SERIKALI YA DKT.SAMIA ITAENDELEA KUWEKEZA MAENDELEO MKOANI PWANI:MSIGWA
Msemaji Mkuu wa Serikali Greyson Msigwa akiongea na Waandishi wa habari( hawapo pichani,) kuhusu uwekezaji Mkubwa wa Viwanda Mkoani PWANI
Na Mussa Augustine,
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya viwanda kwa kuwekeza zaidi ya shilingi trilioni 12.4 katika mkoa wa Pwani, huku Kongani ya Viwanda ya Kwala ikitajwa kuwa kitovu cha mapinduzi ya viwanda nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Bandari Kavu ya Kwala, Msemaji wa Serikali amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia, serikali imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 25.75 kwenye viwanda, na miradi 2,099 imeanzishwa, ikitarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira laki tano kwa Watanzania.
Kati ya miradi hiyo, 1,982 ni mipya, huku miradi ya ubia ikiwa 476, miradi ya Watanzania 719, na mingine ikiwa ya wawekezaji wa kigeni pekee. Ameeleza kuwa asilimia 95 ya miradi hiyo imekamilika na inatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya laki moja.
Serikali imewekeza shilingi bilioni 882 katika Kongani ya Viwanda ya Kwala, eneo lenye hekari 2,500 lililotengwa kwa ajili ya viwanda vikubwa. Kongani hiyo imekamilika kwa asilimia 82, huku miundombinu muhimu ikiwa tayari imetengenezwa.
Miongoni mwa miundombinu hiyo ni pamoja na Barabara za zege zenye uwezo wa kubeba mizigo mizito, Mtandao wa maji na umeme, ambapo megawati 50 za umeme tayari zimefungwa, na lengo ni kufikisha hadi megawati 100,Majengo ya malazi na makazi ya wafanyakazi,Majengo ya kudhibiti moto kwa usalama wa viwanda.
Kwa sasa, waendeshaji 10 wa viwanda tayari wameanza shughuli zao katika kongani hiyo.
Mkoa wa Pwani unashika nafasi ya pili nchini kwa kuvutia uwekezaji mkubwa wa viwanda, ambapo asilimia 67 ya uwekezaji wake katika miaka minne iliyopita umeelekezwa kwenye viwanda.
Kwa ujumla, viwanda vilivyoanzishwa vinatarajiwa kuzalisha bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 6, huku mapato ya kodi kutoka viwanda hivyo yakikadiriwa kufikia trilioni 1.2 kwa mwaka.
Serikali imewataka Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika miradi hii ya kimkakati, hususan katika uanzishaji wa viwanda, biashara na huduma zinazohusiana na ukuaji wa sekta ya viwanda.
Kwa kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu na mazingira bora ya biashara, Tanzania inazidi kupiga hatua kuelekea uchumi wa viwanda na kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa kwa soko la Afrika Mashariki na kwingineko
Post Comment
Hakuna maoni
Chapisha Maoni