NCHI 15 UKANDA WA AFRIKA ZAJADILI MABORESHO YA MIKATABA YA NYUKLIA

Na Mwandishi Wetu.
Nchi 15 kutoka Ukanda wa Afrika zimekutana jijini Dar es Salaam katika mkutano muhimu wa kujadili maboresho ya mikataba ya nyuklia, ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya nyuklia kwa usalama na manufaa ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, alisema mkutano huo umeandaliwa kwa kushirikiana na Wakala wa Nguvu za Nyuklia duniani kwa lengo la kulinda vyanzo vya nyuklia na kuhakikisha matumizi yake hayaleti madhara kwa binadamu na mazingira.
“Leo tumekutana kwa ajili ya maboresho ya mkataba wa nyuklia ili kila nchi iweze kutekeleza miradi yake kwa kuzingatia usalama.
Huu ni mkutano wa kimataifa unaolenga hatua ya kwanza ya kuhakikisha vyanzo vya nyuklia vinatumika kwa manufaa pasipo madhara,” alisema Prof. Mushi.
Ameongeza kuwa yapo masharti yanayotakiwa kuzingatiwa na nchi zote wanachama, huku akisisitiza kuwa ni lazima teknolojia hiyo iwanufaishe wananchi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomic Tanzania, Profesa Najat Kassim Mohamed, alisema mikakati mbalimbali imeandaliwa kimataifa kuhakikisha matumizi salama ya nguvu za nyuklia, ambapo utekelezaji wake unaweza kuchukua kati ya miaka saba hadi kumi.
“Tanzania ina vyanzo mbalimbali vya nyuklia ambavyo vinaweza kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi. Kupitia mkutano huu, tunaweka mikakati ya pamoja na kuhamasisha nchi wanachama kusaini mikataba husika,” amesema Profesa Najat.
Ameongeza kuwa Tanzania ni nchi ya kimkakati kwa mataifa mengine yasiyo na bandari, hivyo inatumika kama njia ya kupitishia vifaa au malighafi za nyuklia kwa mujibu wa taratibu za kimataifa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Nguvu za Atomic Tanzania, John Simba Chaka, alisema moja ya malengo ya mkutano huo ni kubadilishana uzoefu kuhusu taratibu za usafirishaji wa madini ya nyuklia ambayo hutumika katika maeneo mbalimbali duniani.
Mkutano huu unaonesha dhamira ya pamoja ya nchi za Afrika kulinda na kutumia kwa usahihi rasilimali za nyuklia kwa maendeleo ya kisayansi, kijamii na kiuchumi.
No comments
Post a Comment