polisi feki anayedaiwa kuiba banki ya habibu apatikana,
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo,
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleimani
Kova, alisema hadi sasa watuhumiwa waliokwisha kamatwa katika tukio
hilo ni 10 ambao tayari majina yao yalishatolewa mapema katikla vyombo
vya habari.
Alisema hata hivyo katika upelelezi wa
kina imegundulika kwamba kompyuta ya marehemu inamilikiwa isivyo halali
na mtuhumiwa Maiga (Chief) na Polisi wanaendea kufanya jitihada kubwa
kwa lengo la kuipata “laptop” hiyo pamoja na simu moja ya marehemu.
“ Sasa imegundulika kuwa mtuhumiwa huyo
ndiye anayeimiliki laptop hiyo isivyo halali na Kuna dalili kuwa
mtuhumiwa amegundua kwamba anatafutwa hivyo anakwepa kukamatwa na
anajificha maeneo tofauti tofauti ya jiji ikiwa ni pamoja na kusafiri
sehemu mbalimbali hapa nchini kukwepa mkono wa sheria.
“Laptop hiyo ni muhimu sana katika
kukamilisha upelelezi wa shauri la kesi iliyopo mahakamani na katika
taratibu za kipolisi mtuhumiwa wa aina hiyo anatakiwa kutafutwa kwa
mujibu wa PGO No 238.
“Chini ya kifungu No: 238 kifungu kidogo
cha 5(a) cha sheria na taratibu za Polisi katika suala la upelelezi la
watu wanaotafutwa (Wanted Persons), sasa hivi mtu huyo ameingia katika
sifa ya watu wanaotafutwa bila kificho ambapo sheria hiyo pia inatumika
Kimataifa.
“Picha ya mtuhumiwa huyo itaoneshwa
katika vyombo vya habari ili mtu yoyote atakayemwona na kumtambua
ajulishe Jeshi la Polisi kwa madhumini ya kumkamata na kupata laptop
hiyo muhimu.
“ Pamoja na hayo mtuhumiwa mwenyewe ni
busara zaidi angejisalimisha kwani sasa kasi ya kumkamata mtuhumiwa
itaongezeka na itakuwa inamhusu kila raia mwema wa Tanzania au nje ya
nchi kutokana na urahisi uliopo kupitia mitandao ya habari.
“Jeshi la Polisi linawaomba raia wema
wasisite kutoa taarifa zitakazosaidia kumkamata mtuhumiwa huyo kwani
tukio la kuuawa kwa Dr. Sengondo Mvungi limeleta huzuni kubwa kwa
wapenda amani na watanzania wote kwa jumla,,”alisema Kova.
Dk Mvungi ambaye alikuwa mjumbe wa tume
ya mabadiliko ya katiba alivamiwa Novemba 3 mwaka huu nyumbani kwake
Kibamba nje kidogo na Jiji la Dar es Salaam na alifariki dunia Novemba
12 mwaka huu Katika Hospitali ya Milpark iliyopo Johannesburg, Afrika
ya Kusini baada ya kuhamishwa kutoka Kitengo cha Mifupa(MOI) cha
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Wakati huo huo,Jeshi la Polisi
limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili wanaojihusisha na utekaji wa
magari pamoja na ujambazi akiwamo Sadick Mohamed(50) mkazi wa Kigogo
aliyekuwa askari wa kituo cha Polisi Oysterbay ambaye aliachishwa kazi
mwaka 2003 kwa makosa ya kihalifu.
Kova alisema watuhumiwa hao walikamatwa
jana asubuhi katika eneo la round about ya Mivinjeni ambapo walikuwa
wakitaka kuliteka gari la sigara lenye namba T 399 BRF aina ya Canter
mali ya Kiwanda kinachotengeneza sigara aina ya Club.
Alisema gari hilo lilikuwa likipeleka
mzigo wa sigara bandarini kwa ajili ya kusafirishwa kuelekea Zanzibar
kwa ajili ya kupelekwa sokoni.
Alisema katika tukio hilo walikuwa
watuhumiwa wanne ambapo wawili walikimbia baada ya kuona wamezungukwa na
askari na kufanikiwa kumkamata Haji Abas(30)mkazi wa Kinondoni B pamoja
na Sadick ambaye alikuwa amevaa sare za Polisi.
“Alisema watuhumiwa hao walikutwa na
kamba ambayo hutumia kumfunga dereva pindi wanapotaka kuiba gari au
kufanya uhalifu wao, na uchunguzi uliofanyika tumebaini kuwa amehusika
katika matukio mbalimbali yaliyojitokeza hivi karibuni katika Benk ya
Habibu na I&M Bank.
“Kutokana na ugumu wa usafiri
unaowakabili wananchi wa Dar es Salaam watuhumiwa hao hutumia mwanya huo
kuwalaghai abiria kwa kushusha kiwango cha nauli wakidai kuwa
wanawapeleka katika maeneo yao na kisha kuwaibia vitu vyao hususani
pochi za kina mama pamoja simu zao.
“Wahalifu hao tumewakamata wakitumia
gari aina ya Serena Nissan ambayo ina muundo unaofanana na Noah yenye
namba T 335 CLP ambalo wamekuwa wakitumia kufanyia uhalifu huo,”alisema
Kova.
Kova alitoa onyo kwa askari ambao
wameachishwa kazi kwa makosa mbalimbali kutojihusisha na vitendo vya
kihalifu wakiwa wamevaa sare za polisi vinginevyo watachukuliwa hatua
kali kwa mujibu wa sheria pindi watakapo kamatwa.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni