Mkurugenzi Bodi ya Utalii nchini avuliwa madaraka
Dar es Salaam. Serikali imemvua wadhifa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii nchini (TTB), Dk Aloyce Nzuki kutokana na utendaji usioridhisha.
Akitangaza uamuzi huo jana mbele ya waandishi wa habari, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema kuwa ameridhia uamuzi wa bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo ambao walipendekeza mkurugenzi huyo aondolewe.
Katika barua waliyomwandikia Waziri
ikiwa imesainiwa na Mwenyekiti wa Bodi, Charles Sanga na kuridhiwa na
wajumbe wote, walidai Nzuki alishindwa kuutangaza utalii ambalo ndilo
jukumu la bodi hiyo.
"Nilipata barua kutoka TTB ikinishauri
kumwondoa Bwana Nzuki na baada ya kushauriana na naibu wangu na katibu
mkuu nikaona ni vyema kukubaliana na ushauri wa bodi," alisema Nyalandu
jana, huku akiwa na naibu wake, Mahamoud Mgimwa na wajumbe wa Bodi ya
TTB.
Nyalandu alisema Dk Nzuki atapangiwa kazi nyingine ndani ya wizara hiyo .
Aliwaomba Watanzania wenye uwezo
kuomba nafasi hiyo hata wale walio nje ya nchi ili kuweza kusaidia
kukuza utalii wa nchi, uwe mbele ya mataifa mengine duniani.
"Nategemea katika siku 21 nafasi hiyo
iwe imezibwa, kwani nimewashauri watumie kampuni inayoheshimika ili
kufanya mchakato huo ," alisema.
Aliongeza kuwa baada ya mchujo
kufanyika, bodi hiyo itampa majina ya watu watatu ambayo baadaye
atayapeleka kwa Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya moja kuteuliwa kujaza
nafasi hiyo.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni