DIWANI WA KATA YA SARANGA AIBUKA NA FURSA MPYA YA TAKATAKA KUWA MBOLEA, ATOA NENO HILI KWA WAKAZI WA KATA YAKE.
Wajasiriamali wa kata ya Saranga wametakiwa kujiunga katika vikundi ili waweze kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotengwa na halmashauri ya manispaa ya Ubungo.
Diwani wa kata ya Saranga Mh. Edward Laizer akitoa ufafanuzi wa jambo mapema jana mkoani Dar es salaam. |
Hayo yameelezwa mapema Jana mkoani Dar es salaam na Diwani wa kata ya Saranga Mh. Edward Laizer katika kikao Cha dhararura Kati yake na wajasiriamali wa kata hiyo.
Diwani huyo amesema kuwa dhumuni kubwa la yeye kukutana na wajasiriamali wa kata hiyo ni baada ya wao kama viongozi wa kata ya Saranga kupewa mafunzo ya siku mbili na shirika la TGNP, ambapo mafunzo hayo yaliwataka kushinikiza bajeti wanayoitenga iweze kuwa na mlengo wa kijinsia lakini pia walipewa mafunzo kuweza kuwezesha jamii kujipatia kipato kupitia rasilimali zinazowazunguka.
Ameongeza kuwa yeye kama kiongozi wa kamati ya maendeleo ya kata ni jukumu lake kuhakikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanazitumia vizuri fedha za halmashauri na ndio maana amewapa somo lakini pia na mbinu nzuri za kutumia ili kuweza kunufaika nafedha hizo.
"Na ndio maana nimeanza na fursa ya takataka kwa kuwa taka zimekuwa ni changamoto kubwa ndani ya jamii yetu na hata taifa kwa ujumla, lakini kwa sisi Saranga tutaigeuza changamoto hiyo kuweza kuwa fursa, kwani tutakusanya taka kutoka sehemu mbalimbali za kata yetu na tutazigeuza kuwa mbolea ya Mboji ambayo itatupatia kipato sisi kama wakazi wa kata ya saranga". amesema Diwani Laizer
Aidha ameendelea kusema kuwa watakapo kusanya taka hizo watatafuta sehemu ya wazi ili waweze kuzihifadhi taka hizo na kisha kuzifanyia uchambuzi kwa kutenganisha kati ya taka za pastiki ambazo zenyewe zitauzwa kama plastiki zingine, lakini zile ambazo zinafaa kutengenezewa mbolea zitatengeneza mbolea na hivyo watapata fedha kupitia mbolea, kuuza machupa ya plastiki pamoja na ada ya taka itakayotozwa kwenye kila kaya.
Ameendelea kwa kusema zoezi hilo litakuwa jumuishi kwa makundi yote yanayotakiwa kunufaika na huduma za mikopo ya halmashauri bila kuwagawanya kati ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuweza kuleta nguvu ya pamoja na kuhakikisha kata yetu ya Saranga inakuwa safi na mfano wa kuigwa na kata zingine,
Ameongeza kuwa yeye yupo tayari kujitolea eneo pamoja na mikokoteni kwa ajili ya kukusanya taka hizo lakini pia halmashauri ipo tayari kutoa mkopo hata wa gari kwa ajili ya wajasiriamali hao, hivyo kinachotakiwa ni utayari wao pamoja na moyo wa dhati wa kuweza kufanya kazi hiyo.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni