TAIFA LAGAWANYIKA RASMI,KATIBA YA SITTA YAWAPASUA VIONGOZI WA DINI,,UMOJA WAO HUKO SHAKANI SOMA HAPA KUJUA
SIKU moja
baada ya marais wawili wa Tanzania kukabidhiwa Katiba inayopendekezwa, viongozi
wa dini za Kikristo na Kiislam wamehitimisha kikao chao wakiwa na siri nzito
kuhusu mustakabali wa taifa.
Baadhi ya
viongozi wa dini waliozungumza na Chanzo chetu, wamesema kuwa, “katiba
imependekezwa, lakini nchi imepasuka,” na kwamba, hata viongozi wa madhehebu
hayo makuu wamegawanyika vipande vipande.
“Viongozi wa
dini tunaelewana, lakini ukichunguza kwa undani utagundua kwamba tunatiliana
shaka. Katiba hii imetugawa. Kuna mtazamo miongoni mwetu kwamba Waislamu wa
Bakwata ni wa CCM, na maaskofu ni wa Ukawa,” alisema kiongozi mmoja wa Kiislamu
kwa sharti la kutotajwa jina.
Viongozi hao
walikutana kwa siku tatu jijini Dar es Salaam katika mpango wa uhusiano bora
kati ya Waislamu na Wakristo. Washiriki walikuwa Baraza Kuu la Waislamu
(Bakwata), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo
Tanzania (CCT), Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) na baadhi
ya mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.
Shura ya
Maimamu hawakualikwa katika mkutano huo, huku kukiwa na hisia miongoni mwa
Shura ya Maimamu na Wakristo kwamba, Bakwata inafanya kazi kama idara ya
Serikali.
Kwa mujibu wa vyanzo
vyetu kutoka kwenye mkutano huo, licha ya uhusiano mwema uliokuwapo, yalizuka
maneno ya chini chini kati ya baadhi ya maaskofu na masheikh, hasa lilipoguswa
suala la katiba.
Moja ya matukio
yaliyokuwa na mvuto ni lile lililohusisha Sheikh mmoja wa Temeke, Dar es Salaam
(jina tunalo), na Askofu mmoja kutoka Kanda ya Ziwa (jina tunalo).
Sakata lao
lilianza pale Sheikh huyo alipowatuhumu maaskofu kwamba wanatoa matamko
yanayokaa ki-Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi), kuhusu Bunge Maalumu la
Katiba; na kwamba inawezekana maaskofu wanafanya hivyo kwa kuwa viongozi wa
Ukawa, Freeman Mbowe na James Mbatia ni Wakristo.
Ndipo Askofu huyo
naye akahoji, “Kwa hiyo unataka kusema Ukawa ni ya Waktristo? Hivi nyie
Waislamu mnaunga mkono hoja za CCM kwa kuwa ni ya Waislamu? Na kama unasema
Ukawa ni ya Wakristo, unasahau kwamba mwenyekiti mwenza wa Ukawa mmojawapo ni
Profesa Ibrahim Lipumba? Lini tumembatiza akawa Mkristo? Na hao wabunge wa CUF
wote walio Waislamu, wamebatizwa lini?”.
Taarifa zinasema
kuwa, baada ya maswali makali hayo ya Askofu, ilimlazimu Sheikh huyo kutoka nje
kwa muda, huku Sheikh mwingine akimsihi Askofu huyo amsamehe mwenzake, kwa
maelezo kuwa ameteleza kauli.
Hata hivyo,
jana wakati akisoma tamko la pamoja la viongozi hao mbele ya waandishi wa habari
katika Hoteli ya Whitesands, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Yuda
Thadeus Ruwaichi hakugusia mvutano huo, na hakuwa tayari kuulizwa swali lolote.
Walioambatana
na Askofu Ruwaichi kwenye tamko na kukataa kujibu maswali walikuwa ni Katibu Mkuu
wa Baraza la Maaskofu Katoliki, Padre Raymond Saba, Sheikh Hassan Kabeke wa
Bakwata, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga na kwa niaba ya CCT
alikuwepo Mchungaji Leonard Mtaita.
Katika tamko
lao, viongozi wa dini wamesema kuwa wataendelea kuongoza na kusimamia jamii zao
katika kujenga na kusimamia maadili mema, kuongoza jamii kuwa mfano bora na
kuchukua dhamana ya kuhamasisha na kusimamia utu, uhai na ustawi kwa wote.
Vile vile,
wamesema wataendelea kutetea dhana ya serikali kutokuwa na dini, bali raia wa
nchi hii ndio wawe na dini, hivyo kusaidia kutumia vyema uhuru wa kuabudu kwa
kuzingatia sheria za nchi kwa lengo la kulinda umoja, amani na mshikamano wa
kitaifa.
Wameshauri na
kuihimiza serikali iendeleze misingi ya utawala bora, na ihakikishe kuwa
rasilimali za taifa letu zinatumika katika kuwanufaisha na kuwaunganisha
wananchi.
Wamekemea
serikali kwa kutumia mabavu na silaha kugombanisha na kugawa wananchi; kwamba
si busara kutumia mabavu kama njia ya kutatua migogoro katika jamii.
Wakati huo
huo, maaskofu wanaounda Jukwaa la Makanisa, wamesisitiza kwamba tamko walilotoa
dhidi ya mchakato wa Katiba Mpya na mwenendo wa Bunge la Maalumu la Katiba ni
wa kinabii na uzito wake uko pale pale, licha ya kubezwa na aliyekuwa
Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta.
Maaskofu hao,
wameazimia kuusambaza tena jinsi ulivyo na kutia saini zao kama kielelezo cha
kauli yao ya pamoja dhidi ya wale wanaoupinga.
Walisema lile ni
tamko lao la pamoja na wapo tayari kuingia katika historia ya kuwataka waumini
wao kukataa katiba iliyopendekezwa, kwa kuwa haiwakilishi maoni ya wananchi
bali ya watawala
Chanzo ni
Gazeti Makini la Tanzania Daima
Hakuna maoni
Chapisha Maoni