamba

HUYU NDIYE MWANDISHI WA HABARI MSOMI KURIKO WOTE NCHINI,ACHUKUA PHD CHUO KIKUU HURIA NA KUJIWEKEA REKODI KUBWA NCHINI,SOMA HAPA KUJUA


DK HAMZA KONDO
Pichani ni hamza Kondo ambaye ni Mwanadishi wa Habari nchini aliyevunja rekodi kuwa mwanahabari msomi kuriko wote 
CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimekuwa chuo cha kwanza Tanzania tangu nchi ipate uhuru kutunuku shahada ya uzamivu ya mawasiliano ya umma (PhD in Mass Communication) kati ya vyuo vikuu vya serikali na binafsi vipatavyo 61 vinatambulika na Kamisheni ya elimu ya juu Tanzania (TCU).
Mtanzania wa kwanza kutunukiwa shahada hiyo katika mahafali ya 26 ya chuo hicho, yaliyofanyika Bungo, wilayani Kibaha, Pwani ni Dk. Hamza Khalifa Kondo.
Dk. Kondo ambaye pia alikuwa Mhadhiri Msaidizi katika Idara ya Uandishi wa habari na Mawasiliano ya Umma katika kitivo cha sayansi ya Jamii (FASS) wa chuo hicho, ana historia ndefu katika tasnia ya habari hapa nchini.
Dk. Kondo sio tu Mhadhiri, lakini pia ni mpiganiaji wa mstari wa mbele wa uhuru wa habari Tanzania, kwani ndio Rais wa Chama cha Uandishi wa Habari Tanzania (Taja).  Mwenyekiti wa kwanza  na muasisi wa kwa Taja, alikuwa Rais mstaafu wa awamu ya tatu, William Mkapa.
Dk Kondo anasema katika utafiti wake wa miaka minne, ametafiti kama kuna uwezekano wa kuweka kipengele cha sheria katika katiba ya Tanzania cha uhuru wa kupata habari (FOI) bila ya kuingiliwa na sheria yoyote.
Pia utafiti wake umetoa njia sahihi za namna ya kupata haki hiyo muhimu katika kujenga demokrasia.
Anasema utafiti wake pia umetoa majawabu kuhusu kutokuwepo kwa kipengele (Constitution Article) cha uhuru wa habari madhara yake ni kuujenga udikteta na ufisadi kufichika kwa sababu habari za serikali zinakuwa siri za mafisadi.
Kwa ujumla, Dk Kondo utafiti wake umetoa jawabu namna kipengele cha uhuru wa habari kinavyotakiwa kuwa katika katiba ya nchi yenye kuheshimu demokrasia kama Ghana, Nageria, Sweden, Marekani na Uingereza.
Katika utafiti wake, ameeleza huwezi kuweka kipengele cha uhuru wa habari katika Katiba halafu ukasema utatunga sheria ya kusimamia uhuru wa habari au uhuru wa vyombo vya habari uliyomo katika katiba, kufanya hivyo ni kuufuta uhuru ambao umeutoa na hivyo ndivyo yalivyo mapendekezo ya katiba mpya inayopendekezwa.
“Kwa bahati mbaya kutokana na kiwango kidogo cha taaluma ya  mawasiliano ya umma, waandishi wa habari wa Tanzania wamefurahia bila ya kuelewa hakuna uhuru wa habari katika katiba inayopendekezwa kwa vile umewekwa katika kifungu cha 31 (1-3), lakini ukaja kutolewa kijanja katika ibara ya 31(4).
“Ushahidi ni hata wakati wa Bunge maalumu waandishi wa habari walizuiwa kuhudhuria mijadala ya kamati, hapo hutakiwi kuwa na digrii kuelewa kwamba katiba inayopendekezwa hata na Jaji Warioba hakutupa waandishi wa habari uhuru wa habari,” anasema.
Kwa mujibu wa utafiti wa Dk. Kondo, rasimu ya katika tangu ya kwanza, ya pili na katiba inayopendekezwa, imewatosa wanahabari kwa kipengele 31(4) ambacho kimefuta kiaina uhuru uliotolewa katika ibara za 31(1-3).
Kutokana na hilo, anatoa wito kwa wanahabari wazingatie utafiti wake namna ya kupata uhuru wa habari kama unavyotambulika katika kujenga demokrasia. Mfano kule Ghana, Nigeria, Kenya, Sweden, Amerika na Uingereza.
Dk. Kondo katika fani ya uandhishi wa habari, alitunukiwa Diploma ya Uandishi wa Habari na Chuo cha Uandishi wa Habari hivi sasa SJMC mwaka 1981 na akapata  Diploma ya Sheria (ODL) Chuo Kikuu Mzumbe wakati huo (IDM) 1989. Mwaka 1993/94 alikuwa Strathclyde University Glasgow Uingereza akisomea cheti cha elimu ya mazingia (EE).
Mwaka 1997/98 alipa stashahada ya uandishi wa habari za mashirika ya habari ya kimataifa Chuo Kikuu cha JNU Taasisi ya elimu ya mawasiliano ya Umma New-delhi India, mwaka 1999 alikuwa Seattle Washington kwa kozi fupi ya mazingira.
Mwaka 2008 hadi Novemba 2009, alitunukiwa shahada ya uzamili ya mawasiliano ya umma katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT).
Anasema kwa kuwa alipata alama ya juu ya GPA 3.98, wahadhiri hususan Dk. Jemere Araka, alimshauri asichelewe kuchukua masomo ya PhD, ili kulisaidia Taifa katika masuala ya uhuru wa habari.
“Baada ya kupumzika mwaka mmoja 2011 nilijiandikisha kufanya PhD katika Chuo kikuu Huria cha Tanzania na kupata wasimamizi (supervisors) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambao ni Profesa Eno Akpabio na Dk. Masoud Nassor ambao ni mabingwa wa tasnia ya habari, sasa wameenda kufundisha chuo kikuu Namibia,” anasema.
Anaeleza miaka minne ilikuwa migumu, lakini inawezekana cha msingi amewaomba wanahabari wa Tanzania wasifanye kazi kwa mazoea, kwani uandishi wa habari ni taaluma kama taaluma nyingine.
“Ukimwona mtu anakwambia uandishi wa habari si lazima uusomee, kwanza elewa huyo mwenyewe ni kihiyo wa taaluma yetu. Pili, muulize hao wanaosomea duniani kote na hapa nchini mpaka wakuwa madaktari wajinga au wewe ndio mjinga?
“Mimi sina jibu ila watu wa aina hiyo tunao Tanzania na wengine eti wanaitwa ngulu hawana hata digrii. “Nguli”  ni mtaalaam wa kiwango cha juu (expert) sasa unakubali kuitwa nguli hata shahada ya fani hiyo huna tukuoneje?” anahoji Dk Kondo.
Anatoa wito kwa waandishi wa habari Tanzania kujiunga OUT ambayo mwaka huu imeanzisha kozi ya uzamili ya masafa ya mawasiliano ya umma kwa kuwa wanaweza kuendelea na masomo yao huku wakiendelea kufanya kazi zao binafsi au za kuajiriwa.
OUT chini ya uongozi wa Makamu wa Mkuu wa chuo, Profesa Tolly Mbwette kimejipambanua na kuwa chuo kikuu cha kwanza kuwa mstari wa mbele kushirikiana na wanahabari katika kupigania uhuru wa habari kitaaluma ambapo mwaka huu pamoja na kutunuku PhD kwa Dk. Kondo pia kimetunuku Shahada ya kwanza ya mawasiliano ya umma kwa wahitimu 55 na Shahada ya kwanza  ya uandishi wa habari  kwa wahitimu watano.
Historia ya Chuo kikuu huria inatia moyo katika familia ya waandishi wa habari Tanzania kwa vile kimekuwa cha kwanza kuonyesha njia kwamba nchi inaweza kuwaandaa waandishi habari mahiri wenye elimu ya juu kama nchi nyingine na kuachana na kuwa na waandishi makanjanja

Hakuna maoni