ENEO LA LEBANON SOKO LA SAMAKI LA FERRY JIJINI DAR ES SALAAM KINARA KWA UKATILI WA KIJINSIA
Mwenyekiti wa Soko la Kimataifa la Samaki la Ferry, Ali Bunda akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), Dar es Salaam juzi wakati akitoa taarifa ya kupungua kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika soko hilo, baada ya kupata mafunzo kutoka Shirika la Equality for Growth (EfG). Bunda alilitaja eneo la Lebanon katika soko hilo kuwa ni hatari kwa ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto.
Katibu Mkuu wa Soko la Temeke Sterio, Omari Mangilile, akizungumzia kupungua kwa ukatili katika soko hilo.
Mkuu wa Ulinzi na Usalama wa Soko la Temeke Sterio AP 1248 Koplo Chaurembo Shomari, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), Dar es Salaam jana, kuhusu kampeni zilizofanywa na Shirika la Equality for Growth (EfG) za kupinga ukatili wa jinsia katika soko hilo kuwa zimesaidia kupunguza makosa hayo ambapo kwa mwezi Septemba mwaka jana yalikuwa 21 lakini sasa hakuna kabisa.
Mfanyabiashara katika Soko la Temeke Sterio, Robert Kalawila akizungumza na wanahabari.
Mwezeshaji Sheria Soko la Ferry, Fatma Ally akizungumza.
Mfanyabiashara katika Soko la Temeke Sterio, Mariam Juma 'maarufu Mama Kondo' akizungumzia kupungua kwa vitendo hivyo.
Mwezeshaji wa kisheria katika Soko la Temeke Sterio, Augenia Gwamakombe (katikati), akizungumza. Wengine ni wafanyabiashara wenzake.
Mfanyabiashara Tamasha Amri akizungumza.
Mfanyabiashara katika Soko la Temeke Sterio, Vicky
Mbogela akichangia jambo.
Mfanyabiashara, Lushenia Emanuel akijieleza kwa wanahabari.
Muonekano wa Soko la Samaki la Kimataifa la Ferry.
Na Dotto Mwaibale
ENEO la Lebanon katika Soko la Kimataifa la Samaki la Ferry jijini Dar es Salaam limeelezwa kuwa ni kinara kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto.
Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa soko hilo Ali Bunda alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana wakati akitoa taarifa ya kupungua kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika soko hilo baada ya kupata mafunzo kutoka Shirika la Equality for Growth (EfG).
"Vitendo vya ukatili wa kijinsia vimepungua kwa kiasi kikubwa katika maeneo mengine ya soko letu lakini changamoto kubwa ipo eneo la Lebanon huko ukipita usiku unaweza kulia kutokana na vitendo vinavyofanyika" alisema Bunda.
Alisema katika eneo hilo kila vitendo vichafu vimekuwa vikifanyika kwani hivi karibuni kuna mwanaume mmoja alikamatwa baada ya kubambwa akimnajisi mtoto wa kiume lakini alipofikishwa kituo cha polisi mtoto huyo aliomba mwanaume huyo asipelekwe mahakamani kwani alikuwa ni msaada mkubwa kwake kutokana na kupewa fedha za chakula na mahitaji mengine.
"Kauli ya mtoto huyo ilimshitua kila mtu aliyekuwepo kituoni hapo ambapo pamoja na kuomba aachiwe polisi waliendelea kumshikilia ili sheria ichukue mkondo wake" alisema Bunda.
Katibu Mkuu wa Soko la Temeke Sterio, Omari Mangilile alisema ushirikiano baina ya wafanyabiashara, viongozi wa soko pamoja na Shirika hilo na Jeshi la Polisi Kituo cha Chang'ombe kumesaidia kupunguza vitendo vya ukatili wa jinsia katika soko hilo.
Mkuu wa Ulinzi na Usalama wa Soko la Temeke Sterio AP 1248 Koplo Chaurembo Shomari alisema kampeni zilizofanywa na EfG kupinga ukatili huo zimesaidia kupunguza makosa hayo ambapo kwa mwezi Septemba mwaka jana yalikuwa 21 lakini hadi kufikia sasa yamepungua na kufikia mawili na katika baadhi ya miezi mingine yakiwa hayapo kabisa.