Zinazobamba

Puma, Selcom, Sanlam na Tanmanagement insuarance brokers zakubaliana kuanzisha bima ya ajali na maisha

 







Wakurugenzi wa makampuni ya Puma energy Tanzania, Selcom Tanzania, Sanlam pamoja na Tanmanagement Insurance Brokers Limited wakisaini mkataba wa makubaliano ya kuanzisha huduma ya Bima ya ajali na maisha ambayo italenga kuinua sekta ya soko la bima Tanzania.Kuuanzia kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Sanlam Tanzania Bw.Khamis Suleiman,Mkurugenzi Mtendaji wa Selcom Tanzania Bw.Sameer Hirji Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mafuta ya PUMA Energy Tanzania Bw.Dominic Dhanah na Mkurugenzi Mtendaji wa TanManagement Insurance Brokers Limited Bw.Mohammed Jaffer.



Kampuni ya Puma Energy Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Selcom Tanzania, Sanlam pamoja na kampuni ya Tanmanagement Insurance Brokers Limited wamezindua bidhaa ya kipekee ya Bima ya ajali na maisha ambayo italenga kuinua sekta ya soko la bima Tanzania.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mafuta ya PUMA Energy Tanzania Bw.Dominic Dhanah amesema kwa kutumia bidhaa hiyo wateja wote watakaolipia mafuta kuanzia shilingi 10,000/= kupitia Selcom Pay Mastercard QR au kadi ya puma kwenye vituo vya Puma Energy vya Dar es Salaam watapokea bima ya ajali na maisha itakayotumika ndani ya siku saba.

Amesema kupitia makubaliano hayo wanategemea kupata watumiaji wa huduma hiyo wengi hasa kutokana na huduma hiyo kuwa bora na kuwajari wateja wao ambao hutumia huduma hiyo.

“Sikuzote Kampuni hii imekuwa ikijitahidi kushirikiana na makampuni yenye mtazamo kama wetu kuboresha ubora wa huduma zitolewazo kwa wateja wetu. Amesema Bw.Dhanah.

Aidha amesema kuwa huduma hizo za bima ya maisha kwa wateja wao ni moja ya jitihada chanya.Kupitia mpango huo wateja wataweza kupata bima ya maisha bila ya gharama ya ziada, watakachotakiwa kufanya ni kulipia mafutta yao kidigitali kupitia mfumo wa selcom.

“Huduma hii ina akisi maudhui ya kampuni yetu ambayo ni kuchagiza maendeleo chanya kwenye jamii zinazotuzunguka. Kinga ya bima hii itatolewa wakati halisi na haina kipindi cha kusubiri”. Amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Selcom Tanzania Bw.Sameer Hirji amesema  mchakato huo utatumia teknolojia ya kisasa kuhakikisha kwamba wanafikia lengo la kufikisha huduma ya Bima kwa watu wengi iwezekanavyo.

“Selcom inakuja ikiwa na kanzidata ya wateja katika ncha ya chini kabisa ya mnyororo, jambo linalotoa nafasi kwa juhudi za wadau wetu kufikia wateja hawa bila gharama ya ziada”. Amesema Bw.Hirji.

Pamoja na hayo Bw.Hirji amesema ushirikiano wao na Sanlam,Puma na TanManagement unathibitisha wajibu wa viongozi katika sekta husika kwenye kuhakikisha ulinzi wa jamii na uboreshaji wa ustawi wa wateja na jamii nzima kwa ujumla.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Sanlam Tanzania Bw.Khamis Suleiman amesema kupitia makubaliano hayo wanatafsiri kwa vitendo maelekezo ya Wizara ya Fedha na Mamlaka ya usimamizi wa bima ya kufikia lengo la asilimia 50% ya watu wazima walio na angalau aina moja ya ya Bima ifikapo mwaka 2028.

Amesema malengo hayo pia yana dhamira ya kupunguza umasikini kwa kutoa fidia kwa wale walioathirika na hakutakuwa na gharama zozote za ziada kwa mbima katika utaratibu huo.

Vilevile nae Mkurugenzi Mtendaji wa TanManagement Insurance Brokers Limited Bw.Mohammed Jaffer amesema dira yao ni kupanua huduma hiyo vituo vingine vya mafuta na pia kulenga maeneo mengine ambayo yatamnufaisha mteja.

 

Hakuna maoni