NI ZAMU YA HECHE KUFIKISHWA MAHAKAMANI: MWAIPOPO
Na Mwandishi Wetu.Dar es salaam
Sheikh Said Mwaipopo amesema kuwa sasa ni zamu ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, kufikishwa mahakamani kufuatia kauli alizokuwa akizitoa kuwa watazuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mwaipopo ametoa matamshi hayo leo Novemba 7,2026 Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, huku akizitaka mamlaka zinazohusika kumfikisha Heche mahakamani mara moja.
Amesema endapo mamlaka hizo zitashindwa kufanya hivyo, yeye amejipanga kushirikiana na wanasheria binafsi kufungua kesi dhidi yake.
Mwaipopo amesema anashangazwa na watu wanaohoji mabadiliko ya mashtaka yaliyomkabili kiongozi wa CHADEMA, Tundu Lissu, kufuatia kufutiwa kesi ya uhaini na kuhukumiwa kifungo cha miaka minne jela kwa kosa la uchochezi Novemba 6, 2026.
"Awali kulikuwa na maelezo mazito kuhusu mashtaka yaliyokuwa yakimkabili Lissu, hata Heche mwenyewe alikuwa amewahi kutoa kauli akieleza kuwa uchaguzi hautafanyika.Ushahidi wa klipu ninao, hivyo aache kiburi ajiandae kuning'inizwa mahakamani," amesema Sheikh Mwaipopo.
Ameendelea kufafanua kuwa Serikali ndiyo yenye jukumu la kuandaa uchaguzi na kusimamia vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwamo Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Magereza, hivyo ni lazima vyombo hivyo vilinde zoezi la uchaguzi.
Sheikh Mwaipopo amesisitiza kuwa maslahi ya nchi yanapaswa kupewa kipaumbele kuliko maslahi ya vyama vya siasa au watu binafsi, akieleza kuwa nchi ni muhimu zaidi kuliko tofauti za kisiasa.
Kuhusu suala la kufungwa kwa watu kutokana na misimamo yao ya kisiasa, amesema kifungo si suluhisho la kudumu la changamoto za kisiasa, kwa kuwa maisha yanaendelea hata baada ya baadhi ya watu kufungwa.
Amesema hakuna mtu anayependa kwenda gerezani, hivyo ni muhimu masuala yanayohusu siasa, haki na sheria kuangaliwa kwa busara ili kuepusha migogoro na madhara yanayoweza kujitokeza.
Ameongeza kuwa changamoto hizo zinapaswa kushughulikiwa kwa kuzingatia sheria na misingi ya haki, huku akisisitiza umuhimu wa kutanguliza maslahi ya taifa.

No comments
Post a Comment