HABARI ILIYOTIKISA JIJI-- JAJI WARIOBA AMSHUSHUA PINDA, ASEMA NI UNAFIKI KUSEMA RASMU PENDEKEZWA IMEBEBA ASILIMIA 80 YA MAONI YA TUME
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Alisema muundo wa serikali mbili hauwezi kuendelea kwa sababu haiwezekani kuwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano, isiyovuka bahari.
Akizungumza na NIPASHE ofisini kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam jana, Jaji Warioba alisema pia kwamba haoni kama Wazanzibari watakubali kuipitisha Katiba pendekezwa kwa kuwa Ibara ya 294 inataka Katiba ya Zanzibar ifanyiwe marekebisho ili iwiane na Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Alisema wananchi wa pande zote walieleza namna kero za Muungano kwa kina na ndiyo maana Tume yake ikapendekeza muundo wa Serikali tatu kama mwarobaini wa matatizo hayo.
MALALAMIKO YA ZANZIBAR
Alisema malalamiko makubwa kutoka Zanzibar ilikuwa kwamba; la kwanza, wanaona Tanganyika imevaa koti la Muungano kwamba kwa hali ilivyo, wanaofaidi Muungano ni Tanganyika.
Pili, walisema kuongezeka kwa mambo ya Muungano kunapunguza mamlaka ya Zanzibar kusimamia mambo yake.Tatu, kufuatana na makubaliano ya hati ya Muungano, rais wa Zanzibar awe makamu wa rais.
“Katika haya, Bunge Maalum limekubali kupunguza mambo ya Muungano; kwa hiyo katika orodha mpya mambo yote ya uchumi yameondolewa kwenye orodha ikiwa ni pamoja na biashara, mikopo ya nje, takwimu, utafiti na kwamba hata sensa haitakuwa mambo ya Muungano.”
Jaji Warioba alisema sensa ndiyo msingi wa mipango ya maendeleo, lakini sasa baada ya kuondolewa kwenye Muungano, kila upande utashughulikia sensa yake na pia Zanzibar wameridhika na sasa watasimamia uchumi wake kikamilifu na pili imekubalika rais wa Zanzibar atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Mimi naamini, mabadiliko haya hayataisaidia Zanzibar kwa sababu kwa kuondoa mambo yote ya uchumi, Zanzibar ikasimamia mambo yake maana yake ni kwamba serikali ya Muungano itakuwa inasimamia mambo ya Tanganyika tu ndiyo hapo Tanganyika itakuwa imevaa koti la muungano,” alisema Jaji Warioba.
Aliongeza: “Haiwezekani ukasema una serikali ya muungano ambayo haivuki bahari na ndivyo ilivyo sasa na ndiyo yalikuwa malalamiko kwa sababu Serikali ya Muungano haivuki bahari.”
Alisema wananchi wa Bara wanajua kwamba mambo yote yanayowahusu yanashughulikiwa na serikali ya Muungano ikiwamo elimu, afya, maji, barabara na mambo mengine wakati sivyo ilivyo kwa wananchi wa Zanzibar.
“Kwa wananchi wa Zanzibar hakuna hata moja kati ya haya linashughulikiwa na Serikali ya Muungano.”
Alitoa mfano kwamba ndio maana hata kama Waziri wa Ujenzi au wa Uchukuzi wa Bara, hata kama angekuwa ni mtendaji mzuri kiasi gani, hawezi kwenda Zanzibar.
“Hujaona Waziri anavuka kwenda Zanzibar kufanya kazi. Utawaona kwa mfano Magufuli anafanya kazi sana huwezi kumsikia amevuka kwenda Zanzibar. Mwakyembe atatembelea bandari ya Dar es Salaam, lakini hujamsikia amevuka kwenda Zanzibar; kwa sababu Serikali ya Muungano haina madaraka Zanzibar.”
Alisema: “Kwa hiyo huwezi kusema una serikali ya Muungano ambayo haina madaraka upande wa Zanzibar.”Pili, hii serikali ndiyo inayo hodhi sovereignty, sovereignty ya nchi iko chini ya serikali ya Muungano, ndiyo inayojulikana duniani kwamba serikali ya Tanzania ni Serikali ya Muungano.
Alisema rasilimali za Bara ndizo rasilimali za Serikali ya Muungano, hivyo hata inapotaka kukopa hutumia rasilimali hizo na kwamba itakopa kwa ajili ya Bara na kutafuta rasilimali kwa ajili ya Bara pia bila kuhitaji kibali chochote.
Alisema kwa upande wa Zanzibar ni kinyume chake, kwa kuwa haina haki ya kukopa bila kupitia Serikali ya Muungano.
Alisema hiyo ni kwa sababu rasilimali za Zanzibar haziko chini ya serikali ya Muungano hivyo ili ikubali kukopa kwa ajili ya Zanzibar lazima itake dhamana na kwamba hata katika Katiba pendekezwa, Zanzibar itaendelea kuwa na tatizo hilo.
Kuhusu Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, alisema wakati waasisi wa Taifa walipokuwa wanaunganisha vyama vya Afro-Shiraz na Tanu, waliunganisha mambo mengi yaliyolenga kuunda Serikali ya Muungano.
“Kabla ya hapo kulikuwa na rais na makamu wawili; Makamu mmoja ambaye alikuwa makamu wa kwanza alikuwa Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu. Tukasema ukifanya hivi hutaunganisha nchi, ni lazima anayemsaidia rais amsaidie kwa nchi nzima.”
Alisema baada ya kubaini ugumu huo, marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, yaliondoa nafasi za makamu wawili wa rais na kuweka sharti kwamba rais akitoka upande mmoja wa muungano, makamu wake atoke upande wa pili.
Alitoa mfano kwamba wakati ule, rais wa Jamhuri alikuwa Hayati Mwalimu Julius Nyerere (Bara) na Makamu wake akawa Rais wa Zanzibar na wakafuta Waziri Mkuu asiwe makamu wa rais.
Alisema mwaka 1984, upande wa Bara ulidhani Waziri Mkuu atakuwa ni nafasi ya Bara peke yao na wakaamua kuirudisha kwamba naye awe Makamu wa Rais.
Alisema alipoteuliwa kushika wadhifa huo nafasi hiyo mwaka 1985 ilikuwa imerudishwa, lakini mwaka 1992, walibaini kwamba maamuzi hayo yalirudisha nyuma azma ya Muungano, hivyo wakaamua kumwondoa Waziri Mkuu kwenye wadhifa wa Makamu wa Rais kwa nia ya kutoa fursa kwa viongozi hao watoke upande wowote wa Muungano.
Alisema kurudisha makamu wa rais watatu kunafanya wakati wote Rais wa Jamhuri ya Muungano atoke Bara.Ibara ya 99 ya Katiba pendekezwa inaeleza kuwa kutakuwa na Makamu wa Rais watatu ambao watakuwa:
(a) Makamu wa Kwanza wa Rais;
(b) Rais wa Zanzibar ambaye atakuwa Makamu wa Pili wa Rais; na (c) Waziri Mkuu ambaye atakuwa Makamu wa Tatu wa Rais.
“Kwa sababu haiwezekani kwamba ukawa na marais wawili; Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri wote wanatoka upande mmoja na hasa kwa kuwa huyu Rais wa Muungano anashughulikia zaidi mambo ya Bara; kwa utaratibu huu ni kwamba utafanya haitawezekana tena kupata rais kutoka Zanzibar.”
Alisema Zanzibar pia haitaweza kutoa Waziri Mkuu kwa kuwa makamu watatu wanaliopendekezwa mmojawapo ni mgombea mwenza ambaye lazima atoke Zanzibar kwa kuwa rais atatoka Bara, mwingine ni Rais wa Zanzibar na mwingine ni Waziri Mkuu ambaye haitawezekana naye akatoka Zanzibar.
Alisema kwa utaratibu huo, kama taifa tunarudi nyuma kwa kuwa ile dhana ya kiongozi atoke upande wowote ule kiuhalisia haitawezekana.
“Kwa hiyo kwa kufanya hivi mimi sioni kama Zanzibar wamepata faida yoyote.”
Alisema katika mambo ya Muungano, suala la kodi ya mapato yanayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa amabzo zimekuwa za Muungano.
Alisema mgogoro wa kwanza kuhusu Muungano ulitokana na masuala ya mapato na sababu zake zinaeleweka.
“Zanzibar imepewa mamlaka kuendesha uchumi wake, kwa hiyo ni lazima iwe na mapato. Vyanzo vikubwa vya mapato ni hivi vilivyotajwa; kodi ya mapato, ushuru wa bidhaa na ushuru wa forodha. Huwezi kuipa madaraka kisha ukainyang’anya uwezo wa kifedha hiyo ndiyo inayoleta mgogoro.”
Alisema mwaka 1977 iliamuliwa kwamba kodi hizo zinazopatikana Zanzibar zisiletwe kwenye serikali ya Muungano na kwamba ndivyo ilivyo hadi sasa.
Alisema Zanzibar haitaweza kujiendesha bila kodi kwa kuwa nusu ya mapato yao yanatokana na kodi hizo na kwamba mapendekezo yaliyopo kwenye Katiba hayatatekelezeka.
“Na Zanzibar watalikataa. Mimi nadhani hapa wamekosea (BMK). Tume ilipendekeza ushuru wa bidhaa ndiyo iwe kodi ya Muungano kwa sababu kwa upande wa Bara ndio chanzo cha pili kwa ukubwa.”
Alisema mwaka 2012/13; ushuru wa bidhaa uliingizia Bara mapato ya Sh. trilioni 1.3 lakini Zanzibar ilikusanya Sh. bilioni 11 na kwamba fedha hiyo ni kidogo ambayo Zanzibar ingeweza kuchangia kwa kuzingatia kuwa masuala mengi ya Muungano yapo zaidi Bara kama jeshi.
“Matatizo ya Zanzibar hasa kuhusu mikopo na misaada yatakuwa makubwa zaidi. Uhuru wa mahusiano wa mahusiano ya kikanda na kimataifa nao utakuwa mdogo; Zanzibar haiwezi kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Afrika, Sadc, OIC, UN na mashirika yake, kwani uanachama unahitaji sovereignty,” alisema.
MALALAMIKO YA BARA
Alisema wakati wa kukusanya maoni, wananchi wengi wa Bara walilalamikia mabadiliko makubwa ya Katiba ya Zanzibar kwamba imeingilia Katiba ya Muungano kwa kuwa sheria zinazopitishwa na Bunge la Jamhuri haziwezi kutumika Zanzibar bila kuidhinishwa na Baraza la Wawakilishi.
Pili, alisema wananchi wa Bara hawana haki ya kumiliki ardhi Zanzibar na pia hawana haki ya kuchaguliwa au kupiga kura; wakati ni kinyume chake kwa wananchi wanaotoka Zanzibar ambao wanaishi Bara.
Kadhalika, Mahakama ya Rufani haina madaraka Zanzibar, mashauri yanayotokana na haki za binadamu na Mahakama za Kadhi. Pia Katiba ya Zanzibar inavitambua visiwa hivyo kama nchi kamili.
Hata hivyo, alisema inawezekana wajumbe wa BMK walikubaliana ndani ya Bunge mambo kadhaa ambayo hawakutaka kuyaweka hadharani hasa suala la kuirekebisha Katiba ya Zanzibar.
Ibara ya 294 ya Katiba pendekezwa inaeleza kuhusu mambo ya mpito ikiwamo:
(a) kurekebisha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 ili kuwiana na masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 2014;
(b) kutunga na kurekebisha sheria mbalimbali za Jamhuri ya Muungano, sheria ambazo si za Muungano zinazohusu Tanzania Bara na sheria za Zanzibar ili kuwiana na masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 2014.
“Kwa kuwa ardhi imeingizwa kwenye Katiba basi Zanzibar italazimika kubadili sheria yake ili raia wote wawe na haki sawa. Pia sheria za uchaguzi nazo zitabadilika ili raia wote wawe na haki za kiraia. Kama mabadiliko hayo yamekubalika Zanzibar basi wananchi wa Tanzania Bara hawatakuwa na malalamiko yoyote ya msingi,” alisema.
Jaji Warioba aliongeza: “Tatizo ninaloliona mimi ni ugumu wa kufanya mabadiliko haya. Katika taarifa ya Tume tulisema kama kuna jambo ambalo tuliona Wanzanibari wameungana ni Zanzibar kuwa nchi. Ili mabadiliko yafanyike kwenye Katiba ya Zanzibar ni lazima yapatikane maridhiano, pasipo na maridhiano Baraza la Wawakilishi halitapata kura za kutosha kupitisha marekebisho.”
“Hali itakuwa ngumu zaidi kwenye kura ya maoni kama Katiba ya Zanzibar inavyotaka. Kazi kubwa ipo katikakusuluhisha makundi ya Zanzibar kwa suala hili. Uhasama unaoonyeshwa hadi sasa unatia wasiwasi, kama marekebisho hayatafanywa, Katiba inayopendekezwa itabaki ni Katiba ya Tanganyika; Zanzibar itabaki ni nchi yenye mamlaka na madaraka makubwa na Tanganyika ndiyo itakuwa Muungano.”
CHANZO NIPASHE
Hakuna maoni
Chapisha Maoni