PROFESA LIPUMBA AZIDI FUKUZA VIONGOZI NDANI YA CUF,AWATIMUA VIONGOZI HAWA,SOMA HAPO KUJUA
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF)
anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba
leo ametengua uteuzi wa wakurugenzi watano ambao ni wajumbe wa Kamati ya
Utendaji Taifa ya chama hicho kutoka Zanzibar. Kwa madai ya kutoitikia wito wa
kuhudhuria kikao cha kamati hiyo Machi 6, 2017 kilichoitishwa na Naibu Katibu
Mkuu Bara wa CUF, Magdalena Sakaya.
Wakurugenzi waliodaiwa kutenguliwa uteuzi wao ni
pamoja na, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Omar Shehe, Mkurugenzi wa Habari,
Uenezi, Mawasiliano na Umma Salim Bimani, Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi
Abdallah Hassan,Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria Pavu Abdallah na
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Vijana CUF (JUVICUF) Mahmoud Mahinda.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoa tamko
la kutengua uteuzi wa wakurugenzi hao, Prof. Lipumba amedai kuwa atateua
wakurugenzi wengine kabla ya wiki hii kuisha, ili Sakaya aitishe kikao kingine
cha kamati kuu ya utendaji kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mkutano wa Baraza
Kuu la Uongozi.
Licha ya kutengua uteuzi wa wakurugenzi hao, Lipumba
amedai kumuweka kiporo Naibu Katibu Mkuu CUF Zanzibar Nassoro Mazrui kwa madai
ya kutotoa ushirikiano kwa Naibu Katibu Mkuu Bara licha ya kutambua kwamba ni
kiongozi wake halali kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.
“Sakaya amewatumia ujumbe wa simu wakurugenzi wote wa Tanzania
Bara wamehudhuria mwengine alikuwa na ziara na Rais John Magufuli Mtwara lakini
aliaghirisha akaja, kitendo cha wengine kutofika baada ya kupewa taarifa,
siwezi kukubali. Sakaya namuagiza mimi halafu wakurugenzi hawaji na hawatoi
taarifa yoyote? lazima wawe tayari kufanya kazi na katibu mkuu na manaibu
katibu mkuu wote,” amesema Lipumba.
Chanzo changu kilimtafuta mmoja wa wakurugenzi
aliyedaiwa kuvuliwa madaraka yake, na kufanikiwa kumpata Mkurugenzi wa
Habari Salim Bimani ambaye alidai kuwa yeye pamoja na wenzake hawatambui
maamuzi hayo ya Lipumba kwa madai kuwa si mwenyekiti halali kwa mujibu wa
katiba ya CUF kwa kuwa alijiudhuru sambamba na kufutwa uanachama na Baraza Kuu
la Uongozi Taifa la chama hicho.
“Hana uwezo wowote wa kututengua na hatumtambui, kwanza kuna kesi
mahakamani hivyo kila analolifanya ni batili hadi pale mahakama itakapo toa
maamuzi yake. Kwa sasa tunachofahamu ni kwamba anafanya maamuzi kwa masilahi
yake binafsi,” amesema Bimani.