SERIKALI YATANGAZA UTARATIBU WA KUZIONDOA POMBE ZA VIROBA,SOMA HAPO KUJUA
Kufuatia kauli ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa aliyotoa tarehe 16/02/2017 huko Mererani,
Mkoani Manyara kuhusu kusitisha utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe
zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki kuanzia tarehe 1 Machi 2017; na
kufuatia Tamko la Serikali kuhusu dhamira hiyo lililotolewa Bungeni
tarehe 2 Mei, 2016 na kwenye matangazo yaliyotolewa kwenye vyombo vya habari
tarehe 01 Desemba, 2016, Ofisi ya Makamu wa Rais inachukua fursa hii
kutangaza utaratibu wa utekelezaji wa maamuzi hayo ya Serikali.
Waziri mwenye dhamana ya Mazingira atatunga Kanuni
zitakazodhibiti uzalishaji wa vifungashio (viroba) vya pombe kali, kwa mujibu
wa Kifungu 230 (2) (F) cha Sheria ya Mazingira ya Kanuni hizi
zitaweka sharti la kutaka pombe kali inayozalishwa viwandani zifungashwe kwenye
chupa zinazoweza kurejelezwa (recycled) na kwa ujazo usiopungua milligram 250.
Pia Kanuni hizo zitapiga marufuku uzalishaji,
uuzaji, uingizaji nchini na matumizi pombe zilizofungwa kwenye
viroba na mitambo ya malighafi ya vifungashio vya plastiki (viroba)
vitakavyotumika kufungashia pombe kali. Atakayebainika kukiuka
masharti ya Kanuni hizi atawajibishwa kulipa faini, kufungwa jela au vyote kwa
pamoja kama itakavyoainishwa kwenye Kanuni.
Dhamira ya Serikali sio kupiga marufuku vinywaji vya
pombe kali bali ni kutekeleza Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania 1977 ambayo inatoa haki ya kuishi katika mazingira yaliyo safi, salama
na yenye afya. Haki hiyo pia imetiliwa mkazo katika sheria ya Mazingira ya
2004. Hivyo, dhamira ya Serikali ni kudhibiti upatikanaji kwa urahisi
wa pombe kali kunakotokana na kufungwa katika plastiki na kwa ujazo mdogo,
kunakopelekea kuongezeka kwa matumizi ya pombe kali hadi kwa watoto wadogo;
kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na kuzagaa kwa vifungashio hivyo; na
kudhibiti ukwepaji mkubwa wa kodi kutokana na urahisi wa teknolojia na gharama
za kutengeneza pombe kali inayofungashwa kwenye viroba. Inakadiriwa
kwamba Serikali inapoteza shilingi bilioni 600 kwa mwaka kutokana na ukwepaji
kodi kwenye biashara ya pombe za viroba.
Utekelezaji wa maamuzi haya ya Serikali unaanza mara
moja. Ingawa haitegemewi, lakini iwapo kuna Wazalishaji watakaohitaji muda wa
ziada wa kuhamia kwenye teknolojia ya chupa, wataomba kibali maalum cha muda
mfupi ambacho hakitatolewa hadi muombaji awasilishe kabla ya tarehe
28/02/2017:- yafuatayo:-
Ushahidi/Barua kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) kwamba amelipa kodi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Ushahidi/Barua/Cheti kutoka Mamlaka ya Chakula na
Dawa (TFDA) kwamba mzalishaji amekuwa na kibali cha usalama wa kinywaji
kwa miaka yote ambayo amekuwa anazalisha;
Cheti au Barua kutoka Shirika la Viwango Tanzania
(TBS) kwamba mzalishaji anauza bidhaa inayokidhi viwango
Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) au
Ukaguzi wa Mazingira (EA) kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC)/Ofisi ya Makamu wa Rais;
Ushahidi kwamba katika kipindi cha mpito mzalishaji
atatumia teknolojia ya kudhibiti utengenezaji wa vifungashio bandia
(anti-counterfeit technology);
Uthibitisho kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na
Leseni (BRELA) kuhusu usajili wa kampuni na usajili wa chapa ya kinywaji
(brand).
Zipo pombe za viroba zinazoingizwa nchini kutoka nje
ya nchi, hasa kwenye Mikoa na Miji ya mipakani. Wakuu wa Wilaya , kupitia
Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Kamati za Mazingira, wanaelekezwa
kufanya operesheni ya kukamata na kuzuia viroba vinavyoingizwa nchini kinyume
cha utaratibu. Operesheni hii pia inahusu udhibiti wa pombe haramu ya gongo.
Serikali imeunda Kikosi Kazi cha Kitaifa kwa ajili
ya kufanya ukaguzi na ufuatiliaji na hatua hizi. Kikosi hicho
kinajumuisha Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara
ya Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji, Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Shirika la
Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya
Uhamiaji na Jeshi la Polisi. Doria za ukaguzi wa utekelezaji wa
hatua hizi zitaanza wakati wowote kuanzia sasa na hatua kali zitachukuliwa kwa
watakaokiuka. Ofisi ya Makamu wa Rais itaratibu Kikosi hiki.
Kuhusu mifuko ya plastiki, Kanuni za Udhibiti
zinaandaliwa na zuio litatangazwa wakati wowote. Tunapenda kuwaasa
wazalishaji, waagizaji na wauzaji wa mifuko hiyo nao kujiandaa.
Hatua hizi za Serikali sio za ghafla au kushtukiza
kwani taarifa ilitolewa Bungeni takribani mwaka mmoja sasa. Aidha Serikali
ilitoa taarifa rasmi mwezi Agosti 2016 na Desemba 2016 kuhusu dhamira ya
kuchukua hatua hizi. Serikali ilitarajia kwamba wazalishaji wa pombe za
viroba na mifuko ya plastiki watakuwa wamejiandaa kubadilisha teknolojia.
Ofisi ya Makamu wa Rais
20/02/2017