Zinazobamba

BARAZA LA UWEZESHAJI LAWANUFAISHA WAKULIMA WA MPUNGA





Baadhi ya wakulima waliodhaminiwa na serikali kupitia baraza la uwezeshaji la Taifa wakiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi kutoka baraza hilo. unnamed5 
Mmoja ya Mkulima aliyefanikiwa kupata udhamini wa baraza la uwezeshaji akielezea mafanikio yake baada ya udhamini huo ikiwa pamoja na ujenzi wa nyumba ya kisasa na kununua trekta na vifaa kazi vingine.(Picha na Denis Mlowe)
…………………………………………………………………………………………
.
NA DENIS MLOWE, MADIBIRA
BARAZA la uwezeshaji Taifa limewanufaisha jumla ya wakulima 400 wa kilimo cha Mpunga wa bonde la Madibira wilayani Mbarali mkoani Mbeya kwa kuwadhamini kupitia benki ya CRDB tawi la Iringa na Madibira Saccos baada ya kupatiwa mkopo wa shilingi milioni 400 ambazo zimeweza kuwanufaisha katika kilimo cha mpunga kwa kununua vifaa vya kilimo na kukuza kipato.
Akizungumza na Tanzania Daima wakati walipowatembelea wakulima hao na kufanya ukaguzi wa udhamini huo mwishoni mwa wiki, Afisa Mwandamizi Mawasiliano ya Umma na Ushawishi kutoka Baraza la Uwezeshaji Taifa, Edward Kessy alisema kuwa lengo la udhamini wa serikali kwa wakulima hao ni kutekeleza mpango wa taifa wa matokeo makubwa sasa kuwawezesha wakulima kuinua kipato chao na kukuza uchumi wa nchi kupitia kilimo.
Kessy alisema kuwa kupita benki ya CRDB tawi la Iringa serikali wamewadhamini wakulima hao fedha hizo ambazo wanazikopa kupitia Madibila Saccos inayofadhiliwa na benki hiyo na wamepatiwa elimu ya kilimo cha kisasa ambacho kimewasaidia kuongeza uzalishaji mazao na kudhibiti tatizo la njaa wilayani humo.
“Baraza la taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi chini ya mfuko wake wa uwezeshaji mwananchi ambao unatekelezwa kwa kushirikiana na benki ya CRDB imeweza kuwadhamini wajasiriamali mbalimbali  kwa kupitia vyama vya kuweka na kukopa nchini kuweza kupata mikopo ambayo inakuwa mitaji katika kuendeleza biashara zao na kilimo kwa ujumla na itaendelea kutoa udhamini zaidi kwa mwaka wa fedha ujao’ alisema Kessy.
Alisema baraza hilo hadi sasa limeweza kutoa mikopo yenye thamani zaidi ya shilingi bilioni 7 kwa wajasiriamali mbalimbali na wakulima wa mazao mbalimbali na wakulima wa mpunga Madibira wamedhaminiwa shilingi milioni 400 ikiwa ni awamu ya kwanza kwa wakulima hao.
Awali wakulima hao waliishukuru serikali kwa udhamini huo uliowawezesha kujikwamua kiuchumi na kuongeza kipato cha familia sambamba na kuongeza mavuno ya mpunga kwa mwaka jana
Mmoja wa wakulima wa mpunga katika bonge la Madibila, Anchila Seleman alisema kuwa mkopo huo umewawezesha kukuza kipato na mavuno ingawa wanakumbana changamoto ya soko la zao la mpunga hapa nchini.
Alitoa wito kwa baraza la uwezeshaji kuendelea kutoa mikopo kwa wakulima kwa lengo la kuwanufaisha na kuwatafutia masoko nje ya nchi kuweza kuuza mpunga kwa faida tofauti na sasa ambapo soko limekuwa likiwadidimiza wakulima wadogo.
Kwa upande wake,Bruno Theodory Meneja Mahusiano wa benki ya CRDB tawi la Iringa alisema kuwa benki hiyo imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali kwa wakulima hao kupitia mahusiano mazuri waliyoweka na Madibira Saccos ambapo wakulima hujipatia mikopo kila mwaka kutokana na uanachama waliokuwa nao.
Alisema kuwa msimu wa 2013/2014 wakulima walionufaika na udhamini wa baraza la uwezeshaji ni zaidi ya 400 waliojipatia mkopo wa shilingi milioni 1 kwa kila mkulima na kuwasaidia wakulima kuzalisha mazao mengi zaidi tofauti na misimu iliyopia..

Hakuna maoni