Zinazobamba

UGENI TENA WA MARAIS NCHINI,SOMA HAPO KUJUA



Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni anatarajiwa kufanya ziara ya siku mbili nchini kuanzia Jumamosi wiki hii.

Taarifa hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na  Ushirikiao wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga wakati wa mkutano  na waandishi wa habari.

Alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni  kuendeleza uhusiano mzuri uliopo baina ya Uganda na Tanzania, pamoja na  kujadili masula mbalimbali ya kikanda, kimataifa na sekta mbalimbali  za ushirikiano kati ya nchi hizi mbili hususani katika sekta za nishati, biashara na uchukuzi.

“ Mahusiano ya kibiashara kati ya  Tanzania na Uganda yameendelea kuimarika katika miaka ya hivi karibuni,
ambapo mwaka 2016 Tanzania ilifanya mauzo nje kwa Nchi hiyo ya kiasi  cha shilingi bilioni 66.849, ikilinganishwa na shilingi bilioni 78.31  za mwaka 2015” alisema Waziri Mahiga.

Aliongeza kuwa Uganda ni  muhimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo haina Bandari na hivyo  inategemea Tanzania kwa ajili ya kupitisha mizigo yake.

Nchi ya Uganda imezidi kuwa na umuhimu kufuatia uamuzi wa kupitisha bomba la  mafuta nchini Tanzania, kutoka Kabaale –Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga, ambapo bomba hilo lina urefu wa kilimeta 1443 na kipenyo cha  inchi 24.Bomba hilo la mafuta litakalokamilika mwaka 2020 limnatarajiwa kupatia nchi hizi mbili fursa mbalimbali.

“Utekelezaji wa mradi huu utafungua fursa za ajira kwa watanzania, kuchochea shughuli za kiuchumi kwa mikoa inayopita bomba hilo, pamoja na kufungua ukanda wa biashara wa kaskazini mwa Tanzania na Uganda pamoja  na kuimarisha uhusiano katika soko la Afrika Mashariki” alifafanua
Waziri Mahiga.

Katika hatua nyingine, Waziri Mahiga alisema kuwa
kuhusu mgogoro wa nchini Burundi, kumekuwepo na jitihada mbalimbali  zinazofanywa na Rais Museveni pamoja na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa ili kuhakikisha amani
inarejea nchini humo.

Katika ziara hiyo ya Rais Museveni nchini,
atapokelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Johm  Magufuli ambapo atatembelea Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la  kuangalia maboresho yaliyofanywa katika bandari hiyo, pamoja na Kiwanda  cha kutengeneza Juisi cha Azam kilichopo Vingunguti jijini Dar es  salaam.