Zinazobamba

TMA YATANGAZA YA HATARI,YASEMA MVUA KUBWA KUNYESHA NCHINI,SOMA HAPO KUJUA

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), imetoa tahadhari ya kuwepo vipindi vifupi vya mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba.

TMA iliyo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imesema hayo katika taarifa ya utabiri wa hali ya hewa kwa saa 24 zijazo kuanzia saa tatu usiku wa leo Novemba Mosi, 2017.

Mamlaka imesema mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Tanga na Pwani, na visiwa vya Unguja na Pemba itakuwa na hali ya mawingu, mvua na ngurumo katika baadhi ya maeneo na vipindi vifupi vya jua.

Imesema mikoa ya Kagera, Geita, Lindi na Mtwara itakuwa na hali ya mawingu kiasi, mvua na ngurumo katika maeneo machache na vipindi vya jua.



Katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Ruvuma, TMA imesema kutakuwa na hali ya mawingu kiasi, mvua katika maeneo machache na vipindi vya jua.

Taarifa ya Hali ya Hewa imesema mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Katavi na Kigoma kutakuwa na hali ya mawingu kiasi, ngurumo katika maeneo machache na vipindi vya jua.

Kwa mikoa ya Singida, Dodoma, Kilimanjaro Arusha na Manyara, TMA imesema kutakuwa na hali ya mawingu kiasi na vipindi vya jua.

Kuhusu upepo wa Pwani, TMA imesema  unatarajiwa kuvuma kutoka Kusini Mashariki; kwa kasi ya kilomita 30 kwa saa kwa pwani yote.

Mamlaka imesema hali ya bahari inatarajiwa kuwa na mawimbi makubwa kiasi.