MBOWE NI JEURI AIGOMEA MAHAKAMA MARA NNE,HAKIMU ANYWEA.SOMA HAPA KUJUA ZAIDI
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, jana alikwama kwa mara ya nne mfululizo kufika katika Mahakama ya Wilaya ya Hai kutoa utetezi wake kwenye kesi inayomkabili ya kumshambulia mwangalizi wa ndani wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Mbowe anadaiwa kumshambulia mwangalizi huyo, Nassir Yamin, katika Kijiji cha Nshara, Kata ya Machame Kusini, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimnajaro mwaka 2010.
Jana Mbowe alitakiwa kutoa utetezi wake mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Denis Mpelembwa, ambaye hata hivyo na yeye hakuweza kutokea mahakamani hapo kwa maelezo kwamba yupo kwenye mapumziko mafupi.
Akitaja kesi hiyo kwa niaba ya Hakimu Mpelembwa), Hakimu Agness Mhina alisema kutokana na udhuru uliotolewa na upande wa utetezi, kesi hiyo sasa itatajwa tena mahakamani hapo Novemba 6, mwaka huu.
Mahakama hiyo ilimkuta Mbowe na kesi ya kujibu baada ya mashahidi saba wa upande wa mashtaka kufanikiwa kuishawishi mahakama hiyo kwamba siku ya tukio hilo kulikuwa na tafrani iliyojitokeza, jambo ambalo Mbowe atatakiwa kulitolea ufafanuzi.
Julai 18, mwaka huu, Mbowe alitoa udhuru kwamba gari lake liliharibika na kuchelewa ndege wakati Agosti 18 alitoa udhuru wa kuachwa na ndege jijini Dar es Salaam na Septemba 8, mahakama hiyo iliahirisha shauri hilo na kumpa fursa Mbowe kushiriki mkutano wa kutafuta mwafaka baina ya vyama vya siasa vyenye wabunge kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania na Rais Jakaya Kikwete kuhusu mchakato wa Katiba mpya.
Jana Mbowe alitoa taarifa ya udhuru wa kuhudhuria shughuli za kisiasa ambazo hata hivyo hazikutajwa.Katika kesi hiyo, Mbowe anatetewa na Mawakili wawili ambao ni Albert Msando na Issa Rajabu.
Katika uchaguzi huo, Mbowe aliibuka mshindi wa ubunge Jimbo la Hai kwa kupata kura 28,585 akifuatiwa na Fuya Kimbita (CCM) aliyepata kura 23,349, Hawa Kihogo (UDP) 258 na Petro Kisimbo (TLP) 135.
CHANZO: NIPASHE
Hakuna maoni
Chapisha Maoni