Zinazobamba

Doyo: Reli ya SGR na Meli za Kisasa Zitaunganisha Kigoma na Afrika Mashariki, Aahidi Kuimarisha Uvuvi Ziwa Tanganyika


Kigoma.

Mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, akiwa kwenye ziara ya kampeni mkoani Kigoma, ameahidi kujenga meli kubwa ya kisasa ya uvuvi itakayowezesha shughuli za uvuvi ndani ya Ziwa Tanganyika, hususan kwa wakazi wa Kigoma.

Mhe. Doyo amesema meli hiyo itakuwa kichocheo cha ajira kwa vijana zaidi ya 400 ambao watahusishwa moja kwa moja katika shughuli za uvuvi na biashara ya uuzaji wa samaki.

 Akizungumza mapema leo na wakazi wa Mwandiga, Ujiji na kata ya Buzebazeba, Doyo alieleza kuwa meli hiyo pia itawawezesha wananchi wa Kigoma kuuza samaki katika nchi jirani, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

“Kwa asilimia 80, uvuvi ni uti wa mgongo wa uchumi wa watu wa Kigoma. Nitahakikisha tunanunua vifaa vya kisasa vya uvuvi kwa ajili ya vijana wetu, ili wajikwamue kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa,” alisema Doyo.

Aidha, mgombea huyo wa urais aliahidi kuwa, iwapo atachaguliwa kuwa rais, atanunua meli mbili kubwa za kisasa, moja ya mizigo na nyingine ya abiria, kwa safari za kwenda Congo. 

Alisisitiza kuwa Kigoma ina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha biashara Ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na jiografia yake ya kipekee inayopakana na nchi kadhaa. 

Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza muingiliano wa kiuchumi na biashara kati ya Kigoma na nchi jirani.

Mhe. Doyo pia alisisitiza mpango wa kuharakisha utekelezaji wa reli ya kisasa ya SGR kuelekea Rwanda na Burundi, jambo litakalosukuma maendeleo ya biashara na kuongeza fursa za kiuchumi kwa Watanzania.

Kwa upande wa ubunge, mgombea ubunge wa NLD Kigoma Mjini, Bi. Apsa Musa Ramadhani, aliwahakikishia wananchi kuwa endapo atachaguliwa atasimamia kwa karibu mikopo ya halmashauri ili iwafikie walengwa bila upendeleo.

“Mikopo hii imelenga Watanzania wote bila kujali dini, kabila au chama. Lakini kwa sasa mikopo inatolewa kwa upendeleo, jambo ambalo si sahihi. Nitahakikisha kina mama, vijana na walemavu wa Kigoma wanapata haki yao ili kujiletea maendeleo,” alisema Bi. Apsa.

Kampeni za mgombea urais huyo, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa NLD, zinaelekea mkoani Tabora, ambako ataendelea kunadi sera za chama chake kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 29 Oktoba mwaka huu.

No comments