NECTA yawasihi wananchi kuendelea kuwapa taarifa kuhusu watumishi walioghushi au kutumia vyeti vya watu wengine.
Na Eleuteri Mangi, MAELEZO
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) linaendelea
kuwatangazia wananchi kuendelea kuwapa ushirikiano kwa kutoa taarifa mbalimbli
ikiwemo taarifa kuhusu watumishi walioghushi au kutumia vyeti vya watu wengine.
Tangazo hilo limetolewa na NECTA kupitia mtandao
wake www.necta.go.tz hatua ambayo inaendeleza juhudi za kuwafichua watumishi
ambao wanatumia vyeti ambavyo sio vyao.
Kwa mujibu wa tangazo hilo NECTA imewataka wananchi
wenye malalamiko au taarifa kuhusu watumishi walioghushi au kutumia vyeti vya
watu wengine kuwasiliana nao kupitia barua pepe esnecta@necta.go.tz au simu
namba +255 742 484 955.
Wananchi wametakiwa kufikisha malalamiko au taarifa
hizo kwa kuzingatia muda wa saa za kazi kuanzia saa 2:30 Asubuhi hadi 10:30
jioni kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa.
Aidha, tangazo hilo limesisitiza kuwa kwa msaada
zaidi wananchi wawasiliane nao kupitia barua pepe helpdesk@necta.go.tz au simu
namba 0658 116 644 kwa saa za kazi.
Tangazo hilo linaendelea kutoa msisitizo kufuatia
agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
alilolitoa kwa Wakuu wa Mikoa Machi 15, 2016 la kuhakiki watumishi wa Umma na
kuwaondoa watumishi hewa ambao wamekuwa mzigo kwa Serikali yake.