Zinazobamba

Samia mgeni rasmi miaka 25 ya Taasisi ya Anna Mkapa

 



Na Suleiman Magali

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kusheherekea miaka 25 ya Taasisi ya Equal Opportunities for all Trust fund (EOTF) inayotarajiwa kufanyika leo katika ukumbi wa Mwalim Nyerere, Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo ambayo inamilikiwa na mke wa Rais wa awamu ya tatu mama Anna Mkapa, Bw. Stephen Emanuel alisema wiki hiyo itakuwa na mambo mengi na kuwaomba wakazi wa jiji la Dar es salaam kushiriki pamoja katika hafla hiyo.

Alisema Rais Mwinyi anatarajiwa kutoa nasaha kwa wajasilia mali mbalimbali kuhusiana na fursa za kujiongezea kipato.

Bw. Stephen aliongeza kusema kuwa sherehe za miaka 25 ya EOTF itafanyika kwa wiki moja, kuanzia Juni 20, 2022 na kufikia kilele chake Juni 27, 2022 ambapo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufunga sherehe hizo kwenye ukumbi wa Mwl. Nyerere.

“Sherehe zitafanyika kwa wiki moja, Juni 20, ni siku ya ufunguzi na maonyesho ya bidhaa za wanawake wajasiliamali kutoka bara na visiwani, kwa hiyo Mh. Rais Mwinyi atatufanyia ufunguzi,” alisema Bw. Stephen.

Aliongeza kusema siku nne zitakazo fuata zitatolewa mada mbalimbali za ujasiliamali, elimu, maradhi,na elimu juu ya  upatikanaji wa mitaji.

Pia kutakuwa na elimu juu ya stadi za maonyesho ya biashara lakini pia watu watafaidika na elimu juu ya uunganishwaji wa masoko ya bidhaa za wanawake wajasiliamali katika masoko ya Afrika Mashariki.  

Aidha alifichua kuwa mada hizo zitatolewa katika ukumbi mpya wa JKT Mgulani kuanzia majira ya saa tatu asubuhi na yanatolewa bure kabisa.

Mbali na kutoa mafunzo pia kutakuwa na maonyesho mbalimbali ya bidhaa za wajasiliamali, amewataka wakazi wa Dar es Salaam kufika katika ukumbi huo ili kupata ujuzi.

Vilevile alisema Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika burudani ya mpira wa miguu utakao wakutanisha watani wa jadi Simba Queens na Yanga Princes, mchezo utakao chezwa juni 25, 2022 ambapo mshindi atakabidhiwa kombe kubwa la kifahari linaloweza kushindaniwa mwakani.

“Wiki yote inatawaliwa na matukio mengi, tunatarajia Juni 26,kuwa na chakula cha hisan kuichangia EOTF kuendelea na kazi zake, hafla hii ya chakula itafanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee uliopo Upanga Jijini Dar es Salaam,mgeni rasmi katika hafla hiyo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa

Aliongeza kusema kuwa siku ya kilele cha sherehe hizo itafanyika Juni, 27, 2022 ambapo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni Rasmi.

“Tutafunga sherehe zetu katika ukumbi wa Mwl. Nyerere, mgeni wetu atakuwa Rais wan chi, Mh Samia Suluhu Hassan, siku hiyo pia kutakuwepo maonyesho madogo ya bidhaa za wanawake wajasiliamali kutoka bara na visiwani,” alisema

Aliongeza kusema kuwa siku ya kufunga sherehe hizo wahisani ambao wameisaidia EOTF katika kila Nyanja toka mwaka 1997 watatambuliwa na kupewa tuzo. Pia Rais atapata fursa kusikia shuhuda za wanufaika wa mfuko huo

Ends,

 

 

No comments