Miaka 50 ya hospitali ya Bugando
Na. Paschal Dotto-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan,
amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za afya ili kuimarisha
utoaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza katika sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya kuanzishwa
kwa Hospitali ya Bugando zilizofanyika katika hospitali hiyo Jijini Mwanza,
Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali inaendelea kutoa ushirikiano
kupitia mambo mbalimbali ikiwemo utoaji fedha kwa ajili ya maendeleo ya
hospitali hiyo, lakini pia kulipa watumishi jambo ambalo limetekelezwa kwa muda
mrefu baada ya Serikali na hospitali hiyo kuingia makubaliano.
“Miaka 50 ya Bugando, Serikali imetoa ushirikiano mkubwa katika
kuendeleza na kuimarisha huduma za kibingwa ambazo kwa sasa zinatolewa na kuwa
msaada mkubwa kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa katika mikao minane yenye wananchi
milioni 18, ndiyo maana shilingi bilioni 4.2 za IMF zimeelekezwa hospitali ya
Bugando kwa ajili ya kufanya maendeleo kwenye huduma mbalimbali”, alisema Rais
Samia.
Alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Kanisa imeweza kuboresha
hospitali hiyo, ambapo hapo awali ilikuwa na vitanda 550 na sasa idadi ya
vitanda imeongezeka mpaka 950, ambavyo vitaweza kutoa huduma kwa wananchi
katika maeneo ya Kanda ya Ziwa, hiyo inaonyesha mwendelezo wa kutekeleza
makubaliano yaliyoingiwa kati ya Serikali na kanisa yanayoifanya Serikali kulipa
mishahara ya watumishi, ambapo wastani wa shilingi bilioni 20 hutolewa kila
mwaka kwa watumishi 1200 walioajiriwa na Serikali.
Rais Samia aliongeza kuwa katika kuhakikisha dawa zinapatikana
katika hospitali hiyo, Serikali
imeendelea kutoa ruzuku ya dawa kwa wastani wa shilingi bilioni moja kila mwaka na
kufanya upatikanaji wa dawa kuwa mkubwa katika hospitali hiyo ambayo kwa sasa
inahudumia kama Hospitali ya Kanda ya Ziwa kwa ushirikiano wa Kanisa na
Serikali na kuwezesha kutanua huduma tofauti na hapo awali.
“Miaka 50 ya Bugando tumetanua wigo wa huduma zinazotolewa
ukilinganisha na huduma zilizokuwa zinatolewa hapo awali na hivyo kupelekea
Serikali kuipa hospitali hii hadhi ya kuwa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa”, Alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia alisema kuwa katika miaka 50 ya Bugando Serikali
ikishirikiana na Kanisa imeendelea kujikita katika kuhakikisha inasogeza huduma
za kibingwa na huduma bobezi karibu zaidi na wananchi hasa Kanda ya Ziwa ambapo
kwa sasa Hospitali hiyo inahudumu kwa wananchi wa mikao minane yaani Mwanza,
Kagera, Kigoma, Geita, Shinyanga, Mara, Kagera na Tabora.
Aliongeza kuwa katika kutekeleza majukumu ya kuimarisha afya kwa
wananchi Serikali imeendelea kuchangia ujenzi wa wodi za wagonjwa wa saratani
ambapo tayari imetoa shilingi bilioni moja kwa bajeti ya mwaka 2021 na alitoa
wito kwa wataalam wa afya kujikita zaidi katika tafiti zinazobaini sababu na
chanzo cha saratani kwa wanawake hasa Kanda ya Ziwa.
“Miaka 50 ya Bugando ninatoa wito kwa watalaam wa afya kupunguza
kasi ya maradhi yasiyoambukiza ikiwemo kansa, fanyani tafiti na kujikita zaidi
katika kwenye saratani hasa kwa maeneo ya kanda ya ziwa kwani wanawake wamekuwa
wakiathirika sana na kansa ya kizazi na matiti”, Alisisitiza Rais Samia
Rais Samia alisema serikali iliahidi kugharamia ujenzi wa vyumba
vya kuhifadhia mashine za kutolea tiba ya mionzi 6 zilizogharimu shilingi
bilioni 5.5 kwa ajili ya kufungua mitambo ya tiba ya saratani, lakini pia
itahakikisha kuwa ujenzi wa wodi ya
wagonjwa wa saratani unakamilika kwa wakati ili huduma ziweze kupatikana kwa
Wananchi haraka na kwa wakati.
Akizungumzi maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania, Rais
Samia amewahimiza wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kujenga nchi
yao kama ilivyokuwa kwa Serikali zote tano tokea awamu ya kwanza zimekuwa
zikihimiza kufanya kazi, amesema miaka 60 ya uhuru watanzania waendelee kuchapa
kazi katika maeneo yao ili kujenga uchumi wa nchi.
Kwa upande wa huduma za kijamii hususani upatikanaji wa maji na umeme, Rais Samia amewataka
watanzania kuacha kuvamia maeneo yenye vyanzo vya maji ili kuwezesha
uzalishwaji wa maji kuwa mkubwa na kuwezesha upatikanaji wa maji katika maeneo
mbalimbali hasa yale ya mjini akitolea mfano Dar es Salaam kubwa mkubwa na
kufanya mgao wa huduma hiyo kupungua kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee
na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa Bugando imekuwa mshirika mzuri
katika kutoa huduma za afya kwa kushirikiana na Serikali na miaka 50 ya
maadhimisho haya ni miaka ya uhakika wa utoaji huduma za kibingwa kwa wananchi
wa kanda ya ziwa.
“Hospitali hii imekuwa ikishirikiana na Serikali miaka mingi na
imepiga hatua kubwa kufikia hapo tulipo sasa, tayari wewe Mhe. Rais unaendeleza
ushirikiano huo ambapo Serikali yako imetoa fedha za kitanzania Shilingi
Bilioni 4.2 zimeelekezwa hapa kwa ajili ya maendeleo katika mambo ya Oksijeni,
jengo wa wagonjwa wa dharula pamona na MRI na leo umezindua mashine mpya ambayo
itasaidia kutoa matibabu ya kibingwa na kupunguza gharama kwa wananchi”, alisem
Dkt. Gwajima.
Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu, Mwanza Leonard Nkwande alisema kuwa
Hospitali ya Bugando ikishirikiana na Serikali inaendelea kutoa huduma za
Kibingwa na Bobezi kwa wananchi wa maeneo mbalimbali hususani kwa maeneo ya
kanda ya Ziwa.
“ Katika Miaka 50 ya Bugando, tunaona hospitali hii inavyoendelea
kutoa huduma za za kibingwa kuhakikisha wananchi wanapata Afya bora ili waweze
kujenga taifa, tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika
kuhakikisha tunafanya kazi iliyonzuri”, Askofu Mkuu Nkwande.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni