Zinazobamba

Je unajua nini kuhusu bidhaa zenye nembo ya halal?

 



Na Selemani Magali, Dar es Salam

Je unajua nini kuhusu bidhaa zenye nembo ya halal? Mkuu wa Kitengo cha Halal cha Baraza Kuu la Waislamu Tanzania, (Chief Halal), Mohammed Juma ambaye pia ni Imam Mkuu wa Msikiti wa Idrisa anakusaidia kuelewa suala hili muhimu kupitia mahojiano aliyofanyiwa na mwandishi wetu, Selemani Magali.

 

Swali: Nini faida ya huduma ya halal katika jamii na taifa kwa ujumla wake?

Halal Chief: Halal ina faida nyingi. Faida ya kwanza ni kuhakikisha watu wanatumia bidhaa zilizo halal, kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Lakini, kwa upande mwingine halal inasaidia kuhamasisha biashara ya kimataifa.  Nchi kama Austalia na Brazil ambayo ni ya Kikristo, wamelipa kipaumbele suala la halal na matokeo yake wanauza nyama nyingi katika nchi za Mashariki ya Kati, hususan Saudi Arabia, Abudhabi, Oman na India.

 

Ukilingansha umbali wa kuelekea Mashariki ya Kati kutokea Australia/Brazil na  kutokea Afrika Mashariki, unaona wazi kuwa Afrika ya Mashariki ipo karibu zaidi na Mashariki ya Kati. Sasa, kwa nini wenzetu wamelishika soko la nyama? Ni kwa sababu ya nyama zao zimethibitishwa na nembo ya halal kimataifa.

 

Hata kiubora, nyama kutoka ukanda wa Afrika Mashariki ni bora zaidi (more natural) kwa sababu wanyama wetu wanakula nyasi tu. Pia wanyama wa ukanda huu hawakabiliwi na maradhi mengi, na hivyo basi sisi tungepaswa tupate soko kubwa huko.

 

Swali: Ipoje hali ya ‘halal’ hapa nchini?

Halal Chief: Hali ni mbaya sana sababu watu wengi hawana ufahamu wa jambo hili na hivyo wengi wanakula na kunywa bila kuangalia uhalali wa wanachokula. Licha ya kwamba, watengenezaji bidhaa huandika taarifa kuhusu bidhaa husika, hakuna anayejali na kujitahidi kusoma ili kujua bidhaa husika imetengenezwa na nini.

 

Katika kutatua tatizo hilo, mwaka 2016 ilianzishwa taasisi ya Tanzania Halal Certification (THC) ili kufanya kazi ya kuthibitisha bidhaa wakishirikiana na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).  Taasisi hiyo iliyodumu kwa mwaka mmoja, ikafa. Baadae ilikuja taasisi nyingine iitwayo Tanzania Halal Certification (Tan HAC) ambayo nayo ilikufa. Ndipo mwaka 2019, taasisi nyingine ya Mico international Halal Bureau (MIHB) ilizaliwa kuhuisha huduma ya halal hapa Tanzania.

 

Swali: Kwa nini baadhi ya taaisi zilizoundwa hazikufikia malengo yaliyokusudiwa?

 

Chief Halal: Bahati nzuri nilikuwepo katika taasisi zote hizo kama kiongozi. Changamoto zilizokuwepo ni pamoja na viongozi kuingiliana majukumu ambapo unakuta chief halal kwa kutumia misingi ya dini anasema hili, lakini wenye taasisi wanasema vile. Hivyo, kulikosekana maamuzi yenye tija na afya kwa jamii na kwa sababu hiyo, mimi na  wenzangu tuliondoka na tukahamia huku ambako wanaheshimu misingi ya dini.

 

Changamoto nyingine ilikuwa ni maslahi. Huduma ya halal ina pande mbili, kiimani na biashara. Hatukupata ushirikiano mzuri kutoka kwa masheikh, hasa wa ngazi za wilaya na kata ambao walihoji watafaidika vipi na mpango huo? Ikumbukwe, machinjio yote yapo chini ya Bakwata na hivyo masheikh wa maeneo husika hupata kiasi cha mapato. Ujio wa halal haukubainisha maslahi hayo ya masheikh. Hili linaungana na changamoto ya ukosefu wa rasilimali fedha.

 

Swali: Vipi kuhusu changamoto kimataifa?

 

Kimataifa, changamoto ilikuwa ni ukosefu wa utambulisho wa Shirika la Kidunia linaloshughulikia mambo ya halal (JAKIMS). Mpaka sasa taifa halijapata kibali cha kutambuliwa na JAKIMS kwa hiyo hata tukiweka alama zetu za halal hazitambuliki nje ya mipaka ya Tanznaia.

 

Tukiweza kuwashawishi wenzetu wa JAKIMS kuitambua Tanzania, tutapata fursa ya kupeleka bidhaa zetu, hususan nyama, nje ya nchi. Kikwazo kikubwa cha kupata kibali hicho, tangu enzi za THC imekuwa ni ukosefu wa wataalamu waliopitia mafunzo ya JAKIMS. Taasisi hiyo inataka wataalamu watakaofanya kazi ya halal wawe wamefundishwa na watu wao.

 

Wenzetu Kenya walitumia muda mrefu sana kujenga halal lakini  walipiga hatua kubwa baada ya kujiunga na shirikisho la JAKIMS.  Sisi pia tumeanza michakato ya kujiunga na taasisi ya JAKIMS. Zoezi hili limefikia hatua nzuri na haitachukua muda mrefu watatupatia cheti. Ikumbukwe, JAKIMS ni shirika kubwa lenye nchi wanachama zaidi ya 46, zikiwemo za Kikristo na Kiislamu na pia kuna mashirika zaidi ya 60 yaliyosajiliwa – hivyo wana mtandao mkubwa.

 

Hapa juzi, serikali ilitoa miezi mitatu kwa wadau wa nyama kufuatilia kwa nini tunashindwa kuuza nyama nje, ilhali tuna nyama nyingi na tuna watu wa TBS na TFDA ambao wanathibitisha ubora. Mtaalamu kutoka soko la nyama Dodoma alisema, tatizo kubwa ni kutotambuliwa na JAKIMS, kwa hiyo tukipeleka nyama hazichukuliwi. JAKIMS wao wanasoko kubwa la nyama.

 

Waislamu na wasio Waislamu, ikiwemo wazungu, wanaliamini shirikisho hilo kwa sababu wana weledi zaidi zaidi ukilinganisha na mashirika mengine kiasi kwamba, hata kama mashirikisho mengine yamekagua, bado wao wanaweza kugundua tatizo. Kwa hiyo, kitu kikipitishwa na JAKIMS kinaaminika. Katika JAKIMS, wanaotoa cheti ya halal ni watu wengine, wanaokagua ni wengine, na kuna bodi inayofanya maamuzi na hivyo  basi suala la rushwa halina nafasi kabisa.

 

 

 

Swali: Inaonekana una matumaini sana na Mico. Mmejipangaje?

 

Halal inapaswa kuangaliwa kwa undani upana, kuanzia uzalishaji, usafirishaji na uuzaji. Wengi wanadhani suala hilo lipo kwenye kuchinja tu kumbe sio kweli bali linaanzia mbali.  Unaweza kuona watu wamechinja kama inavyotakiwa lakini nyama hiyo ikabaki kuwa ni haramu kwa sababu huenda chakula alicholishwa mnyama kilikuwa ni haramu. 

 

Wakaguzi wetu wa Mico Interanational Halal Bureau watafanya kazi kwa kuangalia mnyororo mzima wa halal: kuanzia chakula anachokula mnyama, hadi nyama inapouzwa kwa mlaji. Tukigundua kuna changamoto, hatuwezi kukupa nembo yetu ya halal.

 

Jambo hili ni zito na linalohitaji uungwaji mkono wa wadau mbalimbali. Kufikia malengo hayo, tumejipanga kuhakikisha tunapata uungwaji mkono  wa wadau na taasisi zingine. Kuna mipango inafanyiwa kazi, si muda mrefu watu watapata taarifa kuwa tupo na tumekuja kivingine.

 

 

Taasisi yetu pia inaamini katika nguvu ya elimu. Watu wakielewa dhana hii ya halal, kila kitu kinawezekana. Kwa hiyo,  ni muhimu ni kutoa elimu ya halal ili watu waelewe kuwa halal si kwenye kuchinja peke yake bali mnyororo mzima. 

 

Tumejipanga baada ya kutoa mafunzo hayo tuwape vyeti maalum wachinjaji hao ili kuwatambua (recognition). Pia, tutatambua machinjio na magari yao kwa kuyapa nembo maalum kuonyesha kuwa wanajua wanachokifanya. Pia, tunajipanga elimu kwa wauzaji, ambao ni wadau muhimu katika hili. Wakielewa, watakuwa msaada mkubwa wa kuwalisha jamii nyama ambayo haina shub’ha.

 

Jambo jingine ni kujenga hamasa miongoni mwa jamii sambamba na kushirikiana na wadau wote walio katika mnyororo wa halal. Tunaamini ukiwakamata wadau muhimu katika mnyororo wa usambazaji, mlaji atakula kilicho cha halal. Pia, ningeandaa takwimu za wadau waliopo katika sekta. Yote haya yatawezekana kama jamii itaelewa kuhusu kazi hii nzito.

 

Swali: Nchi nyingine duniani ambako wamefanikiwa, walifanyaje?

 

Chief Halal: Wenzetu huko duniani wamekuwa na uelewa mkubwa juu ya halal. Hawatumii vitu ambavyo havina nembo ya halal. Malaysia, kwa mfano, kuna idara maalumu ya serikali ndio inafanya kazi hii ya halal ikiingizia serikali mapato makubwa. Wafanyakazi wa idara hiyo wanalipwa vizuri …unaweza kufananisha na mishahara ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT). Halal ni jambo kubwa sana katika nchi za wenzetu.

 

Hapa Tanzania, tunapaswa kuangalia mifumo yetu ili kuifanya sekta hii ikue kwa haraka kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake.

 

Swali: Changamoto gani mnakumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yenu?

 

Chief Halal: Moja ya changamoto ni rushwa. Kwa mfano, kampuni moja ya chakula iliyopo Ubungo (jina tunalihifadhi) waliomba kupatiwa hati ya halal, lakini nilipoenda kukagua walikataa kunifungulia makontena mawili. Nilipouliza kwa nini, walisema zimefungwa na TFDA, lakini TFDA nao walikana. Walisema ingekuwa wao, kungekuwa na nembo (seal) za TFDA.

 

Niliandika taarifa yangu na suala hilo lilipofikishwa katika shura ya viongozi nao walilikataa. Hata hivyo, suala hilo lilipitishwa na wenye taasisi bila ya wengine kujua; nami ndipo nikaamua kuondoka. Siwezi kubeba dhima ya kulisha watu haramu kwa maamuzi yaliyofanywa na mtu ambaye hajui athari ya jambo lenyewe.

 

Pia, tuligundua kampuni moja ya kutengeneza soseji (jina tunalihifadhi) kwa kuchanganya na nyama ya nguruwe. Tuliandika taarifa yetu lakini hakukuwa na hatua zilizochukuliwa. Katibu Mkuu wa BAKWATA wa miaka hiyo aliahidi kuzungumza suala hilo kwenye Baraza la Idd lakini hakufanya hivyo, na sababu haikufahamika.

 

Soseji hizi zinatumika sehemu mbalimbali. Tulipowauliza wauzaji wakasema kwamba, watu wenyewe ndio wanataka bidhaa hiyo. Zipo soseji za aina mbili: za ng’ombe na za nguruwe, lakini jambo la ajabu ni kwamba, hata Waislamu wanaagiza zile zilizochanganywa na nguruwe.

 

Vilevile, tulishuhudia ugomvi mkubwa katika baadhi ya mikoa hadi kufikia watu kupigana kwa sababu ya kutembelewa na watu wa halal. Ukinzani huo ulionekana katika machinjio makubwa matano hapa nchini (The big five slaughter house in Tanzania): Dodoma, Rukwa, Mwanza, Singida na Tanga.

 

 

Swali: mmeanza safari ya kutoa huduma hii ya halal hapa Tanzania, mpango wenu ukoje kuhakikisha mnafanikiwa?

 

Halal chief: Kwanza, sisi wenyewe tumehakikisha tunatambua umuhimu wa halal. Baada ya hapo, tumeanza kuongeza ufahamu wa wadau juu ya umuhimu wa jambo hili, kwa kushirikiana na mamlaka na taasisi nyingine. Kisha mengine yataendelea.

 

Soko la halal ni pana na sisi tunataka tuwe kichocheo cha kutengeneza fursa za kuingiza fedha kwa wengine na kutengeneza ajira. Tunaamini halal ikisimama, hata nchi itafaidika.


 

 

 


Hakuna maoni