Zinazobamba

SAKATA LA MRISHO GAMBO NA WAANDISHI LATUA BUNGENI,SOMA HAPO KUJUA



NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura, amesema suala la waandishi wa habari kuzuiwa kufanya kazi zao na baadhi ya watu, amelisikia bungeni kwa mara ya kwanza.

Hata hivyo, alisema anaamini kuwa kama waandishi wanafuata maadili katika kazi zao na wanatafuta habari kwa ajili ya kujenga na si kuvuruga nchi, haamini kama kuna watu wanaoweza kuwazuia.

Wambura alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Devotha Minja.

Katika maswali yake, Minja alihoji serikali inawachukulia hatua gani watu wanaozuia waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kama ilivyojitokeza hivi karibuni kwa kuwapo matukio ya baadhi ya waandishi wa habari kuzuiwa kufanya kazi zao.

“Kama vile ilivyotokea hivi karibuni kwa kiongozi mmoja kuvamia kituo cha televisheni, baadhi ya waandishi kuvamiwa wakiwa kwenye mkutano wa CUF, baadhi ya wakuu wa wilaya kuwakamata waandishi wa habari na kuwaweka ndani na hata jana (juzi) kule Arusha katika Shule ya Msingi ya Lucky Vicent waandishi wa habari 10 walikamatwa wakiwa wanatimiza majukumu yao,” alisema.

Alihoji: “Ni lini serikali itaacha tabia hii mbaya ya kuwakamata kamata waandishi wa habari wakiwa kwenye majukumu yao?”

Akijibu maswali hayo, Wambura alisema Sheria ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 inasema kazi ya uandishi wa habari ni kazi ya kisheria.

“Lakini anavyosema kwamba kuna watu wanazuiwa kufanya kazi zao, naamini kuwa kama kweli waandishi wanafuata maadili katika kazi zao na wanatafuta habari kwa ajili ya kujenga na si kuvuruga nchi, siamini kama kuna watu wanaoweza kuwazuia,”alisema Wambura.

Alifafanua kuwa Sera ya Habari na Utangazaji inahimiza kwamba taasisi zote za serikali na wadau wote wa habari wanatakiwa kutoa taarifa kwa wanahabari.

“Sera inahimizwa wale maofisa habari katika mikoa na halmashauri wawe tayari kutoa ushirikiano kwa wanahabari ili watekeleze majukumu yao. Sasa kama kuna hili la watu wanaozuia mimi naomba baadaye tuonane na Mheshimiwa Mbunge maana ndiyo kwanza nalisikia hili,” alisema.

Hata, hivyo alisema kuhusu swali la pili Waziri (Dk.Harrison Mwakyembe) alishatolea ufafanuzi wakati anahitimisha hotuba yake ya bajeti bungeni hivyo hataweza kulijibu.

Katika swali la msingi, Minja alihoji ni lini serikali itaanzisha mfumo utakaotambua kazi zinazofanywa na tasnia ya habari.

Akijibu swali hilo, Wambura alisema serikali inatambua na kuthamini kazi zinazofanywa na vyombo vya habari nchini na kwamba mchango wa tasnia hiyo ni mkubwa katika kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii.

Alisema serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuwezesha wanahabari kufanya kazi zao kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu ili kulinda amani na utulivu katika nchi