Zinazobamba

Simba SC yaitaja Arsenal Ikizindua Vikalagosi vyake vya msimu wa 2021/2022

 

 



Timu ya Simba SC imezindua Karagosi (Mascot) na kuipa jina la MO Rafiki, ambao watatumika kusherehesha Mashabiki wake pindi timu hiyo inapokuwa Uwanjani katika michezo yake mbalimbali sambamba na kampeni zake za kutoa misaada kwa makundi maalum.

Hiyo ni moja ya tamaduni zinazofanywa na Klabu zingine dunia katika kusherehesha mashabiki wake, kuwapa hamasa na kuleta umoja katika Soka.

Simba Sc wataanza kuwatumia vikaragosi hivyo kuanzia msimu ujao wa mashindano wakianza na Simba Day, 19 Septemba 2021.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Barbara Gonzalez amesema lengo la kuja na ‘Mascot’ hao ni kugusa maisha ya watu, kuleta furaha kila sehemu timu inapokuwa ikicheza na hata kwenye kampeni zake mbalimbali.

Barbara amesema, “Tunaona timu zilizoendelea ulimwenguni, timu za Arsenal, Manchester United, Everton na nyingine, zinafanya ubunifu kama huu ili kuleta hamasa, umoja kwa mashabiki na hata kwa Wachezaji wanakuwa na furaha wakiwaona ‘Mascot’ hao.

“Nakumbuka Mesut Özil alijitolea kumlipa Mascot wa timu ya Arsenal baada ya kutangazwa hali ya ukata kipindi cha Corona. Tunaona umuhimu wa Mascot hadi Wachezaji walitaka asiondoke ndani ya Klabu”, ameeleza Barbara.

Simba SC inajiandaa na tamasha lake la Simba Day, Septemba 19, 2021 ambapo itacheza mchezo wa kirafiki na Kabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Tamasha hilo litaenda sambamba na utambulisho wa Kikosi chake cha msimu wa 2021-2022.

 

Hakuna maoni