Zinazobamba

MBUNGE LEMA NA HECHE WAMCHARUKIA JPM,NI BAADA YA KUMPANDISHA CHEO DC MNYETI WA MADIWANI,SOMA HAPO

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Godbless Lema wa Arusha Mjini na John Heche wa Tarime vijijini wameshangazwa na hatua ya Rais John Magufuli kumteua aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Arumeru Alexander Mnyeti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Kwa nyakati tofauti wabunge hao kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii wameonesha kukosoa hatua hiyo kutokana na kwamba Mnyeti bado anakabiliwa na tuhuma ya kununua kwa kuwahonga madiwani wa Chadema Mkoani Arusha na kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM) suala ambalo bado lipo chini ya uchunguzi wa Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru)

Kupitia ukurasa wa twitter Heche amesema “Unasema unapiga vita rushwa na ufisadi mtu anatuhumiwa kufanya vitendo vya rushwa bado anachunguzwa unampromote! Unatuma mesegi gani Takukuru?,”

“Ni wazi sasa kwamba nchi hii ni mali ya mtu mmoja akimtaka mtu hata kama ni mchafu kiasi gani sawa na kama hakutaki ukiwa msafi utachafuliwa,” ameongeza.

Kwa upande wake Lema kupitia ukurasa wake wa twitter amesema Takukuru walipewa ushahidi wakasema ni ushahidi mgumu lakini DC Mnyeti mwenyewe alitoa ushahidi kwa kusema kuwa amenunua madiwani wengine Zaidi ya 20.

Ameeleza kuwa mtua hawezi kuonyesha ujasiri kama huo kwenye suala nyeti kama hilo na bado akabaki kazini.

“Kuna watu katika taifa hili hata wakiua hadharani hawaguswi ila kuna wengine wanaobambikizwa makosa,” amesema Lema.

Aidha ameongeza kuwa Mnyeti anatuhumiwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari (Chadema) kuwa ameshiriki kununua madiwani 10 wa Chadema kwa rushwa na kuwasilisha ushahidi Takukuru.