MAUJI YA DK MVUNGI YAITESA MAHAKAMA,DPP AWA BUBU ,SOMA HAPA KUJUA
Washtakiwa 11 wa kesi ya mauaji ya kukusudia ya Aliyekuwa
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi wamegoma
kushuka kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakishinikiza
kuelezwa jalada la kesi yao lipo wapi na imefikia katika hatua gani.
Sakata hilo limetokea leo majira ya saa 4:00 asubuhi, muda mfupi
baada ya Wakili wa Serikali, Peter Njike kumueleza Hakimu Mkazi, Hellen Liwa
kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa, upelelezi wake bado haujakamilika na
akaomba ipangiwe tarehe nyingine kwa kutajwa.
Baada ya wakili Njike kueleza hayo, mshtakiwa Longishu
Losingo alidai mahakamani hapo kuwa Desemba 16,2014 upande wa mashtaka
uliwaambia jalada la kesi yao lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), leo (jana)
wanatuletea hadithi, tunaomba watueleze uhalisia wa kesi hii, tupo gerezani
tunateseka.
Kwa upande wa mshtakiwa Masunga Makenza naye alidai kuwa yeye
hafahamu sheria, kesi yao ni ya muda mrefu na akahoji jalada likienda kwa
DPP linatakiwa kukaa kwa muda gani.
Makenza alidai kuwa kesi yao ni ya kubambikiwa na kwamba
ingekuwa ni kesi halisi upande wa mashtaka ungekuwa umekwisha kamilisha
upelelezi wao na kwamba wao wapo tayari kushtakiwa ila kama upande wa mashtaka
umeshindwa kukamilisha upelelezi mahakama iwaachie huru, wakikamilisha
watawakamata tena.
Wakili wa Serikali, aliieleza mahakama kuwa wameyasikia
malalamiko hayo na kwamba yote yanajikita katika kuchelewa kukamilika kwa
upelelezi na kwamba watahimiza na kufuatilia upelelezi ukamilike mapema.
Jibu hilo halikuwaridhisha washtakiwa hao, mshtakiwa Longishu
alisema “Tumechoka kwa kweli tumechoka hatuna ugomvi na mahakama wala magereza
ila tunaugomvi na waendesha mashtaka kama wameshindwa kukamilisha upelelezi
watupeleke polisi.”
Yote kwa yote washtakiwa hao, wakaiambia mahakama kuwa kutokana
na hoja hizo za upande wa mashtaka leo (jana) hawapo tayari kushuka kizimbani,
watakaa chini hadi waelezwe jalada leo lipo wapi na kesi imefikia katika hatua
gani.
Baada ya washtakiwa hao wote kugoma kushuka kizimbani na kukaa
chini wakisubiri kuelezwa hatma ya kesi yao, Hakimu Liwa aliwasihi
wakubali kuondoka kizimbani hapo kwa sababu yeye siyo hakimu husika
ameitaja tu kesi yao, wamsubiri hakimu husika, Waliarwande Lema wamueleze
malalamiko yao.
Maelezo hayo ya hakimu Liwa walikubaliana nayo na kwa pamoja
wakainuka na kuelekea mahabusu ya mahakama kwa ajili ya kupelekwa mahabusu na
kesi iliahirisha hadi Januari 13,2015.
Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Chibago Magozi
(32), John Mayunga (56),Juma Kangungu (29), Paulo Mdonondo (30), Mianda Mlewa
(40), Zacharia Msese (33), Msungwa Matonya (30), Ahmad Kitabu (30).
Kwa pamoja wanadaiwa kuwa Novemba 3, mwaka 2013,
walifanya kosa hilo la mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni
ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao walifanya mauaji hayo katika
eneo la Msakuzi Kiswegere lililopo eneo la Wilaya ya Kinondoni ambapo kwa
pamoja walimuua kwa kukusudia Dk Sengondo Mvungi ambaye alizikwa kijijini
kwake, Chanjale, Kisangara Juu
Hakuna maoni
Chapisha Maoni