Zitto Kabwe Aikomalia Serikali...... Aomba jumuiya za kimataifa kuchunguza kasi ya ukuaji uchumi nchini
Chama cha ACT Wazalendo kimeziomba Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Dunia (WB) kufanya uchunguzi maalumu wa takwimu za kasi ya ukuaji wa uchumi ya robo ya pili ya mwaka na kuchukua hatua endapo itabainika kile anachodai kuwa Serikali ilipika takwimu.
Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe ametoa msimamo wake huo leo Jumamosi jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari.
Zitto amedai chama hicho kimebaini takwimu zilizotolewa na Serikali za Aprili hadi Juni haziko sahihi.
Amedai takwimu za Serikali zinaonyesha kasi ya ukuaji wa uchumi katika robo ya pili ya mwaka ni asilimia 5.7, tofauti na za ukokotozi kwa kanuni za kiuchumi anazodai zinaonyesha ni asilimia 0.1.
"Hatujatafuta takwimu nyingine, hizi ni taarifa zilezile zilizotolewa na BoT na NBS lakini ukikokotoa utaona uchumi tulionao unasinyaa badala ya kukua na hali ikiendelea hivi hadi Juni 2018 kutakuwa hakuna uchumi Tanzania," amedai Zitto.
Amedai sababu hiyo inachangia maisha ya Watanzania kuendelea kuwa magumu ilhali Serikali imekuwa ikitoa taarifa za uchumi kukua.
Zitto amegusia pia takwimu za mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akidai nazo haziko sahihi.
Amesema ni vyema wakati TRA ikitoa takwimu zake ikaeleza mapato kwa kila idara bila kuchanganya marejesho na madeni ambayo hayajalipwa.
"Taarifa yao ieleze kinagaubaga mapato ya idara ya forodha, walipa kodi wakubwa na walipa kodi za ndani. Wasiishie hapo, kati ya fedha wanazotaja kukusanya iwekwe wazi madeni na marejesho ni yapi tofauti na inavyofanywa sasa," amesema.
Zitto ametaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa mapato ya Serikali ya Julai na Agosti na kuweka wazi taarifa hiyo.