NI URAIS WA RUSHWA NDANI YA CCM 2015,MAKADA WAKE WAMWAGA PESA KAMA NJUGU ILI KUINGIA IKULU,KAGASHEKI ALIA NA LOWASSA,SOMA HAPA KUJUA
WanaCCM wakishangilia katika moja ya mikutano ya kampeni, Picha na Maktaba |
Ikiwa imebaki miezi 10 tu kabla ya
kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwakani, CCM kinaonekana kuteswa na tuhuma za
rushwa inayodaiwa kutolewa na makada wake wanaotajwa kutaka kuwania nafasi
mbalimbali ukiwamo urais.
Hali hiyo
inabainishwa na kauli za baadhi ya makada wa chama hicho katika ngazi
mbalimbali ambao wameamua kulalamika waziwazi ama kupitia vyombo vya habari au
kwenye mitandao ya kijamii.
Moja ya kauli
hizo ni ile iliyotolewa juzi na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki
kwenye akaunti yake ya Twitter akisema: “Mgawo wa Xmass na Mwaka Mpya kwa
wajumbe husika wa CCM ni kucheza na ugumu wa maisha uliopo. Ni ununuzi wa
nafasi na si uwezo wa uongozi. Aibu.”
Alipotakiwa
kufafanua kauli yake, Kagasheki alisema kwenye maoni yake hakutaja mtu licha ya
kwamba wapo wengi wanaotoa zawadi, lakini baada ya kuandika katika mtandao
ameandamwa na baadhi ya watu huku wengine wakimtolea lugha chafu.
“Hii ni line
yangu ninaitumia kutoa mawazo siku zote, lakini nimeshangaa leo watu wameshikia
kidedea maoni hayo mpaka wengine wanatumia lugha kali... sijamtaja mtu kwa
sababu najua wapo watu wengi wanaotoa zawadi,” alisema Balozi Kagasheki
aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii huku akisisitiza kuwa hayo ni
mawazo huru ambayo anayaamini.
Waliyonena kuhusu rushwa
Kauli ya Kagasheki
haina tofauti na zile zilizowahi kutolewa na makada wengine, akiwamo mwenyekiti
wake, Rais Jakaya Kikwete na wengine waliowahi kushika nyadhifa za juu ndani ya
chama hicho na Serikali yake juu ya kukithiri kwa rushwa katika kusaka
madaraka.
Makamu Mwenyekiti
wa CCM, Philip Mangula alimwambia mwandishi wetu jana kuwa suala hilo
linafuatiliwa kwa karibu na dawa yake itaiva Februari baada ya kamati yake ya
maadili iliyofuatilia kutoa tathmini yake.
“Tulipotangaza kuwafungia, tuliunda kamati ya ufuatiliaji
harakati za kila mmoja kuona je, yale tuliyomtaka kutoyafanya ametekeleza? Sisi
tunaheshimu vikao vyetu, hivyo tunasubiri kamati hiyo itakapotuletea taarifa
yake.
“Katika tathmini hiyo kama watakuwapo wa kusamehewa watasamehewa
na kama watakuwapo wa kuongezewa adhabu wataongezewa.”
Kauli ya Mangula ilikuwa inafafanua makada wa chama hicho
waliopewa onyo kali kwa kufanya kampeni mapema na kujihusisha na vitendo
vinavyokiuka maadili ndani ya chama na ndani ya jamii.
Mangula alisema hayo wakati kukiwa na madai kuwa baadhi ya
wanachama wake kudaiwa kugawa fedha kwa wajumbe wa mkutano mkuu na Halmashauri
Kuu ya Taifa (Nec) Zanzibar na maeneo mengine ya nchi.
Mangula jana alikaririwa na gazeti la CCM, Uhuru, akijibu madai
hayo kuwa, “hakuna mwanachama aliye juu ya katiba, kanuni na miongozo ya chama
na hivyo hakitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kutumia fedha.”
Kwa mujibu wa madai hayo, kada mmoja wa CCM anadaiwa kugawa kati
ya Sh1 milioni na Sh500,000 kama zawadi ya sikukuu ya Krismasi kwa wajumbe wa
vikao vya chama visiwani humo.
Mangula alisema kutokana na malalamiko hayo, CCM itapeleka timu
ya uchunguzi kupitia kitengo cha usalama na maadili kuchunguza tuhuma hizo.
Oktoba 25, mwaka jana Rais Kikwete alisema endapo rushwa
haitakomeshwa ndani ya CCM, kitaanguka vibaya katika Uchaguzi Mkuu 2015 na
iwapo kitanusurika hakitapita mwaka 2020.
Kauli hiyo pia inaungwa mkono na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick
Sumaye aliyewahi kuliambia gazeti hili kuwa iwapo misingi ya uchaguzi ndani ya
CCM itaendelea kulalia kwenye rushwa, hataendelea kuwa sehemu yake na kuonya
kuwa tatizo hilo limefikia pabaya na litakiangusha chama hicho.
Mwaka 2011, Rais Kikwete alitangaza mkakati wa ‘kujivua gamba’
akiwataka makada wa chama hicho wanaotuhumiwa kwa ufisadi kutafakari na
kujiondoa ndani ya siku 90, lakini hata baada ya muda huo kumalizika, mkakati
huo uliyeyuka na viongozi wakaanza kubadili maudhui yake.
Waliopigwa ‘stop’
Vigogo waliopewa adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano
na Uratibu), Stephen Wasira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini,
William Ngeleja.
Wanavyoitazama CCM
Wachambuzi waliozungumza na gazeti hili walisema CCM hakiwezi
kupambana na rushwa kwa sababu baadhi ya viongozi wake ni walarushwa na
wamekiondoa katika misingi ya kuwatumikia wananchi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally
alisema: “Chama hakiongozwi kwa makaripio, mkakati wa kujivua gamba na matamko
katika vyombo vya habari. Kinaongozwa kwa mifumo imara, fikra sahihi, dira na
historia yake nzuri.
“Ndiyo maana wanachama wa CCM wamekuwa wakitenda mambo kinyume
na katiba ya chama chao na hakuna wa kuwachukulia hatua. Kolimba (marehemu)
aliwahi kusema kuwa CCM haina dira wala mwelekeo. Hilo linaonekana sasa,
kimeshindwa kukemea rushwa.
Alisema ni vigumu kwa CCM kuikataa rushwa wakati baadhi ya
wanachama wake, tena wenye nyadhifa za juu ndani ya chama hicho wakituhumiwa
kwa rushwa.
“Mchawi yupo ndani ya CCM yenyewe. Profesa Tibaijuka ni mjumbe
wa Kamati Kuu na amepewa mgawo wa escrow lakini chama kipo kimya. Jimbo la
Bukoba Vijijini limegawanyika kwa sababu ya rushwa inayotolewa na wanaotaka
ubunge, hayo yote CCM hawayaoni na kukimbilia yanayotokea Zanzibar,” alisema.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema: “CCM
ni chama ambacho kinajibu mapigo ila hakitoi mapigo. Kinachotokea sasa ni
dalili mbaya kwake kwani kimekuwa dhaifu katika kuwashughulikia wanachama wake
wasio waadilifu.”
Alisema matamko mengi ya chama hicho ni ya kisiasa zaidi na
mengi huishia katika vyombo vya habari. “Hayo yanamaanisha kuwa uwezo wa CCM
umepungua. Mfano ni Chadema kwa sasa kinatoa mapigo na si kujibu mapigo pekee.
Hiyo ndiyo inatakiwa kufanywa na chama cha siasa,” alisema.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema Mangula
alipotangazwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM aliahidi kupambana na rushwa na
mpaka leo kashindwa.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni