Zinazobamba

DC MPOGOLO AVUNJA BARAZA LA MADIWANI ILALA AWAHAKIKISHIA WANACHI WA JIJI LA DAR ES SALAAM KUKAMILIKA KWA MIRADI YA MAENDELEO

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo, amewatoa wasiwasi wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuwahakikishia kuwa miradi ya maendeleo inayokaribia kukamilika itatekelezwa kwa wakati kama ilivyopangwa.

Ametoa kauli hiyo leo Juni 20, 2025 wakati wa uvunjaji rasmi wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, lililokuwa likihusisha madiwani 36 pamoja na madiwani wa viti maalumu 13.

Katika hotuba yake, DC Mpogolo amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam chini ya Mkurugenzi Mabelya ina watendaji makini, wenye maono na wanaotekeleza majukumu yao kwa weledi na uwajibikaji mkubwa katika kusimamia maendeleo ya wananchi.

 "Tuna imani kubwa na uongozi wa Mkurugenzi Mabelya pamoja na timu yake ya wataalamu. Wanajituma, wanafanya kazi kwa uaminifu na wamejipanga kuhakikisha miradi yote inaisha kwa ubora unaostahili," amesisitiza DC Mpogolo.

Sambamba na hilo, Mheshimiwa Mpogolo amempongeza Mstahiki Meya wa Jiji hilo, Omary Kumbilamoto, pamoja na Baraza la Madiwani kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo na ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri, kwani wao ndio sababu ya mafanikio yanayoonekana leo, na wananchi wanafurahia miradi hiyo inayogusa maisha yao moja kwa moja.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji hilo Elihuruma Mabelya, ametoa salamu za pongezi na shukrani kwa Madiwani wote kwa kazi kubwa na mchango wao katika kuleta maendeleo ya Jiji hilo katika kipindi chao cha uongozi.

Amesema kuwa kipindi cha uongozi wa Baraza hilo kimeacha msingi imara wa maendeleo, na kwamba Halmashauri itaendelea kusimamia kwa dhati utekelezaji wa maazimio yote yaliyopitishwa na Baraza hilo.

Amesisitiza kuwa Halmashauri itaendelea kusimamia miradi yote ya maendeleo kwa uwazi na kwa kushirikisha jamii, huku akiwasihi Madiwani waliomaliza muda wao kuendelea kuwa sehemu ya harakati za maendeleo katika kata zao kama wazalendo na mabalozi wa mabadiliko.

“Tutaendeleza kazi na misingi mema mliyoiacha kwa maslahi ya wananchi. Baraza limevunjwa, lakini dhamira ya kuwatumikia wananchi haijawahi kuvunjwa. Tunawaaga kwa heshima, tukijivunia kazi yenu, na tukiahidi kuendeleza misingi hiyo kwa uaminifu,” amesema Mkurugenzi Mabelya.

Naye, Mstahiki Meya, Omary Kumbilamoto, amewashukuru Mkuu wa Wilaya ya Ilala pamoja na watendaji wote wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa ushirikiano alioupata katika kipindi chote cha uongozi wake. 

Amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya mshikamano, maono ya pamoja, na juhudi za pamoja kati ya Baraza la Madiwani na watendaji wa Halmashauri.

Hatua ya kuvunjwa kwa Baraza hilo la Madiwani inatekeleza agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, aliyeagiza Halmashauri zote nchini kuvunja mabaraza ya madiwani ifikapo Juni 20, 2025, kufuatia kumalizika kwa muda wa kisheria wa uongozi wa Serikali za Mitaa.

No comments