Zinazobamba

UCSAF yatekeleza miradi katika kata 829 kati ya kata 1,234 zilizo ainishwa na mfuko

 


Afisa mawasiliano wa mfuko wa UCSAF Bi. Celina Mwakabwale akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya sabasaba, jana




 

Mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) umetoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanalinda miundombinu ya mawasiliano hasa minara ambayo imekuwa ikijengwa karibu na kata zao.

Akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya 46 ya biashara ya kimataifa (sabasaba), Afisa mawasiliano wa mfuko huo Bi. Celina Mwakabwale alisema mawasiliano ni muhimu sana katika maisha ya mtu.

“Ukitaka kujua kuwa mawasiliano ni maisha, jaribu kuzima siku yako leo, hivyo ni vizuri watu wakatambua kuwa kuharibu miundombinu kunapelekea kukatika kwa mawasiliano,” alisema

“Kuna wakati watu wenye nia ovu wanafanya kazi ya kuhujumu miundombinu wakidhani kuwa haiwahusu, miradi ile inawahusu kwa sababu kuna sehemu ya kodi yao imetumika kujenga minara,” alisema

“Mawasiliano yanaokoa maisha, kuna wakati unaweza kuwa na mgonjwa nyumbani, kama hauna simu hutaweza kumsaidia kwa haraka mgonjwa,” aliongeza

Aidha akizungumzia ujio wao katika maonyesho ya sabasaba, Mtaalam huyo wa masuala ya mawasiliano alisema lengo lao ni kuhamasisha na kutoa elimu juu ya huduma wanazotoa.

Alisema Mfuko huo unafanya kazi kubwa ya kujenga minara katika maeneno ambayo hayana huduma na ipo lakini ni hafifu.

Aliongeza kusema mfuko wa Yuksaf umelenga kuleta mapinduzi katika sekta ya mawasiliano kwa umma, tunalenga Zaidi katika maeneno ya pembezoni.

Hapa tumekuja kutoa elimu kwa umma, lengo wafahamu sisi Yuksaf ni watu gani na tunafanya nini katika kazi zetu.

“Hapa tunapokea maoni mbalimbali kuhusu changamoto za mawasiliano katika maeneo wanapotoka, tuko tayari kwa ajili ya kuwahudumia, tunawashauri wananchi waje sabasaba kupata taarifa Zaidi juu ya kazi zinazofanywa na UCSAF, tunao wataalam wa ktosha ambao watawahudumia.

Akizungumzia kuhusu miradi, alisema wanayo miradi mingi ambayo inaendelea ikiwemo mradi wa kufikisha mawasiliano katika maeneno mbalimbali

“Miradi inayotekelezwa ni pamoja na huduma za mawasiliano ya simu, mfuko unafikisha huduma za mawasiliano ya simu katika maeneno yasiyo na huduma hiyo na yenye mawasiliano hafifu, mpaka kufikia April, 2022 mfuko umetekeleza miradi katika kata 829 kati ya kata 1,234 zilizoainishwa na mfuko,” alisema

Aidha kwenye kuboresha usikivu wa redio,Celina alisema kwa sasa mfuko unatekeleza mradi wa kuboresha usikivu wa redio ya taifa na redio ya kijamii katika baadhi ya maeneo ya nchi hasa mipakani.

Alisema wamekuwa wakiboresha usikivu wa redio hasa maeneno ambayo usikivu wake ni hafifu lakini pia wamekuwa wakijenga minara katika maeneno ambayo redio haijafika.

Mtaalam huyo alisema kwa kushirikiana na TBC, mfuko umeweza kukamilisha ujenzi wa studio za redo za jamii Dodoma na Arusha pamoja na vituo vya kurushia matangazo ya radio TBC Taifa na TBC FM.

Vituo hivyo vimejengwa kisaki na mrimba Mkoani Morogoro, Ngara Mkoani Kagera, Ruangwa Mkoani Lindi na Ludewa Mkoani Njombe.

Mbali na mafanikio hayo pia alisema mfuko umefanikiwa kujenga kituo cha miito ya dharura Zanzibar lengo ni kuiwezesha serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa na kituo cha kuratibu taarifa za matukio ya dharura.

Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na Moto, ajali, mlipukowa magonjwa mbalimbali, tayari kituo hicho kimeshakamilika na kuzinduliwa, wakazi wa Zanzibar wameanza kunufaika nacho kwa kupiga simu ya bure kupitia nambari 190.

Vilevile alisema Mfuko huo kupitia mradi wa kuunganisha shule kwenye intaneti, umekuwa ukizipatia shule za umma vifaa vya TEHAMA na kuziunganisha na mtandao wa intaneti kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kujifunza kupitia vifaa hivyo katika hatua za awali.

Mpaka sasa jumla ya shule 811 zimepatiwa vifaa ikiwemo Kompyuta na prita.

Alisema, pia upo mradi wa tiba Mtandao, ambao umelenga kuunganisha hospitali kadhaa na Hospiatali ya Taifa ya Muhimbi (MNH)na Taasisi ya Mifupa MOI ili kuboresha utoaji wa huduma za afya katika hospitali zote zilizounganishwa kwa kuwawezesha wananchi kupata huduma za madaktari

Kimsingi Mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) ulianzishwa na serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sheria ya Bunge nambari 11 ya mwaka 2006 sura ya 422 kwa lengo la kupeleka na kufanikisha huduma ya mawasiliano kwa wananchi waishio katika maeneno machache ya mijini na maeneno mengi ya vijijini ambayo hayana mvuto wa kibiashara kwa watoa huduma za mawasiliano.

Mwaka 2009 kanuni za kuhuisha Mfuko zilipitishwa na Mfuko kuanza kazi Julai 1, 2009.

Dhamira ya mfuko huu ni kuratibu upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini na maeneno ya mijini yenye mawasiliano hafifu kwa kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya mawasiliano, lengo ni kufikia maendeleo ya kiuchumi na kijamii sambamba na dira ya maendeleo ya Tanzania ifikapo 2025.

Dira ya mfuko huu ni kufanikisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano Tanznia kikamilifu na kwa usawa.

 

No comments