MGOMBEA URAIS AAFP ATEMBELEA WAFANYABIASHARA SOKO KUU LA SONGEA.
*Wafanyabiashara wampokea kwa shangwe kubwa.
*Wamueleza kero mbalimbali zinazowakabili,aahidi kuzitatua.
*Wamhakikishia kura za ndio Oktoba 29 mwaka huu.
Na Mussa Augustine.Ruvuma
Wafanyabiashara wa soko kuu la Songea Mkoani Ruvuma wamesema kuwa wanachangamoto kubwa ya kukosa soko la uhakika katika mazao ya biashara wanayozalisha ikiwemo Mahindi.
Wafanyabiashara biashara hao wametoa malalamiko hayo leo Septemba 30,2025 kwa nyakati tofauti sokoni hapo mara baada ya mgombea urais kupitia Chama Cha Wakulima (AAFP)Kunje Ngombale Mwiru kuwatembelea sokoni hapo na kuzungumza nao kabla ya kufanya mkutano wake wa kampeni uliyofanyika kwenye viwanja vya Soko kuu la Songea.
"Nimekuja kuwatembelea wakulima wenzangu,ambao wanauza mazao yanayotokana na kilimo,kwahiyo nimeona sio vizuri nikafanya mkutano bila kuwasalimia wakulima wenzangu,na mimi nitakua mtetezi wenu, tarehe 29 mkinichagua pale basi mtatemba kifua mbele"amesema Mwiru mbele ya wafanyabiashara hao.
Mmoja wa wafanyabiashara hao aliyefahamika kwa jina la Muhibu Hamisi Makilanga maarufu kama "Gogo" amemwambia Mgombea huyo kuwa bei ya mazao ya biashara imekua chini hali ambayo inawakatisha tamaa kuendelea na shughuli za kilimo.
"Kwasababu umeingia kwenye suala la kutetea wakulima tunaomba iwe hivyo hivyo,bei ya mazao iende vizuri,saivi tunataabika sana bei ya mahindi,viongozi wengi wamekuja hapa lakini hakuna hata mmoja aliyesema kuhusu masuala ya kilimo"amesema gogo.
Nae Vido Kalulu mfanyabiashara wa nyama amefurahishwa na hatua ya mgombea huyo kuwatembela wafanyabiashara hao kwa ajili ya kusikiliza kero zao,nakuongeza kuwa wamekua wakipata changamoto mbalimbali lakini wanakosa sehemu ya kuzisemea kutokana na serikali iliyopo kushindwa kuwasidia.
"Tunafurahi kuona rais wetu sisi Wakulima na wafugaji,tulikua na changamoto zetu, lakini hatuna sehemu ya kuzisemea,sisi wafanyabiashara wa nyama tunashukuru sana umekuja manake tulikua hatujui kama tuna rais wetu,tulikua tunaburuzwa lakini tunashindwa wapi tukimbilie,kumbe tunasehemu ya kukimbilia,"amesema Kalulu
Vilevile mfanyabiashara Yusta Nditi amemshukuru Mgombea huyo kwa kuwatembelea nakusema kuwa wamekua wakishindwa kwenda kulima kutokana na mazao wanayozalisha wakipeleka kuuza wanakopwa na malipo yanachelewa kutoka hali inayochangia kushuka kibiashara.
"Ahsante sana rais wetu mtarajiwa kututembelea sisi wakulima,tunalima lakini sisi wakulima tuna kero,mfano mimi ni mkulima lakini nashindwa kwenda kulima kwasababu mpaka sasa kuna mazao tumelima tukapeleka Serikalini tangu mwezi wa nane hadi leo hatujalipwa pesa,na mimi ni mfanyabiashara nategemea nitoe hela kwenye biashara nipeleke shambani halafu nirudishe kwenye biashara lakini kimya mpaka leo,mheshimiwa unatusaidiaje kwa hilo?amehoji Yusta
Akizungumzia malalamiko hayo Mgombea urais huyo amesema kuwa endapo Wananchi watampa ridhaa ya kuwa rais wa JMT atahakikisha anaimarisha masoko ya mazao ya biashara pamoja na kuvifuta vyama vyote vya ushirika (AMCOS) kwani vimekua chanzo cha kuwanyonya wakulima hao.
"Kwanza niwapeni pole sana wana Songea,manake mikutano yangu yote kama mnaifuatilia, kwasababu kuna watu wanawanyonya wakulima wangu kuna chama cha ushirika kinaitwa AMCOS kuna watu wanatoa stakabadhi ghalani nimewambia tarehe 29 mwaka huu mkinichagua vyama hivi vyote navifuta, kwahiyo nikiwa rais nyinyi mtegemee hela zenu mtapata kwa wakati."amesema Mwiru
Nakuongeza kuwa,"Ndio maana nimesema wapo mafisadi huku chini na nime waambia siwezi kukimbilia lkulu nitakaa hadi lijengwe bwawa la mamba Ikulu kwa ajili ya kuwapa adhabu waliokutesa wewe hapo(Yusta Nditi ambaye mfanyabiashara)amesema Mwiru.
Aidha baada ya kuwatembelea wafanyabiashara hao Mgombea huyo kwenye mkutano wa kuhitimisha kampeni Mkoani Ruvuma amewaahidi wananchi wa Mkoa huo kuwa atawatatulia changamoto zote zinazowakabili katika huduma za kijamii pamoja na masuala ya kiuchumi ikiwemo Maji,Umeme,Kilimo,Afya,Elimu, Miundombinu ya Barabara,Madini ,Utalii,pamoja na Masoko ya biashara.
No comments
Post a Comment