Zinazobamba

IFIKAPO MWAKA 2030 WATU MILIONI 300 AFRIKA WATATUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA--BITEKO


NA MWANDISHI WETU

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amesema ifikapo mwaka 2030 watu milioni 300 katika Bara la Afrika watakuwa wanatumia Nishati Safi ya kupikia huku Tanzania ikiwa ni kinara katika kuhamasisha Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia.


Amesema  juhudi zinazofanyika katika kufikia lengo hilo zimepelekea  Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Dunia ( WB) kuunga mkono Ajenda ya Nishati Safi ya kupikia katika bara la Afrika.


Biteko amesema hayo wakati akizungumza katika Mkutano wa Jukwaa la Majadiliano kuhusu Masuala ya Nishati  kwa Bara la Afrika kwa ngazi ya Mawaziri unaofanyika Jijini Dar es salaam kwa siku mbili ulioandaliwa  na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na AfDB.


Amesema AfDB imeichangua Tanzania kufanya mkutano huo wa majadiliano kwa kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kimaendeleo na mafanikio katika Sekta ya Nishati ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika zinazoshirikiana na benki hiyo na imekuwa mfano wa kuigwa na nchi hizo..


Ameeleza kuwa,  katika mkutano huo masuala mbalimbali yanajadiliwa huku lengo kubwa  likiwa ni kuweka mipango thabiti ya kuhakikisha kuwa watu Milioni 300 katika Bara la Afrika wanatumia nishati safi ya kupikia  ifikapo 2030 ikiwa ni miaka 6 kutoka sasa.


" Mkutano huu pia ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa Marais  wa nchi za Afrika unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025 ikiwa ni mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye kinara wa ajenda ya Nishati safi ya kupikia Afrika." Amesema Dkt. Biteko


Amesema Marais hao watakuja nchini kujadili masuala ya nishati katika Bara la Afrika ikiwemo suala la  watu milioni 300 Afrika kutumia nishati safi ya kupikia. 


Ameongeza kuwa, mkutano huo utafanya tafakuri na utaweka mikakati ya kuhakikisha kuwa nishati safi ya kupikia inapatikana kwa uhakika na gharama nafuu ili kila mwananchi anaweza kuimudu.


Amesema mkutano huo ni muhimu kwa Tanzania  hasa kwenye sekta ya nishati kwakuwa imefanya mapinduzi makubwa kwenye nishati  na upatikanaji wa umeme nchini ni wa uhakika na miradi mikubwa inayotekelezwa ipo mwishoni na kwamba kazi kubwa iliyopo ni kuhakikisha watu wanapata umeme kila sehemu.


“Furaha yetu ni kwamba tumepata heshima kubwa ambayo haikuja hivihivi bali ni kutokana na mahusiano mazuri ya kidiplomasia kati nchi yetu, Benki ya Maendeleo ya Afrika ( AfDB) na Benki ya Dunia na kutokana pia na kupiga hatua katika masuala ya usimamizi mzuri wa kisera, uzalishaji, usafirishaji, usambazaji na upelekaji wa umeme vijijini."  Amesema Dkt. Biteko.


Amesema Tanzania imepiga hatua katika kupeleka umeme vijijini na ifikapo Desemba tutakuwa tumepeleka umeme katika vijiji vyote zaidi ya 12,000 na kuhamia katika vitongoji vyote.


Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Kelvin Kairuki amesema Benki hiyo kwa kushirikiana na Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kufanya kazi pamoja kwa sababu Tanzania iko katika mstari wa mbele katika kutekeleza Ajenda ya Nishati safi ya Kupikia ikilinganishwa na nchi nyingine zinazofanya kazi na benki hizo.


Amesema  uamuzi wa kuamua  mkutano mkubwa wa Marais ufanyike Tanzania ni pamoja na  kumuunga mkono  Rais Samia katika juhudi za utekelezaji wa Ajenda ya Nishati safi ya kupikia na kuwa kinara wa ajenda hiyo kwa nchi za Afrika.


Mkutano huo  umehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Kamishna wa Umeme na Nishari Jadidifu Mhandisi Inocent Luoga, Wakuu wa Taasisi zilizochini wa Wizara ya Nishati na wadau wa nishati kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.




Hakuna maoni