MRADI WA WLER KUTOKA TGNP UMEKUWA MKOMBOZI KWA KATA YA PANGANI HALMASHAURI YA KIBAHA
Vitendo vya ukatili wa kijinsia vimepungua kwa asilimia kubwa na jamii ya watu wa Pangani imekuwa salama kutokana na uwepo wa Kituo cha Taarifa na Maarifa kilichoanzishwa na TGNP kwa kushirikiana na UN Women na LGTI kupitia mradi wa WLER (Women’s Leadership and Economic Rights)
Akiongea na waandishi wa habari mapema Oktoba 23, 2025 Katibu Msaidizi wa Kituo cha taarifa na Maarifa kata ya Pangani Ndg. Malaki Lwakebuka amesema kuwa kabla ya kuanzishwa kwa kituo hicho vitendo vya ukatili wa kijinsia vilikithiri katika eneo hilo hususani kwa Wanawake na Watoto.
Ameongeza kuwa miongoni mwa ukatili ulikuwa ni mfumo dume ambao umekuwa ukuwanyima wanawake haki ya kushiriki katika shughuli za kiuchumi na za uongozi.
“Kabla ya kuja kwa Kituo cha Taarifa na Maarifa wanawake walikua wakibaguliwa kwenye kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kuonekana kama ni watu dhaifu wasioweza kuongoza, ila sisi kama KC tulipambana na hayo yote mpaka sasa wanawake wameweza kupata nafasi ya kuongoza ngazi za Vijiji, vitongoji na kwenye mitaa” alisema Malaki
Aidha kwenye vipaumbele amesema wao kama KC walihamasisha kwenye mikutano ya mitaa na kuweza kupata Shule, Zahanati pamoja na kuongezewa walimu katika shule ya msingi Kidimu ambayo ilikuwa na Walimu 9 lakini baada ya mapambano waliongezewa walimu 17 na kufanya jumla ya walimu kuwa 26.
Naye Afisa Maendeleo wa kata ya Pangani Rose Ngalai amesema kuwa anawashukuru TGNP kwa mafunzo hayo kwani yamemuongezea ufanisi yeye na viongozi wenzake katika maeneo yao ya kazi, kwani hapo mwanzo viongozi walipanga vipaumbele wenyewe bila kushirikisha wananchi lakini, sasa wanashirikiana na wananchi kuibua vipaumbele vyao.
Lakini pia ameongeza kwa kusema kuanzishwa kwa Kituo cha Taarifa na Maarifa katika kata hiyo kumeleta manufaa makubwa kwa kuwa wana KC wamekuwa wakiwasaidia kutoa elimu kwa wanajamii kuhusiana na masuala ya ukatili wa kijinsia uwezeshaji kiuchumi.
Aidha ameongeza kwa kusema KC imesaidia kupatikana kwa Shule ya Sekondari Vikawe ambayo serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 750, pamoja na shule ya msingi Miwale ambayo imetengewa shilingi milioni 280, lengo likiwa ni kuwakomboa wanafunzi kutokana na kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Amemaliza kwa kusema KC imesaidia kupatikana kwa mdau aliyechimba visima vitatu kwenye shule mbalimbali za kata hiyo ili kuwasaidia wanafunzi kupata maji kwa ajili ya matumizi ya shuleni, na pia kusaidia watoto wa kike waweze kujistili wanapokuwa kwenye siku zao.








No comments
Post a Comment