Zinazobamba

MAMILIONI YA FEDHA KUTUMIKA KWENYE UCHAGUZI MDOGO WA MADIWANI,SOMA HAPO KUJUA


Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika Novemba 26,2017 katika kata 43 utagharimu Sh2.5 bilioni.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhani amesema msingi wa bajeti ya uchaguzi unategemea idadi ya vituo vya kupigia kura na idadi ya wapiga kura walioandikishwa katika kata husika.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari leo Novemba Mosi,2017 Kailima amesema idadi ya wapiga kura ndiyo inatoa bajeti ya mahitaji ya vifaa vya kuendeshea uchaguzi kama vile karatasi za kura na idadi ya vituo ambavyo vinakuwa na watumishi wasiopungua wanne.

Amesema kituo cha kupigia kura kina watendaji wanne ambao ni msimamizi na msimamizi msaidizi, karani mwongozaji na mlinzi wa kituo.

“Lakini pia kuna watu wa ziada kama wasimamizi wasaidizi wako ngazi ya kata na jimbo ambao wanahusika kusimamia uchaguzi katika maeneo husika,” amesema.

Amesema gharama nyingine za uchaguzi ziko kwenye usafirishaji wa vifaa kutoka Tume kwenda kwenye halmashauri husika na kutoka halmashauri kwenda kwenye kata ambako uchaguzi unafanyika.  “Gharama hizo pia zinahusu utoaji wa elimu ya mpiga kura kupitia machapisho mbalimbali ya elimu ya mpiga kura, maelekezo kwa watendaji wa uchaguzi,” amesema.

Amesema elimu pia hutolewa kupitia vyombo vya habari na machapisho yatakayotumika kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura.

“Kwa uchaguzi huu mdogo bajeti ni Sh2.5 bilioni. Si kwamba kila kata itatumia gharama sawa za fedha hizi, bali kuna kata itatumia Sh20 milioni kutokana na idadi ya vituo vya kupigia kura kuwa vichache na kata yenye vituo vingi kwenye uchaguzi huu itatumia Sh150 milioni,” amesema Kailima.

Kailima amesema vyama vya siasa vinatakiwa kuhakikisha vinawaelimisha wafuasi, wapenzi na wanachama wao juu ya kutekeleza maadili katika kipindi chote cha kampeni.

Amesema maadili yatakiukwa, chama husika pamoja na mgombea watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Kailima amesema baadhi ya vitendo vya kuvunja maadili ya uchaguzi ni kuchana mabango ya wagombea, kutoa lugha chafu wakati wa mikutano ya kampeni na kupitisha muda wa kufanya mikutano ya kampeni.

Amesema kamati za maadili za kata na jimbo zitachukua hatua kali kwa chama au mgombea ambaye atakiuka maadili na kwamba, zinatakiwa kuchukua hatua ndani ya saa 48 baada ya chama au mgombea anapovunja maadili.

Amezitaja baadhi ya adhabu ni kuomba radhi wananchi hadharani, kutotumia vyombo vya habari kwa muda fulani wakati wa kampeni, onyo la maandishi, kusimamishwa kufanya kampeni, mgombea kutangaza mbele ya vyombo vya habari kuwa yeye ni bingwa wa kukikuka maadili ya uchaguzi au kutozwa faini ya Sh100,000.

Mwananchi: